Rais Samia:Tuungane kumkomboa mwanamke wa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) kutumia nguvu ya Chama chao kuungana na kila chama cha siasa kumkomboa mwanamke wa Tanzania.
Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia katika Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lilioandaliwa na BAWACHA katika Ukumbi wa Kuringe.
Aidha, Rais Samia amesema lengo ni kuona mwanamke wa kitanzania anathaminiwa na kupewa haki kama mwingine yeyote duniani kwa kuwa changamoto hazichagui dini, kabila wala itikadi ya kisiasa.


Rais Samia pia amewataka wanawake kutumia siku hii kutathmini maendeleo ya wanawake na changamoto wanazokabiliana nazo kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kupata maridhiano ya haki zao katika usawa wa kijinsia.


Vile vile, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa kufanya kazi kwa pamoja na kushikamana ili kukuza siasa za kistaarabu na za kusikilizana zitakazoleta heshima kwa taifa na kustawisha uchumi.


Rais Samia pia amesema alitumia ubunifu kuunganisha taifa kwa kuhakikisha kunakuwa na maridhiano na uvumilivu ili kuleta mageuzi ambayo yameweka msingi mzuri katika mustakbali wa demokrasia na maendeleo ya taifa letu.
Kwa upande mwingine, Rais Samia alitembelea ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuzungumza na Uongozi wa Mkoa pamoja na wanachama wa mkoa wa Kilimanjaro.