Wananchi washirikishwe kutoa maoni miaka 60 ya Uhuru wetu

Serikali imetangaza utaratibu katika kuelekea kwenye kilele cha sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) ifikapo Desemba 9, mwaka huu.

Tunaupongeza utaratibu wa wizara kujitokeza kuainisha mafanikio ya kisekta yaliyopatikana kwa muda wote huu wa miongo sita. 

Hii ni hatua nzuri, maana inasaidia kuwafanya Watanzania vijana ambao ndio walio wengi, kufahamu tulikotoka, tulipo na tunakoelekea.

Pamoja na kupongeza hatua hiyo, tungeshauri yawepo makongamano ya wazi yanayowahusisha zaidi wananchi wa kawaida ili wapate fursa ya kutoa maoni yao.

Maoni hayo yahusu mwelekeo wetu kama Watanzania katika kuulinda na kuudumisha Uhuru wetu tulioupata kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961.

Kuwepo makongamo ambayo watu wa kawaida kabisa wanaweza kupewa fursa ya kueleza maoni yao na nini kifanyike ili kuulinda Uhuru wetu.

Tunapendekeza hivyo kwa sababu mara nyingi shughuli muhimu na nyeti za umma kama hizi zimekuwa zikihodhiwa na viongozi, hasa wanasiasa na kuwaweka kando wahusika wakuu ambao ni wananchi wa kawaida.

Pamoja na kuwapo kwa hotuba za viongozi, kusikiliza maneno ya wananchi kwa muda kama huu ni jambo muhimu. Mathalani, kumeanza kuwapo nyufa kadhaa katika taifa letu. Baadhi ya nyufa hizo ni kuporomoka kwa maadili, udini, ukabila na ukanda.

Baadhi ya watu, hasa wanasiasa wameanza kuonyesha vimelea vya ubaguzi, hivyo kuhatarisha uhuru wetu. Mambo ya aina hii wananchi wapenda nchi yao wangependa wapate fursa ya kuyaeleza na ikibidi kupendekeza njia za kuyatokomeza. Wanasiasa wameshasikika sana, sasa tuwape nafasi wananchi.

Wakati tukipata Uhuru, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwatangaza maadui watatu – Ujinga, Maradhi na Umaskini. Vita dhidi ya maadui hawa ni ya kudumu. Wananchi wapewe nafasi waeleze ni kwa namna gani wanaiona vita inavyoendeshwa dhidi ya hao maadui, na nini kifanyike ili kuendelea kupata ushindi.

Kwa mfano, mfumo wetu wa elimu unakidhi matarajio ya Tanzania ya miaka mingine 60 ijayo? Tutumie lugha gani kufundishia? Je, kuwatengea wamachinga maeneo badala ya kuwaza zaidi kwenye kilimo na uzalishaji mali kutasaidia kutokomeza umaskini wetu? Je, nini kifanyike katika kuhakikisha Watanzania wanakabiliana na maradhi, hasa yasiyo ya kuambukiza?

Wananchi wa kawaida wanaweza kuwa na majibu mazuri sana kwa maswali haya. Ndiyo maana tunasisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi, kuanzia ngazi ya serikali na kwenye vyombo vya habari.

Muhimu kuliko yote ni kuhakikisha Watanzania wote wanashiriki kuulinda Uhuru wetu ili Tanzania iendelee kuwa taifa moja lililo imara na lenye watu wanaoishi kwa amani, upendo na mshikamano. 

Sote tuna wajibu wa kuhakikisha raia na wageni wanaishi kwa uhuru na kwa haki kwa mujibu wa sheria za nchi. Mungu Ibariki Tanzania.