Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Samia Suluhu Hassan,anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya kilele cha siku kuu ya wafanyakazi duniani,Mei mosi mwaka huu yatakayofanyika kitaifa mkoani Arusha .

Rais wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi Nchini ( TUCTA) ,Tumaini Peter Nyamhokya, ameyasema hayo jijini Arusha alipokuwa akitoa taarifa ya maandalizi ya sherehe hiyo Kwa Vyombo vya habari.

Amesema sherehe za mei mosi kitaifa zitafanyika mkoani Arusha kwenye uwanja wa Shekh Amri Abeid .

Amesema kuwa katika maadhimisho hayo TUCTA inakumbusha Waajiri madai mbalimbali ya wafanyakazi wa Serikali na Sekta binafsi ambayo hayatekelezwa.


Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni “nyongeza ya Mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha “ amesema Nyamhokya.

Ameongeza kuwa , kauli mbiu hiyo inaendana na uhalisia wa maisha ya mfanyakazi kwa sasa kwani gharama za maisha zimepanda na Mishahara haikidhi mahitaji ya kila siku ya mfanyakazi.

Ambapo ameongeza kuwa, endapo Mishahara ikiwa bora itawezesha mafao kuwa bora wakati wa kustaafu ,hivyo basi wameona ni vyema kutumia siku hiyo ya sherehe za wafanyakazi kuikumbusha serikali na waajiri na waajiri wote umuhimu wa kuwa na Mishahara bora inayoendana na hali halisi ya maisha wakiwa kazini na baada ya kustaafu .

“Maadhimisho ya mei mosi mwaka huu yameratibiwa na vyama vyote 13 vinavyounda shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ambapo wameshirikiana pia na vyama vyote vilivyo nje ya TUCTA vilivyojitokeza katika maandalizi hayo” amesema.

Aidha aliongeza kuwa ,maadhimisho hayo yataenda sambamba na michezo mbalimbali ya meimosi yatakayofunguliwa rasmi April 21 ,2024 na Waziri wa kazi ,vijana ajira na watu wenye ulemavu Deogratious Ndejembi.

Aidha ametoa wito kwa wafanyakazi wote waliopo mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kujumuika kwa pamoja siku ya kilele katika maadhimisho hayo kitaifa kwa pamoja na kuienzi siku hiyo muhimu kwa wafanyakazi duniani.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya habari na matangazo mei Mosi, Jane Mihanji,amesema Serikali ni mwajiri namba moja hivyo vyama vya wafanyakazi vina wajibu wa kuzungumza na Serikali pia kuhimiza kufanya kazi kwa bidii na tija.