Miradi ya STAMICO yatajwa

London

Wizara ya Madini imezinadi Leseni zipatazo 441 za utafutaji wa madini muhimu na mkakati na leseni 46 kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo ambazo ni fursa kwa wawekezaji kwa ajili ya kuingia ubia na wamiliki wa leseni hizo kuziendeleza na hatimaye kuanzisha migodi.

Hayo yalibainishwa Novemba 21, 2023 na Kamishna Msaidizi wa Madini kutoka Wizara ya Madini Mhandisi Ally Samaje wakati akitoa wasilisho la Wizara katika Siku ya kwanza ya Jukwaa la Biashara kati ya nchi ya Uingereza na Tanzania ambapo aliieleza hadhira hiyo kuhusu madini muhimu na mkakati yaliyopo Tanzania, fursa zilizopo katika uwekezaji kwenye madini hayo na mikakati ya Serikali katika kuvutia uwekezaji.

Mhandisi Samaje alisema kati ya leseni hizo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linayo miradi ya utafutaji madini muhimu ya lithium, graphite, rare earth elements na shaba ambayo iko katika hatua mbalimbali za uendelezaji na ambazo wawekezaji wanakaribishwa kushirikiana na STAMICO kuziendeleza kufikia hatua ya uchimbaji kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mbali na miradi ya STAMICO, Mhandisi Samaje aliyataja baadhi ya madini muhimu na mkakati katika jukwaa hilo lenye lengo la kukuza ushirikiano wa kikanda na kuwavutia wawekezaji kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini kuwa ni pamoja na madini ya lithium, graphite, iron, nickel, phosphate, rare earth element (REE), cobalt na shaba.

Aliongeza kwamba, moja ya mikakati ya Serikali katika kuendeleza madini muhimu nchini ni pamoja na kupata taarifa za kina za kijiolojia kwa kufanya utafiti wa kina kwa kutumia ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey) mpaka kufikia takribani asilimia 50 ya ukubwa wa nchi ifikapo mwaka 2030 hatua ambayo itavutia uwekezaji nchini hususan katika hatua ya utafutaji wa madini mbalimbali.

‘’Hivi sasa utafiti wa aina hii nchini umefanyika kwa asilimia 16 tu. Hivyo, programu hii ni moja ya masuala muhimu yatakayotekelezwa kupitia “Vision 2030 – Madini ni Maisha na utajiri,’’ alisema Mhandisi Samaje.

Alifafanua kuwa, upatikanaji wa taarifa za kina za kijiolojia kupitia programu ya “Vision 2030 kutasaidia kutambua maeneo yenye viashiria vya madini mbalimbali ili tafiti za kina kama uchorongaji ziweze kufanyika katika maeneo hayo kwa lengo la kubainisha uwepo wa mashapo ya madini yanayoweza kuchimbwa kibiashara.

‘’Upatikanaji wa taarifa za kijiolojia katika maeneo ya wachimbaji wadogo kutasaidia wachimbe kwa tija bila kupoteza mitaji yao. Pia, taarifa zitakazopatikana zitaweza kutumiwa na Wizara na taasisi nyingine za Serikali kama vile Wizara ya Maji kujua maeneo yenye miamba yenye mikondo ya maji chini ya ardhi kwa matumizi mbalimbali,’’ alisisitiza Mhandisi Samaje.

Jukwaa hilo limendaliwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania. Sekta za umma na Serikali kutoka Tanzania Bara na Visiwani zinazoshiriki katika jukwaa hilo ni pamoja na Sekta Viwanda, Kilimo, Madini, Nishati, Uchumi wa Buluu, Fedha, Uwekezaji na Biashara.

Kwa upande wa Sekta ya Madini, ujumbe wake unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara Kheri Mahimbali, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Augustine Olal, Kamishna Msaidizi wa Madini Mhandisi Ally Samaje na Mchumi Aman Ng’oma.

By Jamhuri