Salfa mbovu ya Makonde pasua kichwa

Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Nani aliruhusu Kampuni ya Makonde kusambaza viuatilifu feki aina ya salfa  kwa wakulima wa korosho Mtwara? Hili linabaki kuwa miongoni mwa maswali magumu; JAMHURI linaripoti.

Japokuwa mamlaka zinamshikilia mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Makonde (jina tunalihifadhi kwa sasa) kwa ajili ya uchunguzi, lakini si Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ambao awali walifahamiaka kama TPRI wala Bodi ya Korosho (CBT) wenye majibu ya kueleweka kwa sasa.

Taasisi hizi mbili muhimu kwa maendeleo ya mkulima wa korosho, kwa sasa zinatupiana mzigo huu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Efraimu Njau, anakiri kukamatwa kwa tani 500 za shehena ya salfa iliyothibitishwa kuwa chini ya viwango ikiwa tayari imefikishwa kwa wakulima.

Awali, sampuli ya salfa hiyo ilipelekwa TPHA na ikabainika kuwa haijakidhi viwango stahiki na ikaamuriwa kuwa irudishwe ilikotengenezwa; lakini haikurudishwa, badala yake inasambazwa kwa wakulima.

“Tulijiridhisha kuwa haifai. Tukaamuru isifike kwa wakulima. Mzabuni hakutii mamlaka, tukashangaa kusikia inasambazwa kwa kutumia majina ya ‘wakubwa’,” anasema Njau.

Akiwa katika ziara mkoani Mtwara, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa, Shaka Hamdu Shaka, alionya kutumiwa kwa jina la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kashfa ya usambazwaji wa salfa feki.

Njau anasema kinachosababisha tatizo hilo ni kuwapo kwa wazabuni wengi wanaoingiza salfa nchini.

“Haiagizwi na mtu mmoja, zipo kampuni kama tano au sita ambazo zinaleta, wapo wanaoleta nzuri na wapo wanaoleta mbovu kama hii tuliyoikamata,” anasema.

Anadai ili kuepusha hilo serikali imeelekeza kampuni zinazoagiza salfa kutumia mfumo wa uagizaji wa pamoja (bulk procurement). 

Katika taarifa aliyotoa kwa vyombo vya habari Juni 7, mwaka huu, Njau anakiri kuwapo wafanyabiashara wanaoingiza nchini viuatilifu visivyo na ubora na kuvisambaza kwa wakulima wakati mamlaka ilikwisha kukataza.

Kwa muktadha huo, anasema TPHPA imeunda kamati mbili zinazofanya kazi kwa pamoja; moja ikisimamia ugawaji wa pembejeo kwa msimu wa 2022/23 na nyingine ikifuatilia mwenendo wa viuatilifu visivyo na ubora kwenye zao la korosho.

Juni 7, mwaka huu, akiwa ziarani Mtwara, Shaka alibaini kuwa Kampuni ya Makonde huwashawishi wananchi kususia pembejeo zinazosambazwa na serikali, ikiwahadaa kuwa ingewauzia pembejeo kwa bei nafuu.

Alisema pembejeo hizo ikiwamo salfa zimekwisha kupitwa na wakati na haina viwango na kuonya kutumiwa kwa jina la waziri mkuu katika biashara hiyo.

Shaka alishangazwa na jeuri ya mfanyabiashara huyo ambaye anadiriki kutaja jina la  waziri mkuu kwamba amempa uwakala wa kusambaza pembejeo feki ilhali waziri mkuu hana taarifa.

Katika hatua ya kukabiliana na vitendo hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, ameagiza kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Makonde.

Wakati akikamatwa, imebainika kuwa tayari salfa feki imesambazwa katika wilaya za Tandahimba na Newala ilikokamatwa mifuko 1,500; Tandahimba (mifuko 500) na Newala (1,000).

Siku chache baada ya JAMHURI kuripoti kuwapo sokoni kwa salfa feki mwezi uliopita, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Francis Alfred, alitoa taarifa kupinga takwimu zilizoandikwa na gazeti hili.

Katika taarifa yake alisema msimu wa mwaka 2021/22 salfa inayofaa ambayo imesambazwa kwa wakulima ni tani 13,000 tu.

Pia akakanusha kuhusika kwenye usambazaji wa salfa feki akidai kuwa alichokifanya ilikuwa ni kufuata maelekezo ya TPHPA, na kumuandikia barua mzabuni akimtaka kuiondoa salfa hiyo kwenye maghala ya bodi.

Hata hivyo, barua kwa mzabuni haikutamka kuwa salfa inayotakiwa kuondolewa kwenye maghala ni feki; bali ilimtaka kuiondoa kupisha uhifadhi wa korosho katika maghala hayo.

Akizungumza na JAMHURI wiki iliyopita, Alfred anasema: “Niliandika nikisisitiza utekelezaji wa maelekezo ya TPHPA kwamba aitoe kwenye maghala kuirudisha ilikotoka. Hakuna mahali mimi nilipingana na maekelezo ya TPHPA.” 

Alfred anakataa kuhusika katika usambazaji wa salfa feki maarufu kama ‘Salfa ya Makonde’, akidai kuwa TPHPA ndio wenye jukumu la kudhibiti isisambae baada ya kubaini haifai.

“Kumbuka tayari kuna taarifa nyingi zimetoka na kuna juhudi kubwa zimefanyika kudhibiti salfa iliyo chini ya kiwango isisambae.

“Tunashirikiana na mamlaka za mikoa na TPHPA. Usichukue taarifa yangu na kuilinganisha na taarifa za TPHPA kwa sababu ‘we don’t work in isolation, we collaborate’. Sisi sote ni taasisi za serikali,” anasema Alfred.  

Habari iliyochapishwa na JAMHURI Mei 10, mwaka huu ilieleza namna CBT ilivyoshiriki kusambaa kwa salfa feki, ikimtaja mkurugenzi kufanya uamuzi bila kushirikisha watu wengine ndani ya bodi kumrejeshea pembejeo hizo mzabuni.

Katika habari hiyo, taarifa zilionyesha kuwa salfa hiyo ilikuwa tayari imerudishwa kwa mzabuni na ilikuwa imeanza kufungashwa upya (repackaging) wilayani Masasi.

Taarifa za ndani ya bodi zilibainisha kuwa Mkoa wa Mtwara umeguka jalala la pembejeo na viuatilifu feki kutokana na masilahi binafsi ya wakubwa fulani.

Akizungumzia kuwapo kwa salfa isiyofaa, mkulima wa korosho kutoka wilayani Tunduru, Kapwepwe Halid, anasema tangu serikali iamue kutumia vyama vya wakulima kugawa pembejeo za kilimo ikiwamo viuatilifu, wajanja wachache wametumia mwanya huo kufanya udanganyifu.

Anasema kupitia vyama vya ushirika (AMCOS) vilivyoundwa na serikali kila kata ili viwagawie wakulima pembejeo, kumekuwa na ukiritimba mkubwa, akiitaja Wilaya ya Tunduru kuwa na uhaba mkubwa wa salfa.

“Mahitaji ni makubwa, lakini unakuta pembejeo zinazoletwa ni kidogo sana. Bila shaka wafanyabiashara wanatumia nafasi hiyo kupenyeza pembejeo feki,” anasema Halid.

Kutokana na kuporomoka kwa kilimo cha korosho wilayani humo, Halid anasema huenda hata wao wamekuwa wakitumia salfa isiyofaa kwa kipindi kirefu, kwani yapo mashamba ambayo wanashindwa kuvuna kutokana na maua ya korosho kupukutika baada ya mkorosho kuchanua.

 “Hakuna uwiano wa salfa inayotolewa na vyama vya msingi na mashamba ya wakulima, unakuta mtu anamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari 15, akienda kwenye vyama vya msingi kuomba salfa anapewa mfuko mmoja.

“Wapo wakulima hapa Tunduru waliomba salfa tangu mwaka jana, lakini hadi leo hawajapewa. Sasa wakisikia kuna mfanyabiashara ana salfa ya kutosha, hawawezi kusita kwenda kununua hata kama ni feki,” anasema.

Salfa katika zao la korosho hutumika kuongeza joto kwenye maua kuyalinda dhidi ya ukungu wa baridi unaosababisha yavamiwe na wadudu waharibifu.

Ua la mkorosho hutengeneza tegu, na tegu likikomaa hutengeneza bibo ambapo nalo likikomaa ndilo hutengeneza korosho. Salfa inayoagizwa na kutumika nchini ni ya maji na ya unga.

Kuna aina nne za salfa ya unga zinazojulikana kutokana na waagizaji wake; salfa ya Bajuta inayotoka Arusha, salfa ya Dangote, salfa ya Makonde na salfa ya India.

Mbali na salfa, kuna viuatilifu vingine kadhaa muhimu katika kilimo cha korosho kama dawa za kuboresha maua na mbolea aina ya Busta, kuimarisha maua ya mkorosho yasipukutike wakati wa upepo.

Pia kuna viuatilifu vinavyosaidia kuondoa kutu kwenye korosho na kuifanya iwe nyeupe na dawa aina ya ubwili unga inayosaidia kutokuwa na ungaunga unaotokana na ukungu.