Rais wa Marekani Joe Biden aanguka katika hafla

Rais wa Marekani Joe Biden amejikwaa na kuanguka alipokuwa akikabidhi cheti cha diploma katika sherehe ya kuhitimu kwa Chuo cha Jeshi la Wanahewa la Marekani huko Colorado.

Biden,ambaye ndiye rais mkongwe zaidi wa taifa hilo anayehudumu akiwa na umri wa miaka 80, alisaidiwa kusimama na alionekana kuwa hajadhurika.

Rais alikuwa amesimama kwa takriban saa moja na nusu kupeana mikono na kila mmoja wa wanafunzi 921 waliohitimu.

Awali,mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu ya White House alisema kuwa “yuko sawa”.

“Kulikuwa na mfuko wa mchanga kwenye jukwaa alipokuwa akipeana mikono,” Ben LaBolt aliandika kwenye Twitter baada ya kuanguka siku ya Alhamisi.

“Nilipata mchanga,” rais huyo aliyetabasamu alitania waandishi wa habari alipokuwa akirejea Ikulu jioni hiyo.

Ripoti ya waandishi wa habari wa Ikulu ya White House hapo awali ilisema Biden alijikwaa kwenye mfuko mweusi wa mchanga alipokuwa akipanda jukwaani.