Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela amefanya ziara ya Kutembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Chato ambao unatekelezwa kwa awamu.

Akizungumza mara baada kukagua mradi huo Shigela amesema anamshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao unasaidia kutoa huduma ya afya kwa wakazi wa maeneo mbalimbali hususani wa Kanda ya Ziwa.

Vilevile Shigela ameipongeza TBA kwa ubunifu na ujenzi unaozingatia viwango vya ubora katika utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi amesema miradi mingi inayotekelezwa na TBA Wilayani Chato inajengwa kwa ubora unaotakiwa pamoja na kuzingatia muda wa mkataba.

Akitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa TBA Mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Gefta amesema utatekelezaji wa mradi huo unafanywa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza imefikia asilimia 99 ukihusisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la Madawa na Maabara, jengo la wagonjwa wa dharura, jengo la wagonjwa mahututi, jengo la kuchomea taka pamoja na jengo la kangavuke ( Power house). Aidha Mhandisi Gefta amesema awamu ya pili imefikia asilimia 79 ikihusisha ujenzi wa jengo la wodi la ghorofa mbili, jengo la mionzi ( Radiology) pamoja na kazi za nje ( tenki la maji, vibanda vya walinzi, sehemu ya kuegeshea magari na marekebisho ya mandhari ya nje).

Vilevile Mhandisi Gefta amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na kushukuru uongozi wa Mkoa wa Geita kwa ushirikiano wanaoutoa.

Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Chato unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania ( TBA) kama Mkandarasi na Mshauri Elekezi.

By Jamhuri