Na Magrethy Katengu–Jamuhuri Media Dar es salaam

Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itahakikisha inatoa elimu ya fedha kuanzia ngazi ya elimu msingi hadi vyuo vikuu ili kisaidia kuwawezesha vijana kuwa na Uelewa na Usimamizi wa fedha hata wanapopewa majukumu wa ya kusimamia fedha wawe na nidhamu ya hali ya juu.

Ameyasema hayo leo Aprili 17, 2024 jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akifungua warsha kuhusu uongezaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu iliyowakutanisha viongozi mbalimbali na taasisi na elimu ya juu nchini

Waziri Kipanga amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii kwani kufanya hivyo itakuleta chachu ya kupata wataalamu wazuri ambao watasaidia kupunguza upotevu wa fedha kiholela kama inavyoonekana katika Ripoti inayotolewa na Mkaguzi wa serikali kila inaposomwa.

“Wizara ya elimu ya fedha tutahakikisha inafundishwa katika mfumo wa elimu kuanzia msingi hadi vyuo vikuu ili twende kwa haraka na vijana ambao ni sehemu ya jamii nchini walio na uelewa wa masuala ya fedha hivyo natarajia wakuu wa vyuo mtabeba uelewa huu muhimu kwa vyuo vyetu nchini,” amesema Kipanga.


Sambamba na hayo waziri amesema BoT, itaendelea kusimama na vyuo na taasisi za elimu na Wizara ya Elimu katika kuhakikisha dhana ya elimu hiyo inakuwa endelevu na inafundishwa katika ngazi za jamii hata katika elimu zisizo rasmi.

Pia Waziri ameviagiza vyuo vikuu kushirikiana na BoT kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo ili kuleta tija ya kuboresha mbinu bora na nyenzo za kufikisha ujumbe huo kwa jamii.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipatiwe taarifa ya tathmnini mtakazofanya ili itusaidie katika kufanya maamuzi, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii,” amesema.

Naye Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo amesema elimu ya fedha kila mahali inatumika isipokuwa watu wanachukulia kawaida hivyo sasa watahakikisha inakuwa ni sehemu ya masomo yafundishwe ngazi zote na somo hilo litakaloingizwa kwenye mfumo ya elimu msingi hadi vyuo vikuu.

“Aprili mwaka jana, BoT tuliwashirikisha wakuu wa taasisi za Elimu ya Juu nchini, kwa uwakilishi wa wakuu wa vyuo vikuu pamoja na TCU na NACTIVET kwa lengo la kukubaliana juu ya azma ya kufundisha somo la elimu ya fedha ngazi ya elimu ya juu nchini” amesema Naibu Gavana.

“Hadi hivi sasa taasisi tatu za elimu ya juu zimechukua hatua za kuingiza somo la elimu ya fedha katika mitaala yao, hivyo warsha hii ni kuchochea uwepo wa elimu ya fedha kwa vyuo vingi nchini kuendana na mabadiliko ya mageuzi ya kiuchumi nchini,”amesema.

Gavana Sauda amesema takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 inaonesha takribani watu asilimia 34.5 ni vijana walio na umri kati ya miaka 15-35 hivyo ili kuleta tija na ufanisi katika masuala ya uchumi ujuzi na uzoefu wa masuala ya fedha ni moja ya sifa muhimu kufikia azma hiyo.

Hata hivyo amesema elimu ya fedha kwa Watanzania kutachochea maendeleo kwa kuongeza utumiaji rasmi wa huduma za fedha na kuwawezesha watu wengi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi kukuza uchumi kwa ujumla.

Sauda amesema elimu kwa vijana wa vyuo vikuu itawasaidia kuweka akiba, kupanga bajeti na kufanya uamuzi wa masuala ya fedha kwa kuzingatia viashiria hatarishi na kuelewa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za fedha ili kufanya maamuzi sahihi ya fedha ili waitawale.

” Tunatarajia kujenga ‘displine’ ya fedha kupitia elimu ya fedha kwani watakuwa na uwezo wa kutawala fedha sio fedha kuwatawala vijana hao,” amesema.

Pia amesema BoT kwa kushirikiana na wadau wengine wa Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha, imetoa muongozo na mtaala wa elimu ya fedha kwa wakufunzi ambao utatumika na taasisi za elimu ya juu kwa kuwafundisha watoa huduma za elimu ya fedha kuwafikia wananchi wote walio nje mfumo wa elimu.

“Tayari tumeingia makubaliano na baadhi ya taasisi zaa elimu katika mtaala huo wa kufunzi wa fedha na tulioingia nao makubaliano ni Chuo Kikuu cha Iringa, Zanzibar, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha(IFM) na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania ,” ameseama.

Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA), Felix Adam amesema warsha hiyo ni muhimu kwake kwa sababu hayo maeneo yanayojadiliwa yatawasaidia kuwapa elimu ya fedha wahitimu wao.

” Sisi tuliona changamomoto na tukaanza maandalizi ya mitaala yetu ya elimu na kubuni mambo kadhaa hivyo mafunzo hayo yatasaidia kwenda kuboresha mitaala yetu ikiwa kubadilisha tabia za wahitimu kufanya maamuzi ya matumizi na uwekaji wa akiba ya fedha,” amesema.

Aidha Wanafunzi wa vyuo vikuu wasishangae kuona wanafundishwa elimu ya fedha wasome kwani itawasaidia kuwa bora zaidi hata katika shughuli zao baada ya kuhitimu masomo yao na kuwa bora katika soko la ajira

By Jamhuri