Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametoa mapendekezo kwa Shirika la Reli Tanzania kuona namna ya kuweka kituo eneo la Magindu katika Reli ya Kisasa(SGR)ili wananchi wa Chalinze waweze kunufaika na usafiri wa treni ya mwendokasi.

Akitoa mapendekezo hayo, kwenye kikao cha bodi ya Barabara Mkoani Pwani,alieleza kituo kilichowekwa katika mpango ni KWALA,RUVU ,SOGA ambavyo vipo mbali na abiria watakaotoka Chalinze Jambo litakalowagharimu kwa muda.

Amefafanua, Mamlaka husika iangalie namna ya kusogeza huduma hiyo eneo la Magindu ili iwe ahueni kwa Wanachalinze.

“Kwala,Ruvu,Soga, kwangu Mimi na wenzangu ni mbali,nikienda Dodoma naweza kutumia masaa mengi kama muda tunaotumia sasa na tusione tija,na tusinufaike na mradi huo mkubwa wa kimkakati,Kibaha kwenda Soga ni mbali sana,tutajikuta wengine wakituomba tuwasafirishe hadi Kwala-Soga na gharama zikawa kubwa zaidi “alielezea Ridhiwani.

“Tusipoangalia vizuri Tutatumia miundombinu zaidi ,sikwambii Mkuu wa mkoa uingize hili katika mkakati nitakuwa kama nakuonea ,Ila naomba ufikishe kwa wakubwa mkiona inawezekana kituo hiki kiongezwe kwa manufaa ya wanaotoka Chalinze ,Msata,Mbwewe ,Kimange na kwingine ambao wapo mbali zaidi”alisisitiza  Ridhiwani.

Ridhiwani alisema ,ni Wakati wa kuiangalia Pwani yetu kwa tamaa zaidi ya kimaendeleo na kuinua uchumi .

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ,ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Kisarawe Dk.Selemani Jafo aliomba Wakala wa Barabara kuweka bajeti kwa ajili ya kutengeneza barabara kutoka Msanga -Kimanzichana yenye zaidi ya km.44.

Amesema, barabara hiyo ambayo inaunganisha Wilaya ya Kisarawe na Mkuranga inatakiwa kuingizwa kwenye miradi ya kimkakati ili kurahisisha usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo.

Awali meneje wa TARURA Mkoani Pwani, Leopold Runji ameeleza kuwa , barabara ya kimkakati Kibaha kuelekea treni SGR kituo Cha Soga km 15 ipo katika usanifu ,Ruvu station km 8.

“Kwa Barabara za Mjini Chalinze na Bagamoyo km 8 zinafanyiwa usanifu huku kwa Upande wa Kisarawe tunafungua barabara ya Kisarawe-Mkuranga ya Msanga -Kimanzichana ipo kwenye mpango 2023-2024″alieleza Runji.

Katika barabara za miji Rufiji walianza mita 500, mwaka 2021 mita 500 na sasa watajenga mita 500 nyingine.

Runji alielezea kwa upande wa Kibiti ,lipo daraja la Mbuchi ambalo limekamilika  sasa wanaongeza mtandao wa Barbara Muhoro -Mbuchi hadi Mbwera km 35 ambapo km 23 tayari zinapitika na uimarishaji unaendelea.

“Km 12 Mbuchi -Mbwera kikwazo  daraja la Mbwera tunataka kulijenga ujenzi utaanza mwaka huu 2023″alisema Runji.

Hata hivyo Runji alieleza ,ipo changamoto Mkuranga,Kibiti,Rufiji sehemu kubwa ina mchanga hali inayosababisha mchanga kutolewa ndipo kuwekwe malighafi nyingine za ujenzi ,na kusababisha gharama kubwa .

By Jamhuri