Na Mussa Augustine.

Taasisi ya Philibert Paschal Foundation imekua ikitoa Elimu ya Usalama Barabarani kwa Madereva wa pikipiki za kusafirisha abiria(Bodaboda) ikiwa ni jitihada za kuisaidia serikali kupunguza vifo vitokanavyo na ajali za bodaboda zinazotokea mara kwa mara.

Akizungumza Dar es salaam na JAMHURI Katika Mahojiano Maalumu Nabii na Mtume wa Kanisa la Bwana yesu kwa Mataifa yote lililopo Tabata Kinyerezi ,linalosimamia Taasisi hiyo Nabii Philibert Paschal amesema kuwa Elimu hiyo inasaidia kuwafanya Madereva wa pikipiki za kusafirisha abiria ( Bodaboda) kuheshimu kazi yao nakufuata sheria za usalama Barabarani.

“Sisi kama taasisi tunashauri ufike wakati sasa Serikali iweke masharti ya Madereva bodaboda wasome kwenye vyuo vya Usafirishaji mfano NIT na wawekewe kigezo katika kupatiwa leseni lazima dereva awe amesomea udereva hata kwa kiwango cha cheti ndo apewe leseni hali hiyo itapunguza ajari za barabarani” amesema Nabii na Mtume Philibert Paschal.

Aidha amesema kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Jeshi la polisi Kikosi Cha usalama Barabarani kutoa Elimu hiyo Kwa Madereva bodaboda huku kauli mbiu ikiwa ni “Linda bodaboda na abiria wake”hatua ambayo inawafanya Madereva hao kubadilika na kuheshimu kazi wanayoifanya kwani ndio inayowapatia kipato cha kuendesha maisha yao.

Taasisi ya Philibert Paschal Foundation iliyoanzishwa mwaka 2021 imekua ikijihusisha na shughuli mbalimbali za Kijamii kwa kusaidia makundi Maalumu ikiwemo kundi la Wazee wasiojiw eza,Watoto yatima na waishio kwenye mazingira magumu ikiwa ni sehemu yakuonyesha upendo pamoja na kuhakikisha makundi hayo yanapata mahitaji muhimu ya kibinadamu.

“Tunatoa msaada wa kuwakatia bima za afya na kuwalipia ada za shule Watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu,pia wazee wasiojiweza nao tunajaribu kuwasaidia,tunaonyesha Upendo kwao na kuhakikisha nao wanapata mahitaji muhimu ,hivyo tunaomba wadau mbalimbali waweze kujitokeza kushirikiana nasi katika kufanikisha malengo haya” amesema.

Aidha Kwa mujibu wa Nabii na Mtume Philibert Paschal Taasisi hiyo ina malengo ya kuwafikia watu wengi wenye mahitaji katika sehemu mbalimbali za Mkoa wa Dar es salaam na Mikoa mingine lakini kwa sasa Taasisi hiyo inakumbwa na changamoto ya kukosa rasilimari fedha huku mahitaji yakutoa msaada yakiwa ni mengi,hali ambayo pia imefanya kushindwa kuyatambua makundi yote.

Katika hatua nyingine Kiongozi huyo wa Dini ametoa wito kwa viongozi wenzake wa dini kupendana na kuacha kutendeana vitu ambavyo vinawafanya waonekane ni Watumishi wa shetani nakwamba viongozi hao ndio wanawajibu wa kulinda amani nasio kupandikiza chuki kati yao.

By Jamhuri