TABORA

Na Moshy Kiyungi

Simulizi zinasema zamani wenyeji wa Shinyanga walikuwa wakiokota mawe yanayong’ara bila kutambua kuwa ni mali.

Wazungu walipoyaona mawe hayo mara moja wakatambua kuwa ni almasi, madini yenye thamani.

Inadaiwa kuwa wakaanza kuwalaghai wenyeji kwa kubadilishana mawe hayo na shanga!

Maeneo mengi vijijini yamejaa vipaji vya kila aina, hususan upande wa sanaa, lakini hakuna fursa ya kuviibua. 

Mathalani, vipaji vingi vya kuimba huko vijijini huishia kuburudisha wanywaji wa pombe za kienyeji au katika harusi na shughuli nyingine za kijamii, huku wakituzwa fedha na wakati mwingine pombe.

Katika miaka ya 1980, thamani ya bendi ya muziki wa asili ya Tatu Nane haikujulikana wala kukubalika nchini ingawa nje ya nchi ilikuwa maarufu sana ikiutangaza utamaduni wa Kitanzania.

Mtunzi mahili wa kundi hilo, Omari Naliene, alikuwa na kipaji cha kupuliza filimbi mbili akitumia matundu ya pua, alikubalika sana kimataifa alikopata mikataba lukuki.

Unamkumbuka Saida Karoli? Msanii huyu aliibuka ghafla jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa miaka ya 2000 akitokea mkoani Kagera.

Kilichompa umaarufu ni kibwagizo cha ‘chambua kama karanga’, kilichokubalika na kutia fora katika nyimbo zake nyingi.

Umahiri wa Saida katika kucheza huku akipiga ngoma na kuimba Kihaya na Kiswahili kulimpandisha chati miaka hiyo.

Kama ilivyokuwa kwa almasi za Shinyanga, kipaji cha Saida nusura kiishie Kagera alikozaliwa Aprili 4, 1976 katika Kijiji cha Rwongwe.

Mwanamama huyo hakusoma zaidi ya darasa la tano kwani baba yake hakuthamini elimu.

Ingawa mila na desturi za ukoo wao zinawazuia watoto wa kike kujishughulisha na muziki, mama yake Saida ambaye kwa bahati nzuri alikuwa na kipaji cha muziki, alimtia moyo na kumfundisha masuala mbalimbali ya muziki.

Akiwa na umri wa miaka 20, mama yake alifariki dunia akimwachia Saida amana ya kipaji cha uimbaji na upigaji ngoma.

Kwa maisha ya kijijini, vipaji hivyo havikuonekana kuwa na thamani yoyote.

Mzungu aliyetambua thamani ya almasi kwenye kipaji cha Saida, ni Mkurugenzi wa Kampuni ya FM Production, Felician Mutta.

Akiwa katika shughuli zake za kikazi mkoani; kutafuta wasanii wenye vipaji kwa ajili ya kuwaendeleza, alikiona kipaji cha Saida akiwa kijijini kwao, mara moja akamhamishia Dar es Salaam.

Kitu cha kwanza ilikuwa ni kumfundisha kuimba Kiswahili, lugha ambayo ilikuwa ikimpa shida kiasi fulani.

Baada ya mazoezi matatu, ilimchukua Saida wiki tatu kukamilisha kurekodi wimbo wake wa kwanza, ‘Maria Salome’, ulioitikisa Dar es Salaam kisha nchi nzima na baadaye Afrika Mashariki na Kati.

Septemba 2, 2001, Saida, almasi iliyoibuliwa kutoka Kagera, akazindua albamu ya ‘Maria Salome’ iliyojaa vionjo vingi vya Kihaya.

Kwa wiki sita baada ya hapo, wimbo huo ulikuwa namba moja katika nafasi 10 za juu katika vituo karibu vyote vya redio za burudani Afrika Mashariki.

Albamu hiyo ilisababisha Saida kufanya ziara nyingi huko Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.

Miezi michache baadaye, kiongozi mmoja wa kimila nchini Uganda, Kabaka wa Buganda, akamualika Saida kushiriki sherehe kubwa ya kitamaduni.

Saida alialikwa kama mmojawapo wa wanamuziki wenye mafanikio makubwa Afrika.

Sherehe hizo zilimpandisha chati Saida nchini Uganda hata akapendekezwa kuwa mwanamuziki wa mwaka.

Katika kuthibitisha ubora wa wimbo wa ‘Maria Salome’, mwaka 2016 msanii wa kizazi kipya, Diamond Platinumz, aliurudisha kwenye chati baada ya kuurekodi upya.

Nyimbo zake nyingine zilizotamba ni ‘Kaisiki’ na ‘Ndombolo ya Solo’.

Bila shaka Saida ni maarufu sana Uganda kutokana na ukweli kwamba lugha anayoitumia mara nyingi, Kihaya, inashabihiana na Kiganda, lugha inayotumiwa na Waganda wengi.

Saida amejaaliwa haiba na sauti nyororo yenye mvuto ikinogeshwa na vionjo anuwai vya kijadi katika nyimbo zake takriban zote.

Ni kawaida ya wasomi wanaotokea Kagera kupenda kutumbukiza angalau neno moja la Kiingereza katika sentensi wakati wa mazungumzo, Saida naye, japokuwa si msomi, hujaribu kuingiza vionjo vya Kiingereza kwenye nyimbo zake, kama maneno; ‘Oraita’ akimaanisha ‘alright’.

Ukitaka kufahamu ukubwa wa kipaji cha Saida, angalia ‘video’ zake katika nyimbo za ‘Kasimile Katonda’, ‘Nsenene’ na ‘Karibatano’.

Senene ni mdudu anayependwa mno na wenyeji kutoka mkoani Kagera, wengine hufikia kuzisafirisha kwenda kwa ndugu zao walioko nje ya nchi.

Ukifika vijijini utakuwa umepewa heshima kubwa iwapo utakirimiwa kwa senene, rubisi na kahawa kavu.

Juni 2003, Saida alitoa albamu ya ‘Mapenzi Kizunguzungu’ na kuliteka soko la muziki kwa mara ya pili.

Kwa kuthamini mchango wa Mutta katika maisha yake ya muziki, Saida hakuona ajizi kutoa shukrani zake na kukiri kwamba sifa na mafanikio aliyoyapata ni uwezo wa Mungu aliyemuwezesha Mutta kufika kijijini kwao na kukiona kipaji chake.

Saida Karoli ameajiri wasanii wengi pamoja na wanenguaji katika kundi lake. Siku za karibuni amepakua kibao cha ‘Orugambo’ na video yake imenunuliwa kwa wingi.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0736331200, 0713331200 na 0767331200.

256 Total Views 12 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!