*Halmashauri Dar zawahonga mil. 25/-
*Mbunge CCM asema Chadema ‘inawaovateki’
Kamati ya Kudumu y Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa inatajwa kuwa miongoni mwa kamati zinazonuka rushwa, na kuna habari kwamba wabunge wengine watatu wataunganishwa na mwenzao katika kesi ya kuomba na kupokea rushwa.

Tuhuma za rushwa sasa zinawazunguka wajumbe wake 15 huku mmoja wao, Mbunge wa Bahi, Omary Badwel (CCM), akiwa amefikishwa mahakamani akituhumiwa kuomba na kupokea rushwa.

Anatuhumiwa kupokea Sh milioni moja kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.

Kukamatwa kwa Badwel ni kutimia kwa maneno ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aliyoyatoa bungeni Juni 13, mwaka jana, lakini yakapuuzwa.

Katika tukio ambalo ni la nadra kutokea bungeni, mbunge huyo aliwataja wabunge wawili kati ya watatu aliosema ni wala rushwa ndani ya kamati hiyo. Akitambua kuwa Kanuni za Bunge zinamtaka mbunge kuzungumza jambo alilo na uhakika nalo, Kafulila hakusita kuwataja kwa majina wabunge hao.

Alisema; “Bahati mbaya sana ni kwamba katika dhana nzima ya kusimamia hayo matumizi ambayo tunayapanga na kuyapitisha, kuna tatizo kubwa sana la mfumo ambao una udhaifu wa kifisadi. Kuna waziri, kuna wabunge wanakula rushwa, nimekamata mbunge anaomba rushwa kwenye halmashauri wakati halmashauri ziko chakavu, wanalia na njaa, mipango haiendi, nilikamata mbunge anaomba rushwa.

“Wamo humu ndani, wapo humu kuna akina Zambi, Badwel. Nimewakamata na nimechukua hatua, nchi hii haiwezi ikaendelea kwa staili hiyo, haiwezekani.”

Godfrey Zambi ni Mbunge wa Mbozi Mashariki kupitia CCM.

Kutokana na kauli ya Kafulila, Mbunge wa Muhambe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti, George Simbachawene.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa kujua, kwa sababu kabla ya mzungumzaji aliyepita, Mheshimiwa Kafulila wakati amezungumza, ametaja wabunge ambao wanakula rushwa. Sasa tungependa kujua wewe unachukua hatua gani na pia tungependa tuwajue kwa sababu hapa Watanzania wanaliangalia Bunge zima, sasa hatuwezi tukaacha suala la mtu kutaja kwamba fulani anakula rushwa, fulani amekula rushwa, tuwajue hawa watu ni akina nani na Bunge liazimie, siyo tuache jambo la msingi kama hili kwa Taifa juu juu tu. Tungeomba Mheshimiwa Kafulila awataje hawa watu na Bunge litoe uamuzi kwa sababu ni jambo la msingi sana kwa Taifa.”

Simbachawene alisema kwamba katika utoaji mwongozo, kiti kinaweza kutoa jibu la hapo hapo, lakini pia kinaweza kutoa jibu kwa wakati mwafaka. Sasa ni mwaka mzima jibu la hoja hiyo likiwa halijatolewa na Simbachawene ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

Tukio la wabunge hao wawili waliotajwa, na mwingine mwanamke ambaye hakutajwa bungeni kutokana na muda wa Kafulila wa kuzungumza kumalizika, bado linawafanya wengi wajiulize kama uongozi wa Bunge una dhamira ya kweli ya kupambana na adui rushwa. 

Kabla ya kulizungumza bungeni, Kafulila alipeleka taarifa ya maandishi kwa Spika Anne Makinda kwa maandishi. Pamoja na Spika, taarifa hiyo ilipelekwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kwa Katibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Mswige Bisile.

Maelezo yanaonyesha kuwa Kafulila alichukizwa na kitendo cha wabunge hao kudai rushwa wakati Kamati ikifanya ukaguzi katika halmashauri za wilaya za Mkoa wa Tanga. Jambo hili lilitokea Mei 11, mwaka jana.

Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa inaundwa na Augustine Mrema (Mwenyekiti), Iddi Azzan (Makamu Mwenyekiti), Riziki Lulida, Dk. Zabein Mhita, Zambi, Subira Mgalu, Hasinain Murji, Suzan Kiwanga, Abdallah Rashid Ali, Kafulila, Badwel, Abdul Mteketa, Tauhida Nyimbo, Joseph Selasini na  Kuruthum Mchuchuli.

3769 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!