CCM, Chadema waingiwa shaka
Wakati wajumbe kadhaa wa Kamati hiyo wakituhumiwa kwa ulaji rushwa uliokithiri, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wake kinapata kigugumizi cha kumwajibisha Badwel ambaye tayari kafikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.

Mmoja wa wabunge wa CCM anasema chama hicho hakiwezi kutangaza kumsimamisha Badwel, kwa kuhofu kuwa kufanya hivyo kutaviongezea umaarufu vyama vya upinzani.

“Hapa ilipaswa Badwel asimamishwe ubunge na ikibidi uitishwe uchaguzi mdogo wa ubunge. CCM hatuwezi kukubali uchaguzi mdogo kwa mazingira haya ya sasa ya Chadema ambayo inaonekana kukubalika zaidi,” amesema.

Kwa upande wa Chadema, ukimya wa chama hicho juu ya suala la wabunge kutuhumiwa kula rushwa nalo linazua utata. Wapo wanaoamini kuwa ukimya huo huenda ukawa unatokana na hofu ya chama hicho, hasa ikizingatiwa kuwa kina wabunge katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, wapo wachambuzi wa mambo wanaosema sababu ya msingi ni kutokana na hoja hiyo kuasisiwa na Kafulila, mtu waliyemtimua uanachama. Kafulila alikuwa mwanachama wa Chadema, lakini alipowatuhumu viongozi wa juu kwa ufisadi wakamtimu akaenda NCCR-Mageuzi, ambako alishinda ubunge wa Kigoma Kusini na sasa analipua mabomu bungeni.

By Jamhuri