Sekretarieti yavujisha mitihani ajira za TRA

DAR ES SALAAM

NA DENNIS LUAMBANO

Mitihani na majibu ya usaili wa walioomba ajira zilizotangazwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS) kwa ajili ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) vimevuja, JAMHURI linathibitisha.

PSRS walitangaza ajira hizo Juni Mosi, mwaka huu kupitia tangazo lenye kumbukumbu Na. EA.7/96/01/L/126 ambalo linapatikana katika tovuti yake yawww.ajira.go.tz. Ajira hizo ni Tax Management Officer II (nafasi 22), Customs Officer II (nafasi 6), Tax Management Assistant II (nafasi 8), Customs Assistant II (nafasi 7), Personal Secretary II (nafasi 3) na Tax Investigation Officer II (nafasi 2).

Nafasi hizo za ajira ni 48. Hata hivyo, nafasi mbili za Tax Investigation Officer II zilifutwa na TRA kupitia tangazo la Juni 2, mwaka huu na kuongezwa katika nafasi ya Tax Management Officer II, hivyo kundi hili zikaongezeka kutoka 22 na kuwa 24.

Tangazo jingine la Julai 28, mwaka huu linalopatikana katika tovuti ya PSRS limeorodhesha watahiniwa 8,850 walioitwa katika usaili wa mchujo uliopangwa kuanza Agosti 7 hadi 26, mwaka huu jijini Dodoma, kuomba kupata bahati ya kuajiriwa katika moja kati ya hizo nafasi 48.

Baadhi ya watahiniwa waliofanya usaili katika maeneo tofauti jijini Dodoma wamelalamika kuwa mitihani na majibu vilianza kusambaa mitaani siku kadhaa kabla ya usaili. Maswali na majibu hayo vilionekana katika mitandao ya kijamii.

Mmoja wa watahiniwa aliandika katika mtandao wa kijamii: “Mimi ni kijana kutoka Mkoa wa Kigoma jana (Agosti 7, mwaka huu) nimefanya written interview ya Tax Officer inayosimamiwa na Utumishi. Baada ya kufanya mtihani tukasikia imevuja na leo kuna mdau mmoja amenitumia huo mtihani.”

Kusambaa kwa taarifa hizo kumetokana na walioifanya mitihani hiyo kudai kwamba wenzao kadhaa walikuwa na maswali na majibu kabla ya usaili.

Wakati taarifa hizo zikiendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii, PSRS ilitoa tangazo la kuahirisha usaili mwingine wa TRA uliokuwa umepangwa kufanyika kati ya Agosti 23 na 26, mwaka huu.

Tangazo hilo lililotolewa Agosti 9, mwaka huu na Kitengo cha Mawasiliano serikalini kupitia tovuti ya PSRS linasema: “Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawajulisha waombaji kazi waliofanya usaili wa mchujo Agosti 7, 2021 kwa nafasi za Tax Management Officer II, Customs Officer II, Tax Management Assistant II na Customs Assistant II kuwa usaili uliopangwa kufanyika Agosti 25 hadi 26, 2021 umeahirishwa. Pia usaili wa kada ya Personal Secretary II uliopangwa kufanyika Agosti 23, 2021 nao umeahirishwa. Taarifa zaidi zitatolewa kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira.”

JAMHURI limemtafuta Katibu wa PSRS, Xavier Daudi, bila mafanikio baada ya kujibiwa ofisini kwake kuwa amesafiri, na nafasi yake inakaimiwa na Samwel Tanguye.

Tanguye amezungumza na JAMHURI na kusema hawajapokea malalamiko ya kuvuja kwa mitihani na majibu yake. Amesema pindi wakiyapokea watafanya uchunguzi haraka.

“Hizo taarifa za kuvuja kwa mitihani ziko wapi? Sisi hatujazipata, kwa maana kama ni kero hatujazipata. Sasa labda la kufanya ni lazima tuwe na uvumilivu kwa sababu usahihishaji unaendelea halafu hao vijana wenye hofu wataona matokeo,” anasema Tanguye na kuongeza: “Hao vijana watulie, wasubiri matokeo kwa sababu si kazi ya kwanza tunafanya na TRA, hii ni kazi kama ya tatu au ya nne tunaendelea nayo, kwa hiyo watulie wasubiri matokeo na wakiona matokeo yale basi wataweza kusema kuna chochote kimefanyika kwamba labda kuna mtu alimbeba nani.

“Pili, tunapotoka katika usaili wa mchujo tukawapata wale wachache ambao si wachache, bali ni wengi nao, tunawajumuisha wataalamu mbalimbali, kwa hiyo kama kuna malalamiko yoyote ambayo yapo au kama kuna mwananchi amekujulisha ninadhani ingekuwa ni vema wakatuletea sisi hizo taarifa za malalamiko ili tuanze uchunguzi wa haraka, kwa maana ya kuviandikia vyombo vya uchunguzi na kama kuna lolote lile basi tuanze kulifanyia kazi.

“Lakini hadi tunapozungumza sisi tunaendelea na shughuli zetu na hatujapata malalamiko kutoka kwa waombaji kazi labda kama wao wameyafikisha kwenu, katika mitandao ya kijamii ama wapi.”

Amewataka waliofanya usaili wawe wavumilivu kwa maelezo kwamba watatoa matokeo na kama kutakuwa na ubadhirifu au uvujishaji wa mitihani taarifa zitatolewa kwa umma.

“Vijana wawe wavumilivu, kama kutakuwa na kesi hizo ulizotuambia umesikia au kama kutakuwa na kesi watu kufananisha majibu yao tutaujulisha umma, tumekuwa tukifanya kazi hizi kwa weledi mkubwa kwa niaba ya waajiri wote nchini na hamjawahi kusikia kelele za namna hii. Kama vijana waliofanya usaili walifanya vizuri wataona matokeo yao na kama hawakufanya vizuri wataona matokeo yao, na kama kulikuwa na mambo ya ubadhirifu au udanganyifu pia wataonekana, hayo yanatokea kwa kuwa umma una mawazo kwamba kuna upendeleo na lazima kuwe na vyombo vya kueleza kama ninyi ili wajue ukweli,” anasema.

Kuhusu tangazo la kuahirisha usaili wa Agosti 25 na 26, mwaka huu, Tanguye, anasema kumetokana na ratiba za ndani kuingiliana, na si kuvuja kwa mitihani.

“Usaili uliofanyika Agosti 7, mwaka huu kwa niaba ya TRA ulikuwa ni wa mchujo na kwa sasa taratibu za ndani zinaendelea. Waombaji wanapokuwa wengi huwa tunaandaa usaili wa aina tatu hadi tano. Usaili wa kwanza kabisa huwa ni wa mchujo. Tunawachuja ili kupunguza na kupata idadi, halafu baada ya usaili huo kinachofuata kutegemea na nature ya usaili wenyewe huwa ni usaili wa mahojiano na unakuwapo kama hakuna usaili wa vitendo ambao tulipanga ufanyike kati ya Agosti 25 na 26, mwaka huu.

“Kwa hiyo baada ya usaili wa mchujo kuna kazi ya kuchambua, kusahihisha na kupanga na vikao vingine vinakaa na Agosti 25 na 26, mwaka huu ndipo tulipanga ufanyike usaili wa mahojiano na huo ndio tumeahirisha tarehe yake kwa sababu kuna shughuli nyingine zinaendelea ambazo hazihusiani na usaili na hatujafuta usaili. Tuliona kufikia tarehe hiyo ya 25 na 26 tutakuwa hatujakamilisha ndipo tukautangazia umma na wale vijana kwamba tutawajulisha lini ule usaili wa ana kwa ana utafanyika na hilo ndilo tangazo lililotolewa,” anasema Tanguye.

Katika hatua nyingine, Tanguye amekanusha taarifa kwamba wamepoka majukumu ya kuajiri wafanyakazi wa TRA.

Anasema hata katika mchakato huo wanashirikiana na wataalamu kutoka ndani ya TRA.

“Pitia sheria (namba 8 ya mwaka 2002 na marekebisho yake namba 18 ya mwaka 2007, kifungu cha 29 (1)) iliyoanzisha PSRS halafu utaona tuna wajibu wa kusimamia usaili wa taasisi zote za umma isipokuwa vyombo vya ulinzi na usalama, tunaposema taasisi za umma je, ni zipi hizo?

“Taasisi hizo ni wizara, mikoa, halmashauri, taasisi zinazojitegemea, wakala na mamlaka mbalimbali, na hiyo ni sheria ilitamka namna hiyo. Pili, tunapokea vibali kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa niaba ya serikali kwa ajili ya taasisi zote zikitutaka, na tunaendesha usaili kwa kushirikiana na waajiri husika.

“Hata sifa za hao walioomba nafasi za ajira zimetolewa na TRA wenyewe, sisi kazi yetu ni kuratibu na kuusimamia ule mchakato wa usaili hadi tunaukamilisha na ndipo linatolewa tangazo waombaji waweze kuomba na tunawachuja na tunatoa mrejesho kwa kila aliyeomba kwa nini hajaitwa,” anasema.

Kuhusu baadhi ya watu wanaoajiriwa kufanya kazi TRA bila kuwa na ujuzi wa masuala ya kodi kukosa uwezo katika maeneo yao ya kazi au kiwango cha utendaji wao kuwa cha chini, Tanguye anakanusha tuhuma hizo.

“Tumeshafanya usaili siku za nyuma na watu wako TRA wanafanya kazi, kuna makundi kama mawili au matatu ya mwisho tumewaajiri sisi na wako TRA wanafanya kazi. Sisi tukiona mapato ya TRA yameongezeka, maana yake tumewapelekea wataalamu na tafsiri yake ni kwamba tumefanikiwa, fuatilia tunaowaajiri – utendaji wao wa kazi ukoje?

“Kwa miaka hii mitatu au minne tumeona mapato ya TRA yakiongezeka na tunaamini moja ya vitu tulivyofanya ni kupeleka vijana wanaosimamia maadili ya kazi na taaluma zao kwa ufanisi, kwa hiyo tumefanikiwa katika hilo,” anasema.

Tangu kuanzishwa kwa TRA mwaka 1996 kwa sheria iliyotungwa mwaka 1995, watumishi wote wa TRA wamekuwa wakiajiriwa na TRA bila kupitia Utumishi wa Umma. Kifungu cha 13 (f) cha Sheria ya TRA kama ilivyorekebishwa mwaka 2019 kinatoa madaraka kwa Bodi ya TRA kwa ruhusa ya Waziri wa Fedha kupanga mishahara, masurufu na marupurupu yatokanayo na kazi kupangwa na Bodi kwa watumishi wote, kuanzia kwa Kamishna Mkuu hadi mfanyakazi wa kawaida wa TRA.

“Hii haikufanywa kimakosa. Mzee [Benjamin] Mkapa aliamua kwa makusudi wafanyakazi wa TRA waajiriwe na Mamlaka yenyewe. Hata mishahara aliamua ipangwe na Mamlaka yenyewe. Alisema huku kuna mishahara tofauti na sekta nyingine kwa nia ya kuwafanya hawa wafanyakazi waridhike na wanachopata, hivyo wakusanye kodi kwa uadilifu.

“Sasa kuruhusu hawa wakaenda kusailiwa Utumishi wa Umma unafungua milango ya rushwa. Huko wataingizwa watoto wa shangazi, mjomba, ndugu, jamaa na marafiki bila kujali iwapo wana sifa stahiki au la. Hii ni hatari, haikubaliki. Ni lazima tuheshimu nia na misingi ya kuanzishwa kwa TRA. Sasa unasailije watu usiokuwa na uwezo wa kuwapangia mshahara?” amehoji mmoja wa wafanyakazi wa TRA ya mwanzo kabisa ya mwaka 1996.

Amewataka Utumishi wa Umma kuheshimu nia mahususi ya kuwekwa kwa utaratibu huu wa TRA kuajiri wafanyakazi wake na kuwalipa bila kutumia Utumishi wa Umma, vinginevyo watavuruga mfumo wa ukusanyaji mapato kwa kuingiza kazini watu wasiokuwa na uwezo.