Na Deodatus Balile

Mpendwa msomaji salamu. Sitanii, tangu nimepata pigo la kuondokewa na Mkurugenzi mwenzetu, Mkinga Mkinga, Juni 24, 2021, sijaandika katika safu hii. 

Itanichukua muda kuamini kuwa kweli Mkinga amefariki dunia, ila nalazimika kuukubali ukweli kwamba sisi tu waja wake na kwake tutarejea. Mwenzetu mbele, sisi tu nyuma yake. Raha ya Milele Umpe Ee Bwana, na Mwanga wa Milele Umwangazie, Apumzike kwa Amani… Amina.

Sitanii, kwa vyovyote iwavyo maisha lazima yaendelee. Nikiwa katika kipindi hiki cha majonzi yametokea masuala mengi. Mimi si mwanasiasa, lakini si haba. Uzoefu wa siasa za nchi hii ninao kidogo. Nakumbuka ingawa nilikuwa bado madarasa ya chini, mwaka 1980 nilishiriki angalau kuimba wimbo wa “Enfuka neruga omunju kugya kulima… (Jembe linatoka ndani ya nyumba kwenda kulima).” Hizi zilikuwa kampeni za ubunge kwa Jimbo la Bukoba Mjini kati ya Mwalimu Gabriel Rugumila na Mzee Samweli Ntambala Luhangisa.

Tangu wakati huo Mungu amenijalia kwamba nimezishuhudia kampeni za mwaka 1980, 1985, 1990, 1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020. Za mwaka 1975 nilikuwapo ila sina kumbukumbu nazo vizuri. Kushuhudia siasa kwa muda wa miaka 40 ukiwa unajitambua si haba. Nimeshuhudia kuibuka na kufa kwa vyama vya siasa. Angalau kwa mapenzi ya Mungu nilizaliwa kabla chama cha ukombozi TANU hakijafikiria kuungana na ASP. Baadaye mwaka 1977 ilizaliwa CCM.

Sitanii, sehemu ya kichwa cha makala hii inamtaja Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Binafsi sitaki kuingia katika undani wa kesi inayomkabili Kisutu, inayomfanya aendelee kuishi gerezani Segerea. Jambo moja ninasema, uzoefu wa siasa nilioupata ndani ya nusu karne ya kuzaliwa na kuishi kwangu hapa duniani, unanionyesha kuwa suluhisho la matatizo ya kisiasa haliwezi kupata ufumbuzi kupitia mahakamani.

Miaka sita iliyopita, tulishuhudia matumizi makubwa ya mahakama sawa na ilivyokuwa kati ya mwaka 1928 hadi Desemba 9, 1961 tulipopata Uhuru wa Tanganyika. Mkoloni kila neno lililotolewa na Mwafirika, lilitosha kumfungulia kesi mahakamani. Hata Mwalimu Julius Nyerere alionja adha hiyo mwaka 1958. Binafsi naona hii hamu ya polisi wetu kupeleka mahakamani kila mtu haina afya mbele ya safari.

Nchi ilikuwa imepata utulivu mkubwa wa kisiasa hadi Julai mwaka huu walipoamua kuanzisha kamata kamata. Jumuiya ya kimataifa imeanza kutushangaa tena. Nafahamu huenda kuna wanaonufaika na ukamataji huu wa viongozi wa kisiasa, lakini ninasema hawa bila kujua wanafanya kazi ya kukuza upinzani na kuhatarisha nafasi ya chama tawala kwa kujenga chuki machoni pa wananchi. Hili niishie hapo, ila niseme si kila kosa la kisiasa lazima lipelekwe mahakamani. Ipo siku wakamataji mtanielewa ninasema nini.

Sitanii, kwa kutoandika siku nyingi mambo yanakuwa mengi mezani. Lipo hili la chanjo ya corona. Najua wengi wametoa maelezo ya kina juu ya chanjo hii. Nikiri kwamba mimi na wahariri kadhaa tumechanja chanjo ya corona. Naona kuna kundi la watu linatumia nguvu kubwa kushawishi watu wasichanje. Jambo moja ninaomba kusema. Uhai wa mtu ni jukumu la mtu binafsi. Kila unapopata hamu ya kumshauri mtu, hakikisha una uelewa wa kutosha juu ya unachomshauri.

Wapo waliosema tukichanja tutakuwa mazombi. Wapo waliosema tutakufa ndani ya siku tatu. Wengine baada ya kuona hatufi sasa wamesogeza mbele kuwa tutakufa baada ya miaka miwili. Kwa wenye umri uliopevuka kumbukeni hadithi ya mwisho wa dunia. Tena kumbukeni ile adha ya Y2K mwaka 2000. Wakati huo nilikuwa na mtoto mmoja na nikawa nimejazwa hofu.

Nikajiuliza nikifa mwanangu atabaki au naye atakufa pia. Saa sita usiku ilifika, na leo miaka 21 baadaye, sote tuko hai na nimepata watoto wengine. Ndugu zangu tusidanganyane, angalieni viwanja vya mpira Ulaya vilivyojifungua. Ukipata fursa kachanje. Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.

Sitanii, nafasi inazidi kupelea. Kuna hili la hujuma ndani ya CCM. Tumeziona kejeli na kauli dhidi ya chanjo zinazotolewa na viongozi wenye dhamana ndani ya CCM. Dhana ya uwajibikaji wa pamoja nadhani imeanza kupotea. Nadhani mifumo ya kuwajibishana ndani ya vyama vya siasa, wapo wanaodhani haiwahusu.

Habari yetu kubwa inazungumzia mtandao unaoutafuta urais mwaka 2025. Mimi ninasema nchi yetu ina mambo mengi ya kufanya. CCM na vyama vya upinzani vifahamu kuwa nchi ina hamu ya maendeleo. Uzoefu unanionyesha kuwa tusipoangalia tutageuka taifa la uchaguzi. Kwamba ukiisha uchaguzi wa 2020, tunaanza kuzungumza 2025 kwa miaka mitano yote. Tukimaliza 2025 tunaanza kuzungumza 2030. Hivi tutajenga lini barabara, shule, vituo vya afya, maji, umeme, viwanja vya ndege na mengine mengi?

Ni haki ya kila mwanachama kufikiria kugombea nafasi fulani, lakini haki hii isitumiwe kuhujumu viongozi walioko madarakani. Ajenda za mikutano ya sasa hazipaswi kuwa nani hafai kuongoza kata, jimbo au nchi, bali mikutano ya hadhara inapaswa kuwa ya kuelezana nani aliahidi nini na matarajio ya wananchi katika kipindi cha uongozi wa mhusika. Bila kwenda mkondo huo, tukaanza vita ya kuchimbiana mashimo, nchi yetu itaishia kuwa taifa la uchaguzi miaka yote na maendeleo tutaishia kuyasikia. Mungu ibariki Tanzania.

Please follow and like us:
Pin Share