Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Chalinze

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo amewaasa, askari wa Polisi Chalinze kutokuwa na muhali kwa madereva wanaokiuka Sheria za usalama barabarani.

Akiwa katika siku ya pili ya ziara ya ukaguzi katika Wilaya zilizopo Mkoa wa Pwani na kuzungumza na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali anawataka kutokuacha jukumu la ukamataji wa madereva wanaovunja Sheria kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani pekee,badala yake nao wachukue hatua ili kuweza kutokomeza ajali za mara kwa mara zinazotokana na makosa ya kibinadamu kama vile kuyapita magari mengine bila tahadhari, mwendo kasi, matumizi ya vileo na kutokuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu.

Hivi karibu watu wa nne wa familia moja walipoteza maisha katika ajali ya barabarani eneo la Mapatano, Kata ya Mbwembwe tukio ambalo lilivuta hisia kwa watu wengi kutokana na ajali hiyo ya barabarani.

Kamanda Lutumo alisema ” Askari wote wana jukumu la kutoa taarifa kwa wenzao waliopo barabarani pindi wanapoona dereva anaendesha gari kwa kuvunja Sheria za usalama barabarani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa”.

Aidha, aliwakumbusha umuhimu wa utoaji huduma bora pindi wanapowakamata madereva wanaovunja Sheria kwa kuwaeleza makosa yao kabla ya kutoa adhabu ili wajue makosa yaliyopelekea kupewa adhabu husika.

By Jamhuri