Na Mwandishi Wetu,JammhuriMed8a, Arusha

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini nchini (RITA) umeunda Kamati ya muda itakayochukua majukumu ya Bodi ya Udhamini iliyomaliza muda wake ya Taasisi ya Arusha Muslim sambamba na kuunda kamati ya maalumu ya uchunguzi itakayofuatilia malalamiko ya wanachama kuwatuhumu viongozi hao kuhujumu mali za taasisi hiyo.

Akizitambulisha kamati hizo katika kikao kilichojumuisha uongozi wa RITA, viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Arusha, viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA ), viongozi wa Arusha Muslim pamoja na wanachama wa msikiti huo, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi ameziagiza kamati hizo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu.

“Nimeiagiza Bodi iliyomaliza muda wake kuwasilisha RITA taarifa ya mapato na matumizi,” alisema Kanyusi na kuiagiza kamati ya mpito kuhakikisha inafanya marekebisho ya katiba na uchaguzi unafanyika ndani ya siku 60 ili kupata viongozi watakaosimamia taasisi kwa mujibu wa katiba.

Aidha, Kanyusi ameaitaka pia Kamati maalumu ya uchunguzi kukamilisha kazi iliyopewa ndani ya kipindi cha siku 14 na kuwasilisha taarifa ya uchunguzi RITA.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Khamana Simba ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo kwenye kikao hicho aliwataka wanachama wa Arusha Musilim kuwa watulivu na kwamba serikali ipo pamoja nao kuhakikisha mgogoro huo wa muda mrefu unapata ufumbuzi wa kudumu kwa amani, utulivu na haki.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan inafuatilia kila kitu na ninawahakikishia kuwa ufumumbuzi wa tatizo lenu utapatikana,” amesema katibu tawala huyo na kuwataka waendelee kuwa wamoja na watulivu.

Baadhi ya wanachama Mustapha Mohamedi na Kassim Collins waliipongeza serikali kwa kufuatilia mgogoro huo huku wakiomba hatua zichukuliwe kwa watakaobainika kuwa wamefanya ubadhirifu.

Naye, Naibu Kabidhi Wasii Mkuu, Irene Kesulie aliwatoa hofu wanachama wanaoidai taasisi hiyo kwamba wafuate taratibu ikiwemo kuandika barua na kuziwasilisha RITA ili taratimu za kisheria ziweze kufuatwa na wapate haki yao.

“RITA kama ipo hapa kusimamia haki za wanachama kwa wa sheria na katiba. Tunawasihi endeleeni kuwa watulivu na wavumilivu,” amesema Irene.