Na Mwandishi wetu JAMHURI.

Shahidi wa utetezi,Khalid Kilua katika kesi ya  wizi wa vitu vya dukani vyenye thamani ya Sh 68.4 milioni inayomkabili aliyekuwa Meneja wa Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa Umma(PSSSF),Rajabi Kinande na wenzake amedai kuwa alipewa taarifa ya mdomo ya kuondolewa  kwa Mohamed Soli kwenye nyumba iliyopo mtaa wa Lindi na Kongo.

Kilua ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Kimara akiongozwa na Wakili wa Utetezi,Adinani Chitale mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Ilala,Fadhili Luvinga,alidai wakati akiwa Mtendaji wa Kata ya Gerezani  alipewa taarifa ya mdomo na mtendaji wa mtaa,Mbotela Kolimba kuwa amepewa barua inayotoka Mahakama ya mwanzo ya kariakoo kuhusu kuondolewa Soli kwenye nyumba iliyopo eneo hilo.

“Utaratibu haukufuatwa kwa kuwa sikupata kwa maandishi nilielezwa Kwa mdomo na mtendaji wangu wa mtaa kuna barua amepewa ya kuondolewa kwenye nyumba Soli kwa kuwa amekiuka Mahakama,”amedai Kilua.

Amedai, utaratibu unaotumika kupokea taarifa kupitia maandishi lakini mimi nilipokea kwa mdomo ila Mtendaji wa mtaa alipewa kwa maandishi kuna zoezi la mahakama litaendelea Kwa kuwa Soli amekaidi amri ya  mahakama kuondoka kwenye nyumba iliyopo eneo hilo.

Kilua amedai Juni 16,2020 saa 5:30 asubuhi Soli alifika ofisini kwake na kumweleza kuna watu wamevamia na wametoa vitu  kwenye nyumba yake.

Amedai baada ya kupewa taarifa hizo alimpigia simu Mtendaji wa mtaa na mwenyekiti wa serikali ya mtaa ambapo walielekea kwenye eneo la tukio.

Kilua amedai walipofika eneo la tukio walikuta limezunguushiwa uzio huku likiwa na mabaunsa,akari polisi pamoja na dalali wa mahakama kutoka kampuni ya Rimina Auction Mart aliyejitambilisha kwa jina la Rose.

“Nilipofika niliambiwa na dalali wa mahakama kuwa wanaendelea na zoezi la agizo la mahakama basi tulipojiridhisha tuliondoka kuelekea ofisini kuendelea na shughuli zingine”amedai Kilua.

Amedai vitu mbalimbali vya dukani vikiwemo vya ujenzi vilitolewa nje na mabaunsa waliokuwepo eneo hilo  ambavyo vilikaa nje Kwa wiki mbili huku vikiwa vimezunguushiwa uzio.

Shahidi mwingine,Ofisa Mtendaji wa mtaa wa Mongolandege Kata ya ukonga,Mbotela Kolimba amedai Juni Mosi 2020 akiwa Mtendaji wa mtaa wa Gerezani Magharibi alipokea barua kutoka kwenye kampuni ya udalali hiyo ikieleza kuna maagizo yametoka  mahakamani yakimtaka Soli atoke kwenye nyumba hiyo asipotekeleza atatolewa.

“Juni 15,2020 kampuni ya udalali ilitoa vitu vya Soli nje baada ya kukaidi kuondoka na ilipopita siku nne Soli alikuja ofisini kwangu na kuniambia ameibiwa Kwa kuwa suala hili lilikuja nje ya uwezo wangu sikuweza kufanya chochote,”amedai Kolimba.

Naye mshtakiwa Ashura Kapera ambaye ni daktari wa hospitali ya Muhimbili ametoa Utetezi wake na kudai kuwa Soli alikuwa amewapangisha watu wanne kwenye nyumba yao ya urithi hivyo uamuzi wa mahakama ya mwanzo ilitoa utaratibu aondolewe ili wabaki walithi walioteuliwa kusimamia nyumba hiyo.

“Kampuni ya udalali Rimina  Auction Mart imetekeleza majukumu yake kumtoa Soli awali nilipigiwa simu na dalali wa mahakama kama namfahamu nikamjibu huyo ni kaka mrithi halali kama Mimi lakini katika usimamizi wa mirathi hajawahi kuambiwa akae pale nikamwambia afanye kazi yake,”amedai Ashura.

Washtakiwa  wengine katika shauri hilo ni Farida Mbonaheri(34),Mohamed Miraji(48) na Msafiri Raha.

Katika kesi ya msingi kati ya Juni 16,2020 mtaa wa Gerezani wilaya ya Ilala washtakiwa wote kwa pamoja walivunja na kuingia kwenye duka la Mohamed Soli kwa nia ya kutenda wizi na waliiba vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya  Sh 68.4 milioni.

By Jamhuri