LONDON

Na Ezekiel Kamwaga

Samuel Huntington, pengine mchambuzi mahiri zaidi wa siasa za Marekani katika karne iliyopita, alipata kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu mashuhuri cha Harvard nchini humo. 

Mmoja wa wanafunzi wake alikuwa Fareed Zakaria na anakumbuka somo moja kubwa ambalo aliwafundisha – kwamba kwenye uchambuzi wowote wa siasa, jambo muhimu zaidi kulifahamu ni kipi hasa ndicho kisababishi; yaani kwa lugha ya Kiingereza ‘Independent Variable’.

Kama haujajua kisababishi, ni shida kufanya uchambuzi sahihi. Ni kama msingi wa nyumba – kama ni mbovu, nyumba nzima inakuwa shakani. Nimekumbuka maneno haya ya Zakaria baada ya kusikiliza mazungumzo ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kwenye mjadala wa Clubhouse wa Mei 24, mwaka huu. 

Sikusikiliza mjadala siku hiyo lakini nilisikiliza Mei 30 kupitia akaunti ya YouTube ya Mohamed Ghassani.

Kwenye mjadala huo Lissu alizungumzia kile alichokiita ‘Kosa la Kimkakati’ – la aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na mgombea urais wa Zanzibar katika chaguzi mbalimbali kupitia chama hicho na kile cha CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, kwenye mazungumzo ya miafaka na maridhiano ya Zanzibar.

Lissu alikuwa na hoja mbili kubwa; mosi, kwamba Maalim Seif alifanya mazungumzo na viongozi wa Zanzibar ilhali tangu baada ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964, uamuzi mara nyingi wa visiwa hivyo hufanywa Dar es Salaam au Dodoma. Hapa, kwa kifupi, hoja ya Lissu ilikuwa kwamba Maalim Seif ilibidi afanye mazungumzo na viongozi wa Muungano, si wa Zanzibar.

Hoja ya pili ni kwamba ilibidi mazungumzo hayo yamhusishe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – iwe Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa au John Magufuli. 

Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa Lissu, Rais wa Tanzania ndiye Mkuu wa Nchi, Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Kama kitu mkikubaliana na Rais wa Tanzania, kwa kufuata hoja hii, mara nyingi hakuna wa kupinga. 

Nafikiri hoja hii msingi wake mkubwa ni mazungumzo yanayoendelea sasa kati ya Chadema na Rais Samia Suluhu Hassan.

Nadhani hivyo, kwa sababu Lissu alitumia nafasi hiyo kuponda mazungumzo yanayoendelea sasa kati ya Kituo cha Demokrasia (TCD) na Kamati Maalumu (Kikosi Kazi) iliyoundwa na Rais Samia kuangalia – pamoja na mambo mengine, masuala mtambuka kama sheria za uchaguzi na mustakabali wa kufanya siasa za ushindani nchini. 

Kwa maelezo yake, mazungumzo ya Chadema na Rais Samia yana uwezekano mkubwa wa kupata kinachotakiwa kuliko hayo ya TCD na Kamati ya Mukandala.

Makala hii inasaili maelezo hayo ya Lissu kwa kufanya mambo mawili; mosi, kutazama kama mwanasheria huyo na mbunge wa zamani wa Singida Mashariki alipatia kwenye kisababishi na kuhusu ukuu na mamlaka ya Rais wa Tanzania kwenye kufanya uamuzi wa siasa za ndani ya nchi.

Kuhusu kisababishi

Katika siasa za Tanzania, kisababishi na mhusika mkuu ni Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kuondoa TANU na ASP katika miaka ya mwanzoni ya Uhuru, hiki ndicho chama pekee kilichokaa madarakani nchini. 

Kwa sababu ya namna kilivyosukwa, hasa wakati wa mfumo wa chama kimoja, ushawishi wake ni mkubwa karibu katika nyanja zote za maisha ya Watanzania.

Jambo lolote linalogusa madaraka na ushawishi wa watawala, ni lazima likubaliwe na CCM ili lifanikiwe. Kama ndani ya CCM kuna jambo halikubaliki kwa makundi yaliyomo, ni rahisi kwa suala kupigwa dafrao. 

Kwa hiyo, kwenye muktadha wa Tanzania – na kwa muktadha wa mazungumzo ya Lissu – tatizo si viongozi wa Tanzania; wa Dodoma au Dar es Salaam, tatizo ni CCM.

Hoja yangu ni kwamba miafaka ya Maalim Seif haijapata matunda mpaka leo kwa sababu CCM – kwa ujumla wake, haikuitaka miafaka hiyo.

Na wala tatizo halikuwa Dar es Salaam au Dodoma pekee. Tatizo lenyewe liko Zanzibar pia. Katika andiko la kitaaluma la mwaka 2018 lililoandikwa na Dk. Nicodemus Minde na wenzake lililoitwa ‘The Politics of Continuity and Collusion in Zanzibar’, majimbo 10 yanayofahamika kama ngome za CCM visiwani humo; Chaani, Donge, Kitope, Chwaka, Uzini, Makunduchi, Muyuni, Dole, Amani na Kwahani, yalipiga kura ya ‘HAPANA’ kwa maridhiano yaliyosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Andishi hilo limeweka bayana kwamba kufanikiwa kwa maridhiano kwenye kura ya maoni kulisababishwa zaidi na kuungwa mkono kwake na wafuasi wa CUF kuliko CCM. Kwa sababu hiyo, kama miafaka na maridhiano havikufanikiwa, tatizo si Dodoma wala Dar es Salaam. Tatizo ni CCM. Suluhisho ni CCM.

Kufanikiwa au kutofanikiwa kwa miafaka iliyopatikana na itakayopatikana mbele ya safari, kutategemea namna CCM itakavyopokea jambo hilo.

Kimsingi, andishi hilo la akina Minde linaweka bayana kwamba hoja ya maridhiano iliwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na Mwakilishi wa CUF, Abubakary Khamis Bakari, kwa sababu Karume hakuwa ameihusisha CCM na mtu wa chama chake asingeweza kuwasilisha hoja ya namna hiyo kwa jambo ambalo halikuwa limekubaliwa rasmi na chama tawala.

Nakubaliana na Lissu – nikiondoa neno lisilo na uzito la Dar es Salaam au Dodoma na kuweka CCM, kwamba chama tawala kimekuwa na ushawishi mkubwa katika mambo yanayofanyika Zanzibar. Hata hivyo, si mara zote. 

Kwa mfano, juhudi za CCM Bara kutaka Dk. Salim Ahmed Salim awe Rais wa Tanzania baada ya Mwalimu Nyerere zilipigwa dafrao na Wazanzibari waliomtaka Ali Hassan Mwinyi. Kwa hiyo ni Wazanzibari – wakisaidiwa na wenzao wa Bara waliowaunga mkono, walioamua nani awe Rais wa Tanzania.

Hata maridhiano ya mwaka 2009 yalisababishwa na kufanikishwa na uhusiano binafsi baina ya Rais Amani Karume na Maalim Seif ambao wote ni Wazanzibari. Kama Wazanzibari wakiungana na kuamua jambo lao kwa pamoja – kuna ushahidi kuwa zipo nyakati CCM Bara hukubaliana nao.

Kuhusu mamlaka ya Rais wa Tanzania

Nakubaliana na Lissu kwamba Rais wa Tanzania ana mamlaka makubwa. Hata hivyo, mahali ninapotofautiana naye ni kwenye kuamini kwamba Rais akiamua jambo, hasa la kisiasa, maana yake ni kwamba litafanikiwa. Ukweli wa Tanzania katika kipindi cha miongo minne iliyopita uko tofauti. Nitatoa mifano michache.

Nyerere, akiwa Rais wa Tanzania, alimtaka Salim awe mbadala wake lakini akashindwa. Jakaya Kikwete, akiwa Rais wa Tanzania, alitaka Tanzania iwe na Katiba Mpya wakati wa utawala wake lakini akashindwa. 

Kimsingi, Kikwete alilifanya jambo la mwafaka wa Zanzibar kama ajenda yake binafsi kiasi kwamba alilizungumza katika hotuba yake ya kwanza bungeni Januari mwaka 2006.

Na hii inaondoa dhana kwamba kwa kuzungumza na Samia, Chadema inaweza kupata inachotaka kwa sababu ni Rais. Pengine tunasahau mapema lakini Kikwete alitaka maridhiano Zanzibar kiasi kwamba kuna wakati mazungumzo ya wawakilishi wa CUF na CCM yalikuwa yakifanyikia Bagamoyo – mahali pa karibu na moyo wa Jakaya, ili kuona kwamba mambo yanakwenda vizuri. 

Hata hivyo, kama tulivyoona kwa kura ya maoni Zanzibar, inaonekana CCM yenyewe haikutaka mwafaka au maridhiano.

Ni sawa na suala la Katiba. Serikali ya Kikwete iliunda Tume ya Jaji Warioba na kuingia gharama kubwa kuhakikisha Tanzania inapata Katiba Mpya. Hata hivyo, jambo hilo inaonekana halikukubaliwa na CCM kama chama na matokeo yake yakawa mkwamo.

Hoja yangu hapa ni kwamba kuzungumza na Rais pekee si kete tosha. Rais anaweza kuwa na nia njema na bado akashindwa kutekeleza yanayotakiwa kwa sababu chama chake – CCM, hakitaki kwa sababu yoyote ile. Hata mazungumzo ya Kikosi Kazi kinachoongozwa na Mukandala kupitia TCD yana baraka za Rais lakini jambo muhimu zaidi ni kama yatakayopendekezwa yatakubaliwa na CCM.

Kosa la Lissu, kosa la Maalim

Kuna andishi jingine muhimu la kitaaluma linalofaa kuingizwa katika mada hii. Ni la Nic Cheeseman la mwaka 2010 liitwalo The Internal Dynamics of Power Sharing in Africa. Cheeseman amebainisha makundi mawili tofauti ya vinavyosababisha vyama kuingia kwenye kugawana madaraka – kundi la waliogombana vita ya wenyewe kwa wenyewe na lile la maeneo ambako ni vigumu mmoja kushinda kwa kura nyingi kwa sababu ya migawanyiko ya kihistoria.

Kwa sababu Zanzibar haijatoka moja kwa moja katika vita ya wenyewe kwa wenyewe licha ya rabsha za Vita ya Juni 1961 na Mapinduzi ya 1964, inaingia zaidi katika kundi la pili la migawanyiko ya kisiasa. 

Katika hilo andishi lake, Cheeseman anasema kuna vikwazo viwili vikubwa katika kuamua aina ya ushirikiano; kwanza, ni namna gani wahusika wanaaminiana wenyewe kwa wenyewe na kama mahasimu wana nguvu zinazotoshana au zisizotoshana za kufanyiana unyama.

Namna pekee ya kujenga kufahamiana na kuaminiana ni kuwa na kitu kama SUK. Kwa sababu pasipo kufanya kazi pamoja na kuona kuwa inawezekana, itakuwa vigumu kujenga kuaminiana. Kwa sababu hiyo, naamini Maalim Seif alikuwa sahihi kukubali kuingia kwenye mwafaka na maridhiano kwa vile ndiyo namna bora zaidi ya kujenga kuaminiana ambako ni muhimu kwenye kusonga mbele.

Kosa pekee ambalo alilifanya Maalim Seif lilikuwa ni kutoihusisha CCM – kwa mapana na marefu yake, kwenye kufanikisha jambo lake hilo. Kwa sababu hiyo, ingawa alikaa na kushikana mikono na Karume, SUK iliingia kwenye shida miaka michache mbele kwa sababu CCM kama chama hakikuwa sehemu ya makubaliano.

Lakini, kama ningekuwa mwanasiasa na kuambiwa nini kianze – kati ya kuimarisha uhusiano na CCM na kuingia ndani ya SUK na kuimarisha kwa kuanzia humo, ningechagua la pili. Hii ni kwa sababu, nikimnukuu Kwame Nkrumah: “Jambo la kwanza ni kuingia madarakani, halafu mengine yatafuata.” Lakini kuingia madarakani katika mazingira tepetevu ya SUK 2020, ilikuwa ni kamari ambayo ingeweza kulipa mwaka 2015 – kama isingekuwa kwa mambo ya Jecha na wahafidhina wa CCM.

Kosa la Lissu ni kuamini kwamba Wazanzibari wenyewe hawana uamuzi katika hatima yao. Kwenye hili la maridhiano, ni kama tu hawajaamua. Tatizo – kama utafiti wa akina Minde ulivyoonyesha, Wazanzibari wenyewe bado hawako pamoja kwenye jambo la maridhiano, na CCM yenyewe bado ina kundi la watu wasioamini katika mwafaka au wasioamini katika utawala ambao wenyewe watakuwa nje ya madaraka.

Picha isiyozungumzwa

Nilishangaa kwamba hakukuwa na mjadala mpana kuhusu ni kwa nini kwenye mkutano wa mwisho kati ya viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na Rais Samia ulimhusisha pia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana na viongozi wengine wa chama tawala. Mikutano ya mwisho ilimhusu Mbowe na Samia peke yao.

Picha niliyopata ni kwamba Samia alikuwa anakihusisha chama chake katika mikutano yake hiyo. Watu wengi walikuwa wanazungumza kana kwamba bado ni mkutano kati ya Rais na Chadema. Sina taarifa za uhakika kama maana ya kuwahusisha vigogo wale wa CCM ni kwamba kuna baraka za chama au makubaliano yatakayofikiwa yatakubaliwa na wenye chama chao.

Sijui kilichozungumzwa lakini mimi ni mmoja wa wanaoamini kwamba kwa mwafaka na maridhiano kamili ya kisiasa kufikiwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake, ni lazima kisababishi kikuu cha matukio ya kisiasa na kijamii hapa nchini kihusishwe katika kukubali kwa ujumla wake.

Mwandishi wa makala hii ambayo kwa mara ya kwanza imechapishwa katika tovuti ya Udadisi ni mwanafunzi anayesomea masuala ya Siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS). Amewahi kuwa mhariri wa magazeti kadhaa ya Tanzania. Anapatikana kwa email: [email protected]

By Jamhuri