NHC lajipanga kutekeleza mradi wa Samia Housing Scheme

Shirika la Nyumba la Taifa limejipanga kutekeleza mradi wa Samia Housing Scheme unaotarajia kujenga nyumba zaidi ya 5000 na kuzalisha ajira zaidi ya Elfu Ishirini na Sita.

Hayo yameelezwa na Daniel Kure Afisa Mauzo na Masoko Mwandamizi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa wakati akizungumzia ushiriki wao katika Maonyesho ya Madini yanayoendelea Mkoani Geita ambapo amesema kuwa wataanza na awamu ya kwanza katika Mkoa wa Dar es salaam na kisha Dodoma.

Afisa huyo amesema kuwa wameshiriki katika maonyesho hayo ili kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mradi huo na hivyo kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kwa wale wote wenye mahitaji ya nyumba waweze kupata kwa wakati.

Afisa Mauzo na Masoko Shirika la Nyumba la Taifa NHC  Bw. Daniel Kure akitoa maelezo kuhusu mradi wa Samia Housing Scheme unaojengwa Kawe katika jiji la Dar es Salaam kwenye maonesho ya tano ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika EPZA Bombambili mkoani Geita.

Amesema kuwa mradi huo umeangalia vipato vya watanzania wote kwa kuangalia madaraja mbalimbali wakiwemo watumishi wa serikali,sekta binafsi pamoja na wafanyabiashara.

‘Mradi huu hadi utakapokamilika katika awamu zote utagharibu Bill 466 na utekelezaji wake utaanzia eneo la Kawe Tanganyika Packers baada ya hapo ndipo utasambaa kwa nchi nzima na tunatarajia tutajenga Nyumba 5000’amesema Daniel

Daniel amewataka wananchi wote wanaohitaji nyumba wahakikishe wanatumia fursa hiyo mapema kwani wataanza kuutekeleza kuanzia mwezi wa kumi na baada ya miezi kumi na mbili watakuwa wameukamilisha.

Mounekano wa nyumba mbalimbali katika picha zitakazojengwa kwenye mradi wa Samia Housing Scheme Kawe jijini Dar es Salaam.

Aidha Daniel amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika Maonyesho hayo ili waweze kupata taarifa kamili kuhusiana na mradi huo.

‘Nyumba zetu zinakuwa ghali kwa sababu tunapewa eneo na Halmashauri eneo ambalo hakuna miundombinu ,barabara,maji na umeme hivyo mara nyingi sisi ndiyo tunagharamia na hivyo kufanya gharama kuongezaka na kuwa kubwa na watanzania wanaona kama gharama kubwa lakini ukizingatia gharama zote hizo unaona kabisa ubora wa nyumba zanyewe na huduma tunayoitia ’amesema Daniel

Hata hivyo amesema Shirika la Nyumba la Taifa NHC katika kutekeleza hiyo miradi linaingia katika mchakato wa kununua Ardhi pamoja na kuweka miundombinu mbalimbali ili kurahisisha huduma zote.