Waziri Kalemani atumia kivuli cha ‘maagizo kutoka juu’

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, ametajwa kutumia lugha ya kwamba kuna “maagizo kutoka juu” mara nyingi anapowapa maelekezo watendaji wa wizara yake kuhakikisha mambo yanapitishwa haraka, JAMHURI limeambiwa.

JAMHURI limeelezwa kuwa kama si Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Injinia Leonard Masanja, kukataa “kutii maagizo kutoka juu” Kanuni mpya za uagizaji mafuta kwa kuwapa wazawa zabuni zingepitishwa bila kupitia kwenye Baraza la Mawaziri.

“Nilishangaa kwa kweli. Waziri alikuja ofisini akawa anamwagiza katibu mkuu akamilishe Kanuni azisaini bila hata kupitia kwenye Baraza la Mawaziri. Akamwambia Kanuni hizo zinatungwa na waziri, hivyo zisainiwe kwani kama ni kuulizwa yeye ndiye ataulizwa,” kimesema chanzo chetu na kuongeza: “Katibu Mkuu alimwambia waziri, ‘Mheshimiwa, tukizipitisha hizi Kanuni kama unavyotaka tutaishia mahakamani. Tutafungwa, nami siko tayari kwa hili’,” kimesema chanzo chetu kingine.

Kwa miezi ya Julai na Agosti, 2021 bei za mafuta nchini zimepanda kwa kiwango cha kutisha kutokana na baadhi ya vigogo kupenyeza masilahi binafsi katika mfumo wa uagizaji mafuta nchini ambapo gharama za kusafirisha mafuta zimeongezeka mara dufu.

Inatajwa kuwa kutokana na shinikizo la waziri, katibu mkuu aliandika barua kwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuwataka watenge asilimia 20 ya zabuni za mwezi Julai na Agosti kwa ajili ya kampuni za wazawa pekee, hali iliyoleta zahama.

“Uamuzi huu ambao unaelezwa kuwa unanufaisha mtandao mpana wa vigogo serikalini, umeleta sintofahamu. Bei za kusafirisha mafuta ya dizeli zimepanda kutoka wastani wa dola za Marekani 24 (Sh 55,200) kwa tani hadi dola za Marekani 47 (108,100) kwa tani katika Bandari ya Dar es Salaam. 

Bandari ya Tanga usafirishaji umepanda kutoka dola za Marekani 48 (Sh 110,400) hadi dola za Marekani 72 (Sh 165,600) kwa mwezi Agosti na inaendelea kupanda. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza bei za mafuta nchini kwa mtumiaji wa kawaida,” kimesema chanzo chetu kutoka serikalini.

Ongezeko hilo linamaanisha kuwa kwa mafuta ya dizeli yanayoshushwa kwenye boya namba 1,2 na 3 kwa mwezi Agosti, 2021, ambayo ni jumla ya tani 268,314, uamuzi huu umeongeza gharama ya kuingiza dizeli nchini kwa wastani wa Sh 13,415,700,000. 

“Hizi fedha zinakamuliwa kwa Watanzania kwenda kuwezesha ‘wazawa’, yaani kampuni zilizosajiliwa Tanzania,” kimesema chanzo chetu. Hata kwenye petroli na mafuta ya taa nako kumetokea madhara ya bei kwa uamuzi huu.

Mwezi Julai, bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepanda kwa TZS 156/lita, 142/lita na 164/lita, mtawalia.  Mwezi Agosti, 2021 bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa TZS 21/lita, TZS 36/lita na TZS 55/lita, mtawalia. 

Sehemu ya ongezeko hili inatajwa kuwa imetokana na utaratibu mpya wa kutumia waagizaji mafuta wa ndani ambao wanasafirisha mafuta kwa bei juu kuliko kampuni za kimataifa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandishi Leonard R. Masanja, amezungumza na JAMHURI na amekiri kuandika barua ya kwenda kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon, yenye Kumb. Na. CAD.290/308/01 ya Juni 11, 2021 inayowaelekeza PBPA kutenga asilimia 20 ya biashara ya mafuta yote nchini kwa ajili ya kuagizwa na wazawa.

“Nakiri hii barua niliandika mimi. Shinikizo lilikuwa kubwa kuwa tupitishe Kanuni utaratibu huu uanze. Mimi nikajiuliza hivi ikitokea utaratibu ukawa haujakwenda vizuri itakuwaje? Mchakato wa kufuta Kanuni ni mrefu, si nitakuwa nimeipotosha serikali? Kwa kweli kwa masilahi mapana ya nchi na kwa kukataa shinikizo lililokuwa mbele yangu, nikaamua nifanye majaribio. Unaweza ukasema kwa nia njema nilijilipua nipate msingi wa kuishauri serikali.

“Niliiandika hiyo barua kutaka asilimia 20 ya zabuni itengwe kusaidia kuzijengea uwezo kampuni za ndani, lakini kilichotokea umekiona. Bei zimeongezeka, kilio kimekuwa kila kona. Sasa najiuliza, kama ningekubali kupitisha zile Kanuni ikawa nimeishauri serikali kuwa wazo hili linafaa tuwape wazawa nafasi, ingetokea hivi ningesema nini?” Mhandisi Masanja ameliambia JAMHURI.

Masanja hakutaka kwenda mbali zaidi, ila amesema anaishi maisha magumu kiasi kwamba kwa sasa kutokana na mashinikizo anatumia vidonge vya pressure (shinikizo la damu). Wiki iliyopita JAMHURI lilimkariri Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, akisema uamuzi wa kuzipendelea kampuni za ndani umefanywa kwa nia njema kuwezesha kampuni za wazawa kushiriki biashara ya kuagiza mafuta nchini. Hata hivyo, alikiri kuwa uamuzi huu umepandisha bei na “Serikali imeunda timu na inayapitia yote hayo. Timu ipo inafanya kazi na itakuja na majibu ya maswali yote hayo unayouliza.”

Chanzo kingine kililiambia JAMHURI kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza bei hizo zishushwe. “Baada ya agizo la Rais Samia, utaratibu huu umesitishwa kwa mwezi Septemba, 2021 na kuendelea. PBPA wamerejea katika utaratibu wa zamani. Cha ajabu, kwa meli itakayoleta mafuta wiki ya kwanza ya Septemba, kila tani moja itasafirishwa kwa dola 6 (Sh 13,800), badala ya dola 47 (Sh 108,100) za mwezi Agosti, 2021 kwa dizeli inayoletwa nchini. Sasa tunajiuliza, kwa nini Julai na Agosti tulitwishwa mzigo wote huu? Kama wanataka kusaidia wazawa si wawaondolee hizo kodi wanazosema wanalipa?” kimehoji chanzo chetu kingine.

Pia, JAMHURI limeambiwa kuwa Waziri Kalemani awali alikuwa amezuia nguzo kutoka Afrika Kusini zilizoletwa na kampuni ya kutoka China zikakaa bandarini kwa muda mrefu akisema zitumike nguzo za ndani na ni “maagizo kutoka juu” ila wizara ikaamua kumkaidi ikaziruhusu ili kunusuru hali.

Eneo jingine inasemekana Kalemani amekataa ushauri wa EWURA juu ya viwango cha kuunganisha umeme nchini ambavyo kila mteja alipaswa kulipa angalau Sh 164,000, yeye akatangaza nchi nzima itaunganishwa umeme kwa Sh 27,000 kasoro katikati ya Jiji la Dar es Salaam. 

“TANESCO inahitaji Sh bilioni 84 kufungia umeme wateja waliopo, bila wateja wapya. Hakuna vifaa, hakuna fedha, yeye akaona afanye siasa akashusha hadi Sh 27,000 kwa sasa ni zahama,” kimesema chanzo chetu.

Kalemani hakuishia hapo. Wazalishaji wa umeme katika maeneo yaliyojitenga na gridi ya taifa (isolated grid) ameagiza wauze umeme kwa Sh 100 kwa uniti. Hakuangalia wamewekeza fedha kiasi gani. Hii imefanya wawekezaji wengi kuitelekeza miradi na wananchi wamerudi gizani katika maeneo ambayo hayana gridi ya taifa na yalikuwa yanategemea wazalishaji binafsi. “Kwa jinsi alivyoshusha, ina maana mwekezaji akakope fedha benki kulipia wananchi umeme, hii haiwezi kutokea,” kimesema chazo chetu kutoka wizarani.

Waziri amekwenda mbali zaidi. “Wabunge wenye masilahi na vinasaba vya mafuta, walimtikisa bungeni, akaamua kuhamishia mchakato wa vinasaba TBS bila kuwapo zabuni. Hapo katikati akataka kulirejesha suala hili wizarani, watendaji wakakataa. Sasa kuna uchunguzi juu ya mchakato ulivyokwenda, yote hii anasema ni ‘maagizo kutoka juu’. 

“Mbaya zaidi, waliomshauri sasa tayari vituo vyao vimekwisha kukamatwa vikiwa vimechakachua mafuta kwa kutumia mafuta ya transit kwa zaidi ya asilimia 30 na vimepigwa faini.

“Walidhani vinasaba vikienda TBS watachakachua bila uangalizi wa karibu. Sasa wamekamatwa wanahaha kila kona wakisema wanatafutwa. Jamani huyu waziri anaiua hii wizara,” kimesema chanzo chetu kingine. JAMHURI bado linaendelea kumtafua Kalemani, japo juhudi hazijazaa matunda.