url-1Katika sehemu ya kwanza ya ripoti hii, tulikuletea hadidu rejea alizopewa Jaji Joseph Warioba na wajumbe wenzake wa Tume ya Kuchunguza Kero ya Rushwa Nchini na sehemu ya vyombo vya dola vilivyotajwa kuwa wanakula rushwa. Katika sehemu ya pili leo, tunakuletea mwendelezo wa ripoti hiyo. Endelea…

 

VYOMBO VYA HABARI:

(i) Waandishi  hupokea rushwa ili kuandika au kutoandika, kutangaza au kutotangaza habari zinazojenga ama kuharibu sifa za mtu au taasisi.

(ii) Baadhi ya maofisa wa vyombo vya habari hupokea rushwa ili kuandika au kutangaza uzuri au ubaya wa vyombo fulani fulani.

 

NISHATI, MADINI NA MAJI

(i) Wafanyakazi wa Shirika la Ugavi la Umeme (TANESCO), wanadai hongo ili wawaunganishie umeme waombaji wapya.

(ii) Wafanyakazi wa Idara ya Madini hudai hongo kutoa leseni za uchimbaji madini na ugawaji wa maeneo ya kuchimba madini. Wanadai pia hongo ili kutoa thamani ndogo kwa madini yanayosafirishwa nje ya nchi.

(iii) Watumishi wa Idara ya Maji hupokea rushwa ili kutoa upendeleo wa mgawo wa maji mijini.

(iv) Wafanyakazi wa Idara ya Maji mijini wanadai rushwa ili waweze kuunganisha mabomba ya maji ya wateja na bomba la kusambaza maji.

 

SERIKALI ZA MITAA:

(i) Rushwa hutolewa ili kupata idhini ya maombi ya leseni za biashara kuanzia kwenye ngazi ya kata hadi wilayani.

(ii) Rushwa hutolewa kwa wajumbe wa Baraza la Usuluhishi la Kata ili kutoa upendeleo katika maamuzi kwa upande fulani.

(iii) Watumishi wa halmashauri za miji na wilaya wanadai na kupokea rushwa wakati wa kuajiri, kupandisha vyeo na kutoa madaraka.

(iv) Watumishi wa Serikali za Mitaa hudai na kupokea rushwa ili kutoa huduma mbalimbali kama unyonyaji wa maji machafu, utoaji wa tiba na kadhalika.

(v) Viongozi wa halmashauri za miji na mitaa hudai na hupokea rushwa ili kuidhinisha na kutoa tenda kwa makampuni binafsi.

(vi) Madiwani hupokea hongo ili kuidhinisha ujenzi wa vibanda vya biashara sehemu zisizoruhusiwa na kulinda visibomolewe.

(vii) Mabwana na mabibi afya wa halmashauri za miji hutishia kuwafungia leseni wafanyabiashara na hivyo kupokea rushwa.

1. Kundi la pili la wapokea rushwa ni viongozi na watumishi wa umma wa ngazi za juu ambao kujihusisha kwao katika vitendo vya rushwa ni matokeo ya uroho wa mali na fedha kwa vile hawafanyi hivyo kwa madhumuni ya kukidhi haja za msingi za maisha yao na familia zao (Grand Corruption). Vipato vyao vya kihalali vimetosheleza mahitaji yao na wamekwishajilimbikizia mali na fedha za kutosha.

2. Mbinu ambazo wamekuwa wanatumia kudai na kupokea rushwa ni kama ifuatavyo:

(i) Viongozi wanaopaswa kutoa maamuzi mbalimbali muhimu ya kitaifa, uhongwa na wafanyabiashara ili kufanya maamuzi kulingana na matakwa ya wafanyabiashara hao. Kwa mfano ugawaji wa maeneo ya uwindaji (Hunting Blocks), viwanja katika maeneo nyeti, urejeshaji wa nyumba zilizotaifishwa n.k.

(ii) Viongozi kupeana madaraka ya uenyekiti au ukurugenzi wa bodi za mashirika ya umma kwa upendeleo bila kuzingatia ujuzi, uwezo na masilahi ya taifa.

(iii) Watendaji wakuu hudai na kupokea rushwa ili wakiuke kanuni na taratibu za kutoa zabuni.

(iv) Viongozi wenye mamlaka ya kufanya maamuzi au watendaji wakuu wenye uwezo wa kuathiri maamuzi hutoa misamaha ya kodi mbalimbali kinyume cha sheria baada ya kupokea rushwa.

(v) Watendaji wakuu hudai au hupewa rushwa ili kuwasaidia wafanyabiashara kukwepa kodi.

(vi) Viongozi huingilia shughuli za watendaji wakuu na kufanya maamuzi kama ya kugawa viwanja au maeneo mengine ya ardhi yasiyoruhusiwa kisheria ama kwa upendeleo wa kujuana au baada ya kupokea rushwa.

(vii) Watendaji wakuu huingia katika mikataba na makampuni kwa ajili ya kazi za kitaifa bila kujali masilahi ya taifa.

(viii) Viongozi na watendaji wakuu kugawa maeneo ya uwindaji kutoa vibali vya uvunaji wa misitu, uchimbaji madini pamoja na uvuvi bila ya kuzingatia masilahi ya taifa.

(ix) Wanasiasa hutoa rushwa kwa wajumbe ndani ya vyama vya siasa au katika chaguzi nyingine ama kwa wananchi ili waweze kupigiwa kura ama wananchi waweze kuwapigia kura wagombea wao.

(x) Maofisa watendaji wakuu serikalini na kwenye mashirika ya umma kutojali viwango vya kazi zinazotekelezwa na makampuni walioingia nayo mikataba kutokana na kuwepo kwa vipengele vya rushwa ndani ya mahusiano yao, na hivyo kuwawezesha kupokea kamisheni hasa katika kazi za ujenzi na ununuzi wa vifaa.

(xi) Rushwa katika idara zinazohusika na ugavi wa nafasi za masomo nje ya nchi ambapo mzazi hudaiwa rushwa au mzazi mwenye uwezo hutoa rushwa hata bila kudaiwa ili mwanae apatiwe masomo nje ya nchi.

(xii) Viongozi ndani ya Serikali hupokea rushwa na hutoa siri za Serikali kwa watu wasiostahili ili kuwawezesha kukabiliana na maamuzi na maagizo ya Serikali.

(xiii) Wagombea ubunge kutoa rushwa kwa wapigakura ili wachaguliwe.

(xiv) Wabunge kuwakilisha madai ya uongo kuhusiana na shughuli zao za ubunge.

(xv) Wabunge walio kwenye kamati hukirimiwa, hulipiwa mahali pa kulala na chakula na hupewa fedha na wakuu wa mashirika au idara zinazoshughulikiwa na wabunge hao.

(xvi) Wabunge huwahonga waandishi wa habari ili waandike habari kuwahusu wao.

(xvii) Wabunge hupokea au hudai zawadi wanapotembelea viwanda vya umma na vya binafsi.

3. Tume imeainisha aina nne za vitendo vya rushwa, yaani kuomba na kupokea hongo; kulimbikiza mali kama vile nyumba na magari kwa njia ya rushwa; zawadi zenye sura ya rushwa na upokeaji wa kamisheni baada ya kufanikisha mikataba au ununuzi wa vifaa.

4. Kutokana na picha inayoonekana na kutokana na maelezo ya hapa juu,  Tume imetafakari kwa kina namna ya kuandaa mkakati wa kupambana na rushwa. Hata hivyo Tume inaamini kuwa ili kupata ufumbuzi wa kudumu ni muhimu kuangalia sababu zilizolifikisha Taifa kwenye hali hii.

Tume inatambua kuwa Tanzania haikuwa na tatizo la kitaifa la rushwa katika miaka ya 1960. Rushwa imeanza kujitokeza kwa kasi katika miaka ya mwishoni ya 1970 na hatimaye kukithiri katika miaka ya mwishoni ya 1980. 

Wakati huo rushwa iliacha kuwa tatizo linalokabili tabaka la wafanyakazi wa umma wa ngazi za chini na kati pekee na kuanza kuwakumba pia wanasiasa na watendaji wakuu serikalini na katika mashirika ya umma.

5. Tume imebaini kuwa sura ya rushwa ya miaka ya 1970 na ile ya miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 ni tofauti, ingawaje sababu zake zinaweza kuwa zile zile.

Ili kukabiliana na rushwa kikamilifu, Tume inaamini kuwa hapana budi kutambua vianzio vya rushwa na kukabiliana navyo kikamilifu. Tume inaamini kuwa ugunduzi wa kiini cha ugonjwa ni hatua kubwa ya kupata dawa ya kuponyesha au kuzuia.

 

RUSHWA KUANZIA MIAKA YA 1970

6. Matatizo makubwa ya kiuchumi yaliyolikumba Taifa mwishoni mwa miaka ya 1970 yalisababisha Serikali ichukue hatua mbalimbali za kisiasa, kisheria na kiuchumi katika jitihada ya kukabiliana na hali hiyo.

Kodi zilipanda, sera ya biashara ya ndani ilitoa ukiritimba kwa mashirika ya biashara ya umma katika uuzaji wa bidhaa adimu na muhimu; vizuizi vingi viliwekwa katika maisha ya kila siku ya raia kama vile vizuizi barabarani ili kuratibu usafirishaji wa mazao, uzuiaji kuendesha magari Jumapili mchana na kadhalika.

Mfumo wa vibali uliibuka bila utaratibu wa usimamizi na udhibiti unaoeleweka. Wakati huo huo gharama za maisha zilipanda kwa kasi kuliko ongezeko la  mishahara ya watumishi wa umma. Miiko ya uogozi iliwazuia watumishi wa umma kupata kipato cha ziada kutokana na biashara na shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Kwa jumla baadhi ya watumishi wa umma na viongozi walianza kubuni mbinu za kupata mapato ya nyongeza ili kukidhi maisha yao. Mara nyingi baadhi ya mapato hayo ya nyongeza yalikuwa haramu.

7. Tume imefanya tathmini kuhusu tatizo la rushwa nchini na kubaini kuwa rushwa katika miaka ya 1970 ilitokana na mambo yafuatayo:

(i) Matatizo ya utekelezaji wa sheria na kanuni

Kuwepo kwa sheria na kanuni zilizo ngumu kutekelezwa na kusimamiwa. Kwa mfano sheria ya uzuiaji milki ya magari (Motor Vehicles Restriction or Acquisition Act), Road Toll na ile ya kuzuia uendeshaji wa magari Jumapili na vizuizi vya barabarani hazikuwa rahisi kutekelezwa kutokana na ukosefu wa nyenzo za kusimamia. Matokeo yake zilitoa mianya ya rushwa.

 

(ii) Utovu wa usimamizi na uwajibikaji

Tafsiri potofu ya Ibara ya 15 ya Mwongozo wa TANU wa 1971 ilisababisha viongozi kulegeza usimamizi katika sehemu zao za kazi kwa hofu ya kuitwa wanyapara na kupoteza nafasi zao. Matokeo yake yalikuwa watumishi wabovu kuweza kutumia nafasi zao kazini kwa kujinufaisha binafsi. Wakati huo huo utamaduni wa uwajibikaji ulidorora na kusababisha mambo yaende kiholela. Hali hii ilitoa mianya ya rushwa.

 

(iii) Taratibu ndefu na ngumu

Ili kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, Serikali iliweka taratibu kadhaa ambazo zilikuwa ni ndefu na ngumu. Kwa mfano, utaratibu wa kumiliki gari ulihitaji kibali ambacho kilipitia kwenye mkondo mrefu.

Vile vile kipindi hiki kilishuhudia uongezekaji wa urasimu katika  kutoa mizigo bandarini na kupata leseni za biashara. Binadamu kwa ujumla hapendi usumbufu. Usumbufu huo ulitoa mianya kwa watumishi wa umma kutumia nafasi zao kudai hongo. Pia uliwashawishi raia waliokuwa wakihitaji huduma kutoa hongo.

 

(iv) Uadimu wa bidhaa muhimu

Mwishoni mwa miaka ya 1970 taifa lilishuhudia upungufu mkubwa wa bidhaa muhimu (Consumer goods). Wakati huo huo, ukiritimba uliotolewa kwa makampuni ya umma ya biashara uliwapa viongozi wa mashirika hayo mamlaka makubwa ya uamuzi.

Kutokana na upungufu wa bidhaa hizo pamoja na umuhimu wake katika maisha ya kila siku ya raia, mianya mingi ya rushwa ilijitokeza kwa viongozi wa mashirika hayo kupata chochote na upungufu huo uliwachochea raia wenye uwezo kuhonga ili wapate bidhaa hiyo.

 

(v) Mishahara midogo na upandaji wa kasi wa gharama ya maisha

Kama ilivyokwishaelezwa mwishoni mwa miaka ya 1970, mtumishi wa umma kwa mara ya kwanza alijikuta anashindwa kuishi kwa kutegemea kipato chake cha mshahara kutokana na upandaji wa gharama za maisha.

Hali hii iliwafanya watumishi wengi kutafuta mbinu za kupata kipato cha ziada ili kumudu maisha. Wengine walianzisha miradi halali kama ya ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa. Lakini wapo waliotumia nafasi zao za kazi kupata kipato cha ziada nje ya utaratibu wa haki na sheria.

 

(vi) Ukosefu wa uhakika wa usalama wa ajira

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Taifa mwaka 1975, Serikali ilipunguza asilimia 10 ya watumishi wake. Kazi hii iliendelea mwaka 1985, 1992/93, 1994/95 na 1995/96. Vigezo vilivyowekwa kutumiwa katika kazi hiyo havikufuatwa kikamilifu.

Matokeo ya kazi hii ni kwa baadhi ya watumishi hodari na wasio na dosari kukumbuwa na zoezi hilo na wengine wabovu kubakia kazini. Hali hii ilizaa wasiwasi wa kutojiamini miongoni mwa watumishi wa serikali. Hofu hii lichangiwa kwa baadhi yao kuamua watumie nafasi zao kudai na kupokea hongo ili kujikinga na hatma isiyotabirika.

 

(vii) Kukosekana kwa dhamiri ya kisiasa

Moja ya sababu za kushamiri kwa rushwa nchini ilikuwa ni kukosekana kwa dhamiri ya kisiasa. Rushwa ilianza kujadiliwa kwa nguvu sana tangu wakati wa ‘wahujumu uchumi’ na mjadala huo kuhitimishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM cha mwaka 1989, ambacho kilijadili taarifa mbalimbali kutoka taasisi za umma, chama, Serikali na taasisi za dini.

Matokeo ya mjadala huo ni taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya CCM – Dodoma iitwayo ‘Muhtasari wa Taarifa ya Uchambuzi wa Mikakati na Mbinu za Kupambana na Rushwa Nchini.’ Matarajio ya mjadala huo yalikuwa ni kwamba mbali na viongozi wa kisiasa kuendelea kukemea rushwa, maamuzi na maagizo ya CCM yangeliingizwa katika mpango wa Serikali ili iandalie taratibu za kiutawala za kudhibiti rushwa.

Hakuna ushahidi kuwa maamuzi hayo yaliwasilishwa serikalini na Serikali kuyatolea maelekezo ya utekelezaji. Kwa hiyo maamuzi ya chama hayakuwa na nguvu ya kiserikali au ya kisheria kuwashinikiza watendaji wakuu serikalini kuyatekeleza.

Wakati viongozi wa juu wa taifa waliendelea kukemea rushwa, hakuna hatua zilizowekwa sambamba kwa watendaji wakuu wote kuwa viongozi wa kuondoa rushwa katika maeneo yao ya kazi. Vita hivi havikuwa vya wote jambo ambalo lilichochea kasi ya kuenea kwa rushwa nchini.

 

(viii) Udhaifu wa vyombo vya dola

Vyombo vya dola vimeongeza kushamiri kwa rushwa kutokana na sababu mbili; udhaifu wa ndani ya vyombo hivyo vyenyewe na kujihusisha na rushwa na ubadhirifu.

Mahakama za mwanzo na polisi ambazo ziko karibu na wananchi ndizo zenye tuhuma nyingi za rushwa na utovu wa maadili, hekima na uadilifu. Aidha, iko tabia ya kulindana miongoni mwa baadhi ya mahakimu na polisi wanapokabiliwa na tuhuma za rushwa.

Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Usalama wa Taifa vyote vinakabiliwa na matatizo ya vitendea kazi. Aidha, baadhi ya watumishi wa vyombo hivi wametumbukia katika baa hili na hivyo kufanya zoezi zima la  kukabiliana na rushwa kuwa gumu.

8. Ingawa rushwa imeanza kuonekana wazi katika jamii ya Watanzania katika miaka ya 1970, hata hivyo rushwa hiyo iliwahusu wafanyakazi wa tabaka la chini na la kati (Low-level corruption). Hawa walidai na kupokea rushwa kukidhi mahitaji yao. Katika kipindi hicho viongozi wengi wa ngazi za juu walikuwa ni watu safi, wenye tamaa za kawaida na hawakujihusisha katika vitendo vya rushwa.

9. Mwanzoni mwa 1983 Serikali iliendesha msako wa wahujumu uchumi nchi nzima. Miongoni mwa malengo ya kampeni dhidi ya wajuhumu uchumi ilikuwa ni kupambana na watoa na wapokea rushwa. Pamoja na kwamba kampeni hiyo ilifanyika kwa kishindo kikubwa na watuhumiwa wengi kukamatwa na kuzuiliwa, vita hivyo havikufanikiwa.

Hii ilitokana na ukweli kwamba kampeni hiyo ililenga kwenye matukio na si kwenye viini vya tatizo. Hata hivyo, mafunzo yaliyotokana na zoezi hilo yalisababisha Serikali kubadili sera ya biashara ya ndani na kulegeza masharti ya biashara. Watu wenye fedha nje ya nchi waliruhusiwa kuagiza na kuingiza nchini bidhaa na kwa hivyo kupunguza rushwa iliyokuwa imeshamiri katika nyanja ya biashara iliyokuwa imeshikiliwa na mashirika ya umma.

10.  Baada ya 1985 sura mpya ya rushwa ilianza kuonekana. Baada ya kulegeza masharti ya biashara ya ndani, misingi muhimu ya kisiasa na kijamii iliyotawala maisha ya raia, hasa watumishi wa umma ilianza pia kulegezwa. Sambamba na mabadiliko haya, rushwa ilianza kunyemelea ngazi za uongozi. Kufikia miaka ya mwanzoni mwa 90 rushwa ilishamiri ndani ya tabaka la uongozi wa juu (High-level corruption). Tatizo hili lilitokana na mambo yafuatayo:

 

(i) Kuwepo kwa fedha nyingi katika uchumi

Nyongeza kubwa iliyoletwa na ukuaji wa biashara baada ya ulegezaji wa masharti ya biashara, ilisababisha kuwepo kwa wingi wa fedha kwenye mikono ya wachache na ambayo iliwapa matajiri hao tamaa ya kununua haki ambayo hawakustahili. Hii ilikuwa ni pamoja na ukwepaji wa kodi, ulanguzi, ulaghai wa ardhi, biashara haramu kama ya madawa ya kulevya na uingizaji wa bidhaa zenye ubora hafifu. Viongozi wachache walishawishiwa na wenye fedha na kukubali kutimiza tamaa hizi.

 

(ii) Ukaribu wa wafanyabiashara na viongozi

Mwanzoni mwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Pili, viongozi wa kisiasa walijenga uhusiano wa karibu sana na wafanyabiashara, hasa wenye asili ya Kiasia. Baadhi ya wafanyabiashara hao walishiriki katika tafrija mbalimbali zilizohudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kununua picha, saa au kalamu za viongozi hao na hata mikufu, vidani na hereni za wake zao. 

Kwa kufanya hivyo walipiga picha pamoja na viongozi. Hawa walizitundika picha hizo madukani na maofisini mwao na kuonyesha jinsi walivyo karibu na viongozi katika jumuiya zao. Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa karibu na viongozi walikusanya pesa kwa madai kuwa walikuwa wakiwapelekea viongozi.

Ukaribu uliojitokeza baina ya viongozi na wafanyabiashara ulisababisha viongozi waingilie shughuli za watendaji na kufanya maamuzi kuwasaidia baadhi ya wafanyabiashara. Baadhi ya maamuzi hayakufanywa kwa kuzingatia masilahi ya taifa, bali kwa manufaa yao binafsi na wafanyabiashara hao. Hali hii ilidhihirisha wazi ni jinsi gani viongozi walikuwa wamejitumbukiza katika vitendo vya rushwa, jambo ambalo lilichochea zaidi ongezeko la rushwa nchini.

 

Kwa mwendelezo wa ripoti hii, usilikose JAMHURI wiki ijayo.

Please follow and like us:
Pin Share