Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Kibaha

Halmashauri nchini zimetakiwa kushirikiana na Serikali kupunguza umaskini kwenye baadhi ya kaya ikiwemo  ,kuvikopesha vikundi vya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini( TASAF) ili viweze kujiinua kiuchumi.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete alitoa rai hiyo wakati alipofika kijiji cha Kisanga kata ya Masaki wilayani Kisarawe Mkoani Pwani ,kujionea shughuli zinazofanywa na wanufaika wa TASAF .

Alieleza, mapambano ya kuondoa umaskini ni ya wote,kwani zipo fursa katika Halmashauri nchini zifikie makundi hayo.

Ridhiwani alisema , utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaelekeza kuanzishwa kwa miradi ya kujikwamua kiuchumi, ili kuondoa umaskini na utegemezi ili wenye uhitaji waweze kuishi bila utegemezi.

Amesema ,TASAF ni moja ya miradi hiyo ,ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imeurithi na inaendelea kupeleka fedha ili wanufaika wafaidike na mradi huo.

“Kuvaa madela na kanga isiwe kigezo cha kuwanyima mkopo ya halmashauri, mafanikio ya mtu hayaangaliwi kwa umaridadi wake, wanawake hawa nao wanauhitaji wa mikopo hii”

Ridhiwani alielezea, Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa kuwapigania Watanzania kuondokana na hali mbaya ya maisha, ambapo ndani ya miaka miwili Bilioni 51 zimepelekwa kuwezesha wanufaika hao.

Vilevile aliwataka watendaji wa TASAF kuendelea kutambua wenye uhitaji bila kuweka vikwazo.

Awali mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ,Edmund Livinda amefafanua kuwa,mradi wa TASAF ulianza kutekelezwa 2015 Septemba kwenye  vijiji 49 kati ya vijiji 77 ikiwa ni sawa na asilimia 70 na jumla ya walengwa 2,120.

Idadi iliongezeka baada ya zoezi la uibuaji 2021 vijiji 28 na walengwa walifikiwa 3,280.

Livinda alisema , Januari -Februari 2023 imepungua 3,013 na imepungua kutokana na baadhi ya wanufaika kutolewa kutokana na sababu mbalimbali.

Anasema jumla ya mizunguko 37 imefanyika toka Januari -Februari 2023 na sh.bilioni 3.256 zimeahaulishwa kwa walengwa.

By Jamhuri