RC Chalamila aridhishwa na ujenzi wa shule ya sekondari ya Mvuti

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Novemba 20, 2023 amefanya ziara kukagua ujenzi wa shule ya sekondari Mvuti iliyopo kata ya Msongola-Ilala na kupongeza ujenzi huo wa kisasa. 

Mhe. Chalamila alimpongeza mkuu wa shule kwa  usimamizi wake licha ya kuwa figusufigusi hazikosekani lakini amejitahidi kusimama kwenye misingi na kuonesha ishara nzuri ya usimamizi wa fedha kwa usasa wa shule hiyo yenye madarasa, bati bora, ’tiles ‘, madirisha ya vioo na ‘gypsum board’.

Pia Mhe Chalamila alisema, “Sasa akishakamilisha kabisa shule yetu hii, maana yake mwisho wa siku tutapata majawabu mazuri, yeye ndiye mjenzi kwakuwa fedha zinaingia kwenye shule yake maana yake ni kwamba amefanya kazi nzuri pamoja na wenzake.”

Vilevile RC Chalamila alitoa wito kwa viongozi wote kuwa waaminifu wanapokabidhiwa pesa za miradi ya shule zitumike vile zilivyoagiziwa ili thamani ya majengo iendane na fedha husika, ambapo amemshukuru mhe. Raisi Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha anazotoa na kuboresha maendeleo ya elimu nchi.

Kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Mhe. Edward J. Mpogolo alisema shule nyingi zilizopewa fedha wameshindwa  kujenga shule za kisasa hali inayopelekea ukarabati wa mara kwa mara wa majengo,  na aliahidi kuanzia sasa shule zote za wilaya ya Ilala zitajengwa kwa mfumo wa ’tiles’, ” Tulikuwa tumeathirika kila baada ya muda mfupi madarasa yale yanatoboka watoto wanakaa kwenye vumbi, mtoto anatoka darasani unafikiri ametoka uwanjani.”

Naye Diwani wa Kata ya Bw. Msongola  Azizi Mwalile alimshukuru mhe Chalamila kwa ziara yake licha ya kuwa kuna ubovu wa barabara hasa kipindi hiki cha mvua,  pia alipongeza kwa pesa walizopewa za kuwezesha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule hiyo, vilevile hakuacha kugusia changamoto wanazozipata ikiwemo ukosefu wa maji, barabara na migogoro ya mipaka.

Ikumbukwe kwamba mradi huo wa shule ndiyo mradi mkubwa  wakwanza wa kisasa katika kata hiyo wenye thamani ya shilingi milioni 528.