Komanya Kitwala (aliyevaa kaunda suti ya bluu) akipokea msaada wa nondo kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule.

Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Tabora, Sofia Jongo, ameingilia kati ubabe wa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Komanya Kitwala, akimtaka kufuata sheria katika uongozi wake.

Hayo yamejitokeza takriban mwezi mmoja tu baada ya JAMHURI kuripoti taarifa za DC kutumia madaraka yake kuwakamata watu na kuwashitaki kwa madai ya ‘kuwachafua’ viongozi kwenye mitandao ya kijamii ya ‘Whatsapp’.

Waathirika wa kamatakamata ya DC ni ‘ma-admin’ (viongozi) wa makundi ya Whatsapp na wachangiaji kadhaa wa hoja zinazodaiwa kumkwaza Komanya.

JAMHURI linafahamu kuwapo kwa mgogoro na mivutano ya kiuongozi baina ya mkuu wa wilaya hiyo na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora, huku viongozi wa chama wakidai kuwa chanzo chake ni ubabe na jeuri ya DC.

Hata hivyo, kwa sasa mgogoro huo unaelekea kupata suluhu baada ya ziara ya Rais John Magufuli mwezi uliopita, aliyeelekeza kutafutwa kwa suluhu ya kudumu ili kuwapelekea wananchi maendeleo.

Akizungumza na JAMHURI, RPC Sofia anasema amezungumza na Komanya na kumshauri ajiepushe na kutumia amri na matamko yasiyozingatia sheria dhidi ya wananchi.

“DC alikuwa anatuandikia barua mara kwa mara akitaka tumkamate huyu au yule. Kisheria hili lilikuwa linaleta mkanganyiko.

“Mazungumzo yangu na DC yalifanyika kabla ya ziara ya Rais Magufuli hapa Tabora. Nilimkanya aache tabia hiyo, kisha nikapeleka taarifa kwa mkuu wa mkoa,” anasema RPC.

Anasema hata agizo la Rais kwa mkuu wa mkoa tayari limeanza kufanyiwa kazi, pia Kitwala ameanza kuufanyia kazi ushauri aliopewa.

“Tumemshauri ajiepushe na mivutano na viongozi wa kisiasa ili shughuli za kiserikali ziendeshwe kwa kuzingatia kanuni na sheria za kiutawala,” anasema Sofia.

Akizungumza na gazeti hili akiwa jijini Dodoma kikazi, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Philemon Sengati, anakiri suala hilo kufikishwa ofisini kwake.

Hata hivyo, Dk. Sengati hakuwa katika nafasi nzuri ya kufafanua zaidi, kwa kuwa hakuwapo ofisini kwake, akiahidi kuzungumza kwa kina atakaporejea Tabora.

Awali DC Komanya alilalamikiwa na viongozi wa Kamati ya Siasa ya CCM wilayani humo, akiwamo katibu wa kamati hiyo, Nicholaus Malema, akidai DC haonyeshi ushirikiano.

“DC hataki kushirikiana na mtu yeyote wilayani hapa, anafanya anavyojua mwenyewe. Hatekelezi maelekezo ya chama yanayotolewa na Kamati ya Siasa ya wilaya. Anadai kuwa yeye anaripoti kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, basi,” anasema Malema.

Mvutano huo ulishika kasi wakati DC Kitwala alipoandikiwa barua na Malema akitakiwa kuwasilisha nyaraka za utekelezaji wa Ilani ya CCM kabla ya Januari 20, mwaka huu; akagoma.

Baada ya kugoma, kamati hiyo ilimuita DC Januari 7, mwaka huu kwa lengo la kumshauri lakini hakuwa tayari kuwasikiliza akidai kwamba viongozi hao hawana uwezo wa kumshauri.

“Hana imani kama anafanya kazi chini ya chama ngazi ya wilaya. Akiagizwa na chama anaona kama hatendewi haki.

“Hilo alilithibitisha kwa kinywa chake. Alisema mimi niondoe hisia kwamba yeye ni mdogo (kimadaraka/kiuongozi) kwangu,” anasema Malema.

Mbali na hayo, Kitwala analalamikiwa kuendekeza migogoro isiyo na maana na wasaidizi wake, akiwashitaki na kesi kufikishwa mahakamani.

“Ana mgogoro na viongozi karibu idara zote zilizo chini yake, akiona unamkosoa, hachelewi kuliagiza Jeshi la Polisi likukamate,” anasema Malema.

Mmoja wa viongozi waandamizi wa chama wilayani humo amelieleza JAMHURI kuwa tatizo la Kitwala ni kutotambua maadili ya kiuongozi na kwamba anapenda anachokisema yeye kila mmoja akubaliane nacho.

 “Wajumbe wengi hupingana na hoja zake, anapokuwa kwenye vikao vya Kamati ya Siasa, anapaswa kutambua ameingia kama mjumbe, si DC,” anasema kiongozi huyo.

Malalamiko mengine dhidi ya Kitwala ni kuwanyanyasa wananchi wakiwamo wasaidzi wa mama lishe, wahudumu wa klabu za pombe (mabaamedi) na nyumba za kulala wageni, akiwalazimisha kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali (maarufu kama vitambulisho vya Magufuli) kinyume cha utaratibu.

Vitambulisho hivyo, kwa mamalishe, hutakiwa kumilikiwa na mjasiriamali aliyewaajiri wengine na si wote waliopo eneo hilo.

Aidha, wananchi wanailalamikia ofisi ya DC kuwabagua kimatabaka, kwa madai kuwa amewahi kuweka tangazo linalowakataza kufika ofisini hapo wakiwa na usafiri wa baiskeli au pikipiki. 

Emmanuel Basonga, mkazi wa Tabora Mjini anasema: “Aliweka bango hilo. Kwamba ukiwa na shida ya kiofisi katika ofisi yoyote iliyo karibu na yake usifike hapo na baiskeli au pikipiki, ila ni magari tu.

“Tangazo lile liliwaongezea gharama watu wanaotoka vijijini, kwani walilazimika kuwapa fedha watu kuwalindia usafiri wao. Sidhani kama hii ni sahihi kufanyika katika ofisi za umma!”

JAMHURI limeelezwa kuwa gharama ya ulinzi wa baiskeli na pikipiki ilikuwa kati ya Sh 500 na Sh 1,000.

Hata hivyo, tangazo hilo liliondolewa siku chache kabla ya ziara ya Rais Magufuli.

JAMHURI limemtafuta DC Komanya kutaka ufafanuzi wa madai hayo, lakini akakataa kusema lolote akidai hawezi kuyatolea ufafanuzi kwa njia ya simu.

“Si utaratibu wa serikali kufanya kazi kwa kutumia simu. Njoo ofisini au mtume mwakilishi wako wa Tabora aje hapa,” amesema Komanya.

Hata alipopelekewa maswali kwa njia ya SMS na kukumbushwa kwamba kwa mujibu wa sheria mawasiliano ya kielektroniki yanatambulika, Komanya hakuwa tayari kusema lolote.

Komanya Kitwala (aliyevaa kaunda suti ya bluu) akipokea msaada wa nondo kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule.

By Jamhuri