Na Mwandishi Wetu, JAMHURI MEDIA, Dar es Salaam.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa hukumu ya miaka 22 jela iliyotolewa kwa Mama Maria Ngoda wa Iringa, kufuatia kosa la kukutwa na nyama ya swala yenye thamani ya shilingi laki tisa na elfu nne mia saba hansini saba na senti moja (904,757.1/E).

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dkt. Anna Henga katika taarifa iliyotolewa l leo Novemba 08, 2023 ambapo imeeleza kuwa “Tukio hilo linaonyesha changamoto kubwa katika mfumo wa sheria nchini, na linazidi kuchochea wito wa kufanyika marekebisho muhimu katika mifumo ya sheria.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) Dkt. Anna Henga

“ Ni wazi kuwa nchini kumekuwepo na mifano mingi ya matukio ya uhalifu mkubwa ambapo watuhumiwa wamekuwa wakipewa adhabu ndogo au hata kutopewa adhabu kabisa.”Amesma Dkt Henga.

Amesema , Ripoti za ufisadi wa mabilioni ya fedha za umma kutoka Mamlaka ya Ukaguzi na Utekelezaji wa Serikali (CAG) zinaleta maswali mengi juu ya uzingatiaji wa sheria na utoaji wa haki na kupelekea maswali muhimu kuhusu usawa wa sheria na jinsi inavyowashughulikia raia. Swali la msingi linabaki: Je, hukumu hii inalingana na uzito wa kosa? Hukumu ya miaka 22 jela kwa Mama Maria ni adhabu kali sana.

“Hili ni jambo linalozua hisia za simanzi na maswali kuhusu utaratibu wa kutoa hukumu za jinai”.

Aidha ameeleza kuwa, inaonesha jinsi mfumo wa sheria unavyoweza kuwa mkali kwa watu wa tabaka la chini na kutokutazama kwa makini makosa makubwa yanayofanywa na watu wenye hadhi, ushawishi katika janii au hali nzuri ya kiuchumi.

 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetoa rai kwa wasimamizi wa Haki na sheria kuchunguza upya hukumu hiyo  na kuhakikisha kuwa Mama Maria anapata fursa ya kusikilizwa upya, kujitetea na kuhukumiwa kulingana na uzito wa kosa analodaiwa kufanya.

“Ni muhimu sana kuwa na mfumo wa sheria unaosimamia mazingira, nia, na hali ya watuhumiwa, na kutokutumia ubaguzi wa aina yoyote, iwe ni kwa misingi ya hali ya kiuchumi au ushawishi wa kijami ili kuhakikisha haki inatendeka na kuwa na mfumo wa sheria unaoweka kipaunbele cha usawa na haki kwa wote. Wote tuna wajibu wa kusimama kwa pamoja kudai haki kwa Mama Maria Ngoda na wanavwake wengine wanaopitia changamoto kama hizi.”

 LHRC imetaka uwepo wa sauti za mabadiliko pamoja na ushirikiano katika kutetea haki na usawa katika mifumo ya sharia.

By Jamhuri