NA MICHAEL SARUNGI

Mabadiliko ya ratiba yanayofanywa kila mara
na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa
kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) ni miongoni mwa changamoto
zilizoshindikana kupatiwa ufumbuzi huku klabu
zikiendelea kuumia kwa kulazimishwa kuandaa
bajeti ya ziada.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati
tofauti, makocha na wadau wa michezo nchini
wamesema hali hiyo imekuwa ikizilazimu klabu
kuwa na bajeti ya ziada hasa kipindi hiki
ambapo ligi imeanza bila ya uwepo wa
mdhamini mkuu.
Kocha Mkuu wa Ndanda FC, Malale Hamsini,
amesema klabu za mikoani hazina wadhamini
na nyingi zinategemea vyanzo vya mapato
kutokana na viingilio milangoni kwa ajili ya
kulipa mishahara, gharama za kambi, usafiri na
matumizi mengine.
Ligi inapoahirishwa kwa visingizio vya kupisha
michuano ya kimataifa inaonyesha ukosefu wa

umakini wa kiutendaji kwa watendaji wa bodi
ya ligi kwa kushindwa kuitafsiri ratiba ya
michuano ya kimataifa ambayo hutolewa kabla
ya kuanza kwa ligi mbalimbali ndani ya nchi
wanachama wa CAF na FIFA.
Kutokana na kufahamika huko kwa ratiba ya
AFCON, bodi ya ligi walipaswa kupanga ratiba
kwa kuzingatia ushiriki wa timu za taifa katika
michuano mbalimbali na kujifunza kutoka ligi za
nchi nyingine ambako pamoja na kuwa na timu
nyingi bado ratiba zao haziingiliani.
Kocha Mkuu wa Klabu ya Mbeya City,
Nsanzurwimo Ramadhan, amesema
kuahirishwa kwa mechi kwa ajili ya timu ya taifa
ni jambo jema lakini wahusika wanapaswa
kuzionea huruma klabu nyingi zinazojiendesha
kwa kujikongoja huku zikiwa na bajeti ndogo
isiyotosheleza mahitaji.
Upangaji wa mechi za ligi unapaswa kuzingatia
ratiba za mechi za kimataifa za timu ya taifa ya
vijana, wakubwa pamoja na zile za klabu shiriki
katika michuano mbalimbali ya kimataifa ili
kuepusha mkanganyiko huu ambao umekuwa
ukilalamikiwa kila mwaka na klabu na wadau
wengine.
Bodi inapaswa kujifunza kutoka katika ligi
mbalimbali duniani, mfano Ligi Kuu ya England
ambayo ina jumla ya timu 20 lakini bado ratiba
yao imekuwa haibadiliki kila mara, labda
yanapokuwepo majanga ya kiasili kama mvua,

maafa na mambo mengine yasiyo zuilika.
Kocha Mkuu wa Mbao FC ya jijini Mwanza,
Amri Said, amesema bodi imeshindwa kupata
dawa ya kuzuia upanguaji wa ratiba, jambo
ambalo malalamiko yake hayajaanza leo na
kuongeza kuwa inashangaza kuona ligi
inasogezwa mbele kutoa nafasi kwa timu ya
taifa wakati ratiba ilikuwa ikifahamika.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface
Wambura, amesema bodi imekuwa ikijitahidi
kuepusha mabadiliko yasiyokuwa ya lazima ila
inafika wakati hulazimika kupangua ratiba
kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao
kwa masilahi ya mpira.
Wambura amesema mabadiliko ya hivi karibuni
yalitokana na ombi la Kocha wa Timu ya Taifa,
Emmanuel Amunike, aliyetoa mapendekezo ya
kuhitaji muda zaidi ya wiki moja kuweza
kukutana na wachezaji wa ndani walioitwa
kuunda kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars)
kutokana na ugeni wake.
Amesema kutokana na umuhimu wa Taifa
Stars, bodi ya ligi ililazimika kuchukua uamuzi
wa kubadili ratiba ya baadhi ya mechi za ligi
kuu inayoendelea kwa manufaa ya timu ya taifa
ili kocha apate nafasi pana ya kuwafahamu
wachezaji wake wanaounda kikosi.
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau, amesema
uwepo wa mwalimu mpya katika timu ya taifa
na wachezaji wengi wanaounda kikosi hicho

wanacheza ligi ya ndani, ndiyo maana TFF kwa
kushirikiana na bodi wamefikia uamuzi wa
kuahirisha baadhi ya mechi.
“Hatuwezi kujilinganisha na nchi kama za Afrika
Magharibi zenye wachezaji wanaocheza ligi
mbalimbali barani Ulaya, hatuwezi kuiga kila
wanachofanya kwa kuita wachezaji kabla ya
siku tatu za kucheza, hii ni tofauti na hapa
kwetu ambako wachezaji wengi wanacheza ligi
ya ndani,” amesema Kidau.

Mwisho

By Jamhuri