Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema kuwa shirika lisilo la kiserikali la Site Trust Foundation lipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi katika sekta ya afya ,elimu, maji, michezo na mazingira katika jamii kwa lengo la kukuza ustawi wa maisha yao ya kila siku.

Homera ameyasema hayo jana wakati akiitambulisha taasisi hiyo kwa wananchi wa kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma ambapo katika utambulisho huo uliohidhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa chama na Serilikali akiwemo Mkuuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Labani Thomas ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Wilman Kapenjama Ndile ambapo utambulisho huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmahauri ya Manispaa ya Songea.

Amesema kuwa shirika hilo la Site Trust Foundetion lina wajibu mkubwa wa kugusa maisha ya wananchi wakiwemo wa Mkoa wa Ruvuma na kuwashika mikono wale wenye uhitaji ili kugusa maisha na kutimiza nia na ari ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baadhi ya wajasiriamali wakiwemo mama lishe wakiwa na baadhi ya viongozi wa Shirika la Site Trust Foundation kabla ya kupewa majiko ya gesi

Amefafanuwa kuwa katika sekta ya afya shirika hilo la Site Trust Foundation linajitahidi kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi katika kuhamasisha na kuwaelewesha kufuata huduma ya afya kwenye vituo vya afya pia kusaidiana na Serikali kuhakikisha kuwa mazingira ya utoaji wa huduma yanaendelea kuboreshwa kama ilivyo adhima ya serikali ya awamu ya sita ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

”Ndugu mgeni rasmi mazingira ni uhai na shirika letu lisilo la kiserikali la Site Trust Foundetion linaamini utunzaji wa mazingira ndio mtaji wa kizazi chetu kijacho ,hivyo pamoja na utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira ususani kwenye vyanzo vya maji shirika litahakikisha pamoja na mambo mengine linakwenda kuongeza upandaji miti katika maeneo yetu yenye uoto wa asili yaliyoharibiwa”amesema Homera.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Wilman Kapenjama Ndile amesema kuwa maendeleo licha ya kuwa Serikali imejikita zaidi kuyaboresha katika sekta mbalimbali pia sekta binafsi inamsaada mkubwa katika kusaidiana na serikali kuhakikisha kuwa huduma mbalimbali za kijamii zinaboreshwa na si vinginevyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera akilitambulisha shirika la Site Trust Fondation kwa wakazi Mkoa wa Ruvuma.

Hata hivyo amewataka wananchi mkoani humo kutoa ushirikiano kwa shirika hilo ambalo lieonesha kuwa na dira ya kusaidia huduma mbalimbali za jamii kuanzia ngazi za chini wakiwemo mama lishe, wajasiliamali, wakulima pamoja na wafanyabiashara kwani shirika hilo litawea kusukuma maendeleo ya wananchi mbalimbali wa mkoa huo.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria utambulisho wa shirika hilo lisilo la kiserikali wameoneshwa kufurahishwa nalo na wameiomba ijikite zaidi kuhakikisha wananchi walioko vijijini pale wanapohitaji msaada waweze kusaidiwa na pia wameshukuru kwa msaada wa majiko ya gesi ambayo yatasaidia kwa kiwango kikubwa kwa lengo la kutunza mazingira.

By Jamhuri