Mapinduzi ya kijeshi, ulafi wa madaraka Afrika

DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Baada ya kutawaliwa kwa miaka zaidi ya 70, hatimaye nchi za Afrika zilianza kujitawala na kuunda jumuiya mbalimbali chini ya jumuiya mama, OAU na baadaye AU zenye madhumuni ya kulinda amani, umoja na mipaka ya Afrika.

Nchi nyingi za Afrika zimepata uhuru wa bendera huku zikikabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo ya uchumi tegemezi, ukuaji mdogo wa demokrasia uchu wa madaraka na elimu duni ya uraia kwa wananchi.

Baada ya nchi za Afrika kujitawala na kuunda serikali zao kwa mujibu wa katiba ya kila nchi. Vyombo vya ulinzi na usalama vikapewa jukumu la kulinda nchi, mipaka, raia na mali zao. Tofauti kabisa na inavyotokea katika baadhi ya nchi hizo.

Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuja na hatua mbalimbali za fikra katika mageuzi ya siasa na uchumi imara baada ya uhuru.

Mwalimu anasema uhuru ni kazi, kauli ambayo ilitoa funzo kwamba kupata uhuru haikuwa kazi ya lelemama na kuwataka Waafrika kuheshimu uhuru na kuulinda kwa nguvu zote.

Kutoka ‘Uhuru ni Kazi’ ilifuata kauli na fikra ya ‘Uhuru na Kazi’, kauli ambayo ilimaanisha kupata uhuru tu pekee haitoshi, lazima wananchi washirikiane na serikali kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo endelevu.

Katika insha zake, Mwalimu amewahi kuandika: ‘Uhuru na Ujamaa’. Aliamini katika ujamaa kwa kumaanisha kwamba watu wakiishi pamoja kwa amani na upendo ni rahisi kufanya kazi na kuleta ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Kama hiyo haitoshi, Mwalimu Nyerere anasema uhuru na maendeleo ni vitu viwili ambavyo haviwezi kutenganishwa. Taifa lenye uhuru kamili ni lile ambalo lina uwezo wa kujitegemea.

Mwalimu alianza kuangalia mfumo mzima wa dunia kama ambavyo unahitaji hatua zichukuliwe ili kuendeleza maadili hayo ya usawa wa binadamu na kuweka rasilimali za nchi katika mikono salama ya umma huku akikemea uchu wa madaraka na tamaa za viongozi kujilimbikizia mali.

Wakati Mwalimu Nyerere akihubiri hayo, Dk. Kwame Nkrumah, Rais wa Kwanza wa Ghana, yeye akawasisitiza viongozi na watawala wa Afrika kwamba watafute kwanza ufalme wa siasa kama njia sahihi ya kukuza uchumi na maendeleo ya bara hilo.

Katika hatua nyingine, nchi za Afrika zilianza kurejea katika mfumo wa vyama vingi vya siasa miaka ya 1990 kwa madhumuni ya kupanua wigo na uhuru wa wananchi katika uwanja wa siasa.

Pamoja na malengo mazuri ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa, bado mfumo huo unakumbana na vikwazo mbalimbali vinavyosababisha migogoro na machafuko ya kisiasa miongoni mwa nchi za Afrika.

Chaguzi nyingi katika mfumo huo zinakabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwamo umaskini, ukosefu wa usawa, ujinga, rushwa na siasa zisizo na maadili. 

Vikwazo vingine ni pamoja na kukata tamaa ya kisiasa, woga wa siasa, utamaduni wa kisiasa uliolazimishwa, ubaguzi na kushamiri kwa uongozi wa mabavu.

Demokrasia inaelezwa kuwa ni njia ya kutawala ambayo mawazo ya watu hufikiriwa katika kufanya uamuzi wa umma na wananchi kushirikishwa.

Wananchi walifanyiwa wasichokitaka na watawala matokeo yake ni vurugu na machafuko ya kisiasa yanayosababisha vita kwa wenyewe na kuzalisha wakimbizi.

Migogoro na machafuko ya kisiasa yameendelea kuzikumba baadhi ya nchi za Afrika na kusababisha kuundwa kwa serikali za mpito ambazo pia zimeendelea kupambana na nguvu za kijeshi kwa kila upande kung’anga’ania madaraka huku raia wakiendelea kutaabika na shughuli za uchumi kudorora.

Sudan ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayoendelea kukumbwa na migogoro na machafuko ya kisiasa kwa miaka mingi hata baada ya taifa hilo kugawanyika kuwa mataifa mawili; yaani Sudan na Sudan Kusini mwaka 2011, hatua ambayo ilitazamiwa kutuliza ghasia katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta. 

Maandamano yalianza kutokea tena Desemba 2017 yaliyochochewa na kupanda kwa bei ya mikate na mafuta, hatua ambayo ililenga pia kumuondoa madarakani Rais Omar Al-Bashir.

Hatua hiyo ya maandamano ilitokana pia na kushutumiwa kwa utawala wa Al-Bashir kusababisha kudorora kwa uchumi wa Sudan, kuminywa kwa demokrasia na kung’ang’ania  madaraka.

April 11, 2019, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan Burhan, alifanikisha mapinduzi ya kumuondoa madarakani Rais Omar Al Bashir ambaye aliiongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1989 hadi 2019, ukiwa ni utawala wa miaka 30.

Kama ilivyokuwa mwaka 2019, maandamano yaliaanza kwa wiki kadhaa kabla ya jeshi kuingilia kati na kumuondoa Bashir ambaye naye alichukua madaraka ya nchi hiyo kwa kupindua iliyokuwa serikali ya ushirika iliyoongozwa na Waziri Mkuu Sadiq Al-Mahdi.

Oktoba 25, mwaka huu, Jeshi la Sudan likiongozwa na Jenerali al-Burhan lilichukua  udhibiti wa serikali ya kiraia na kutangaza mapinduzi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa serikali ya kiraia, Abdallah Hamdok, alichukuliiwa na kuwekwa mahali pasipojulikana. Sababu ya Hamdok kushikiliwa ilielezwa kwamba ni kiongozi huyo kugoma kutoa ushirikiano kwa jeshi wakati wa kufanyika kwa mapinduzi hayo.

Kiongozi wa jeshi, Jenerali al-Burhan, alitoa tangazo hilo kupitia hotuba yake kwa njia ya televisheni kwamba serikali ya mpito ya Sudan imevunjwa.

Kwa mujibu wa jenerali huyo, sasa jeshi litajaribu kurejesha nchi katika mkondo wa demokrasia na kukabidhi mamlaka kwa serikali ya kiraia baada ya Uchaguzi Mkuu wa Julai 2023.

Mapinduizi yanayoendelea nchini Sudan ni mzozo wa hivi karibuni katika kipindi cha machafuko nchini humo. Hayo ni matokeo ya kutoaminiana kati ya viongozi wa kijeshi na wa kiraia.

Pande hizo mbili zimekuwa zikigawana madaraka tangu mwaka 2019, kufuatia kupinduliwa kwa Rais al-Bashir, nchi iliingia kwenye utawala wa mpito.

Viongozi wa jeshi waliendesha nchi pamoja na raia kupitia kamati ya pamoja inayojulikana kama Baraza Kuu.

Al-Bashir ambaye alikuwa akitafutwa na Mahakama ya Kimataifa (ICC) kuhusu uhalifu wa kivita kwa kuandaa uhalifu dhidi ya binadamu katika Jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan, ameshakabidhiwa kwenye mahakama hiyo.

Mbali na Sudan, Mei mwaka huu, aliyekuwa Rais wa mpito nchini Mali, Bah Ndaw na waziri wake mkuu, Moctar Ouane, waling’olewa madarakani siku moja baada ya kukamatwa na jeshi.

Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya umma (ORTM), Assimi Goita, anasema: “Mimi ndiye niliyewaondoa madarakani viongozi hao wawili, Rais Bah na Waziri Mkuu Ouane kutokana na kuvunja vipengele vya utawala wa mpito.”

Kama hiyo haitoshi, Septemba mwaka huu, Luteni Kanali Mamady Doumbouya aliongoza mapinduzi yaliyomng’oa madarakani Rais Alpha Conde (83) wa Guinea ambaye ni kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo.

 Conde alibadilisha katiba mwaka 2010 ili agombee kwa muhula wa tatu, tamaa ambayo imekaribisha mapinduzi ya kijeshi kuchukua nafasi.

Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama, aliwahi kusema Afrika si tu inahitaji viongozi imara, bali inahitaji mfumo imara wa uongozi.

Serikali za mpito si suluhisho la kudumu la uongozi wa kidemokrasia. Viongozi wanaoingia madarakani waongoze kwa sheria na kuzingatia matakwa ya katiba ya nchi. Tusipomaliza vita, vita vitatumaliza.

0755 985 966