Lilian Lundo na Veronica Simba, JamhuriMedia, Geita

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imekuja na mpango wa kutoa mikopo midogo kwa ajili ya kujenga vituo vya mafuta vidogo vidogo vijijini ili kuzuia ajali za moto zinazotokana na kuuza mafuta ya Petroli kwenye madumu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati wa hafla ya uwashaji wa umeme wa REA Jimbo la Geita Mjini, mkoani Geita leo Oktoba 2, 2023.

“Tumekuja na mpango wa kuwapa watu mikopo midogo, tuanzishe vituo vya mafuta vidogo vidogo vijijini ili watu wetu waache kuuza madumu ya Petroli humu, na baadae wanapata ajali ya kuunguzwa na mafuta hayo,” amesema Dkt. Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akikata utepe kama ishara ya kuwasha umeme katika kijiji cha Nyanguku mkoani Geita leo Oktoba 2, 2023.

Vilevile amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inagawa mitungi ya gesi kwa ruzuku ndogo ili kuwasaidia Wanawake Watanzania kupika kwa kutumia nishati hiyo mbadala.

“Rais anapenda wanawake Watanzania, ameyaona mateso yao ya kupika kwa kutumia kuni, tumekuja na nishati mbadala ya kuwasaidia Wanawake wa Tanzania wapike kwa kutumia nishati mbadala,” amesema Dkt. Biteko.

Wakati huo huo Dkt. Biteko amewaomba viongozi wote waliochaguliwa na kuteuliwa kusimamia miradi ya Serikali na fedha zote zinazoletwa ziwahudumie Watanzania.

“Hakuna maana yoyote, sisi viongozi kuwa tunaishi maisha ya mjini lakini wananchi wetu wa vijijini hali zao ngumu. Mhe. Rais anatoa fedha kwa ajili ya watu hawa, anatoa fedha anajima, anapambana kwa ajili ya maendeleo ya watu, anataka kuona wananchi wanahudumiwa,” amesema Dkt. Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akibonyeza kitufe kuwasha umeme katika kijiji cha Nyanguku mkoani Geita leo Oktoba 2, 2023.

Hivyo ametoa wito kwa viongozi wote, kuhudumia wananchi masikini wanaotaka kujipambanua kupata maendeleo yao.

Naye, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 39.1 kwa ajili ya kuweka umeme vijiji vyote vya Mkoa wa Geita ambavyo havijpata umeme.
 
Aidha ametaja miradi mitatu inayoendelea kutekelezwa katika Jimbo la Geita Mjini kuwa ni Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Kupeleka umeme Pembezoni mwa Miji pamoja na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza na wananchi baada ya kuwasha umeme katika vijiji vya cha Bunegezi na Nyanguku mkoani Geita leo Oktoba 1, 2023.
Sehemu ya viongozi wa chama na Serikali na wananchi wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati wa hafla fupi ya kuwasha umeme vijiji vya Nyakungu na Bunegezi mkoani Geita leo Oktoba 2, 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela  akitoa maelezo ya awali kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko wakati wa kuwasha umeme katika kijiji cha Bunegezi mkoani Geita leo Oktoba 2 , 2023.

By Jamhuri