Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa tiba Mkoa wa Singida vyenye jumla ya takribani Sh.Milioni 222.472.

Vifaa hivyo ni pamoja na majenereta, sambamba na vifaa vitakavyotumika kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya muda na huduma nyinginezo ambavyo vimekabidhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kituo cha Afya Sepuka na Hospitali ya Wilaya ya Singida, Ilongero.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambayo ilishuhudiwa na wabunge, watendaji wa idara mbalimbali za sekta ya afya, wananchi pamoja na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa alisema kazi hiyo ya usambazaji wa vifaa hivyo ni jukumu lao walilopewa na Serikali.

” Kazi yetu kubwa sisi MSD ni Uzalishaji, Ununuzi, Uhifadhi na Usambazaji wa bidhaa za afya na vitendanishi hapa nchini ambayo tunaifanya kwa mamlaka ya kisheria,” alisema Jumaa.

“MSD leo tupo hapa Ikungi kwa ajili ya kukabidhi jenereta, kitanda cha kufanyia upasuaji, Ultra-Sound mashine pamoja na mashine ya kuasaidia kuwapatia joto watoto wachanga na waliozaliwa kabla ya wakati.(njiti-Infant Radlant warmer) vyenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 72

Jumaa alisema lengo kubwa la kupelekwa kwa vifaa hivyo ni kuhakikisha huduma za uzazi zinaboreshwa na kuwa katika wilaya hiyo MSD ilikuwa inakamilisha vifaa ambavyo ilikuwa imepokea fedha zaidi ya Sh. Milioni 300 ili kukamilisha usambaji wake.

Alisema MSD Kanda ya Dodoma imepokea maombi ya vifaa tiba zaidi ya 700 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ajili ya vituo vya Afya na Zahanati.

“Ukiangalia muda tuliopokea fedha hizi na utekelezaji wa kupeleka vifaa hivyo ni muda mfupi sana na hiyo imetokana na Serikali kuboresha huduma za MSD na kufikia hatua hii ya kukamilisha vifaa ambavyo hatukuvipeleka awali na kuvipeleka sasa baada ya fedha zake kuzipokea muda mfupi uliopita,” alisema Jumaa.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha na MSD imekuwa ikinunua na kusambaza vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya kote nchini ambapo aliishukuru kwa hatua hiyo na kueleza kuwa inajenga morali kwa watumishi wa sekta ya afya na kuipenda kazi wanayoifanya.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu aliishuru Serikali na MSD kwa kupeleka vifaa hivyo na kueleza kuwa sekta ya afya ni uhai na kuwa watu wakiwa na afya njema ndipo wataweza kufanya kazi zao vizuri.

“Leo hii tunashuhudia vifaa hivi vilivyo letwa na Serikali kupitia MSD na kukabidhi hospitali yetu ya Ikungi maana yake ni utekelezaji wetu wa kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo tuliiomba kwa muda mrefu,” alisema Mtaturu.

Alisema kujenga majengo tu ya hospitali haitoshi na kuwa inahitaji na vitu vya ziada vikiwemo vifaa na kuwa madaktari na wataalamu wengine wamesomeshwa kwa lengo la kuwasaidia watu kutibu maradhi mbalimbali na kwa kuvitumia vifaa hivyo ndio wanaweza kufanya kazi yao kwa urahisi iwe kwa kupima na kufanya upasuaji.

Mtaturu alisema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya afya hapa nchini hivyo kila mtu mpenda maendeleo anapaswa kumshukuru kwa jinsi anavyo iendesha nchi kwenye sekta mbalimbali.

Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu akipokea vifaa hivyo kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Sepuka alisema miongoni mwa vifaa alivyo pokea kutoka MSD ni jenereta lenye ukubwa wa KVA 60 na vifaa vingine 11 ambavyo baadhi ni toroli la kuwekea vifaa wakati madaktari na wauguzi wanapokwenda kutoa huduma, vifaa vinavyotumika kumsaidia mtoto baada ya kuzaliwa aweze kupumua vizuri na kuwa vifaa vyote alivyovipokea vinatumika kupingana na uzazi pingamizi na lengo lake ni kumuokoa mama wala mtoto wasife wakati wa kujifungua.

Alitaja vifaa vingine alivyopokea ni mashine kwa ajili ya hewa, mashine ya kupimia uzito, kifaa cha kutundikia dripu ya maji, kifaa cha kuwapa joto watoto waliozaliwa kabla ya muda, kifaa cha kuvuta uchafu kwenye njia ya hewa baada ya mtoto kuzaliwa, saa ya ukutani, kifaa kinachobeba vifaa vya kumuhudumia mtu aliyepata majeraha na pampu inayotumika kumnyonya mtoto kwa ajili ya kuondoa kitu kilichokwama kooni au kupoteza fahamu baada ya kupaliwa na kuwa vifaa hivyo vyote vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 82.

Kingu aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha na akapongeza maboresho makubwa yaliyofanywa ndani ya MSD na kueleza kuwa MSD ya leo ni ya kisasa na mkombozi kwa wananchi katika kazi ya kutoa huduma za afya si kwa Mkoa wa Singida pekee bali kwa nchi nzima kazi ambazo zimekuwa zikionekana kupitia vyombo vya habari.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea jenereta na gari la kuwabebea wagonjwa na wajawazito ambao wengi wao walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa umeme wa uhakika wakati wakipata huduma hasa za upasuaji na kukosekana kwa gari la kuwapeleka hosptali wanapokuwa wagonjwa.

Ighondo alisema pamoja na kupelekewa gari hilo pia Serikali kupitia MSD imewapelekea kifaa kinachotumika kwa ajili ya kuwaongezea joto watoto wanaozaliwa chini ya muda.

Alisema mbali ya gari hilo la wagonjwa vifaa walivyopokea vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 62.7

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dorisila Mlenga, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Grace Ntogwisangu pamoja na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel waliishukuru Serikali kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vinakwenda kuwarahisishia utendaji wa kazi za kutoa huduma kwa wananchi ambapo walisema watavisimamia na kuvitunza ili viweze kudumu kwa muda mrefu wakizingatia Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.

Wananchi Elesisia Mlenga, Asha Salim, Asha Musa, Mwalimu Tatu Njoka, Ashura Iddi na mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Seketoure, Getruda Yona waliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapekea jenereta na gari la wagonjwa na kueleza kuwa vifaa hivyo vinakwenda kuwasaidia katika kupata huduma bora za afya.

Mwanafunzi Getruda Yona alimshukuru Rais Samia kwa kuwajengea shule na kuwapunguzia umbali mrefu ambapo walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 10 kwenda shuleni kabla ya kujengewa kwa shule hiyo ya Seketoure

By Jamhuri