Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Tabora

Wakulima nchini wametakiwa kuzingatia kanuni za kilimo bora na kufuata maelekezo ya wataalamu ili kuwa na kilimo chenye tija.

Ushauri huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akifungua maadhimisho ya siku ya mbolea duniani katika uwanja wa Chipukizi uliopo katika halmashauri ya manispaa Tabora.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Simon Chacha alisema kilimo cha kisasa ndio msingi sahihi wa kumwinua mkulima na kumwezesha kuwa na uchumi endelevu.

Alibainisha kuwa maadhimisho hayo ni muhimu sana kwa kuwa yatawapata fursa wakulima kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea hivyo kuongeza uzalishaji.

Chacha alifafanua kuwa Mkoa huo licha ya kuwa na km za mraba zaidi ya 20,000 zinazofaa kwa shughuli za kilimo lakini zinazolimwa ni kati ya 6000 na 7000 tu.

Alisisitiza kuwa sekta ya kilimo na ufugaji katika Mkoa huo inachangia zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya Mkoa hivyo akabainisha kuwa kama wakulima watazingatia ushauri wa wataalamu uchumi wao utaboreka zaidi.

Alitoa mfano wa msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 ambapo jumla ya tani milioni 1.16 za mazao mchanganyiko ya chakula zililimwa ikilinganishwa na msimu wa 2021/2022 ambapo uzalishaji ulikuwa tani laki 973 tu.

‘Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wakulima na kuendelea kutenga fedha zaidi ili kuboresha shughuli zao’, alisema.

DC Chacha alieleza kuwa juhudi hizo zimewezesha wakulima wa Mkoa huo kuendelea kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara hivyo kujiongezea kipato.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania (TFRA) ambao ndio waandaaji wa Maadhimisho hayo Anthon Dialo alimshukuru Rais Samia kwa kuweka mpango wa kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima.

Alisisitiza kuwa uelewa wa matumizi sahihi ya mbolea ya ruzuku utaleta tija kubwa kwa wakulima nchini.

Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Ramadhan Kapela alipongeza kazi nzuri inayofanywa na TFRA katika kuhakikisha mbolea ya ruzuku inayotolewa na serikali inawafikia wakulima wote.

Aliwataka kuhakikisha changamoto ya mbolea kuchelewa kuwafikia wakulima inatatuliwa mapema kabla ya kuanza msimu mpya wa kilimo.

By Jamhuri