*Mtandao wa ‘mwendazake’ watajwa kumchimba Rais Samia kuelekea 2025

*Ulikusanya mamilioni wakati wa uchaguzi kutoka kwa wagombea ubunge, udiwani

*Mfanyabiashara tajiri Kanda ya Ziwa atajwa kushikilia fuko la fedha zilizokusanywa

*Mamluki waliounga mkono kushughulikiwa, watajwa kubadilika kulinda masilahi

NA MWANDISHI WETU

DODOMA

Kuna fukuto kubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa kutokana na mtandao uliojengwa na Mwenyekiti, Rais John Magufuli, wakati wa uongozi wake wa miaka mitano na miezi minne Ikulu, ambao kwa sasa unaamini ‘tonge’ linawatoka mdomoni kutokana na mwelekeo mpya wa siasa nchini, JAMHURI limebaini.

Chanzo cha habari cha kuaminika kinasema mtandao huo uliopenyezwa katika siasa na nafasi nyeti katika utumishi wa umma, unajipanga kwa nguvu kubwa na sasa unamchimba chini kwa chini Rais Samia Suluhu Hassan, ukitaka kujenga upya himaya iliyobomoka baada ya kifo cha Rais Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka huu.

“Hawa mamluki waliotoka kusikojulikana wakapewa nafasi kubwa na madaraka katika siasa na utumishi wa umma ndio hatari kubwa kwa sasa. Matukio tunayoyaona yenye lengo la kumhujumu Rais Samia, walianza kujipanga siku nyingi. Kwanza, hawakufahamu kuwa Rais Magufuli angefariki dunia kabla ya kumaliza muda wake.

“Pili, walidhani hata kama angekuwapo ukwasi waliokusanya wangeutumia kumweka madarakani mtu wao wanayemtaka. Tumesikia mara kadhaa wanajigamba kujenga ngome ya kikanda. Wanatukuza ukabila na kuutumia kama nguvu ya kuwaunganisha. Mwalimu [Julius] Nyerere alikemea kwa nguvu kubwa ukabila, lakini kwa bahati mbaya watu aliowaamini Rais Magufuli walikuwa wanaitumbukiza nchi hii katika ukabila.

“Hesabu idadi ya watu aliowapa madaraka katika vyombo na taasisi mbalimbali. Ukisikia Rais ameteua, si kweli kwamba watu wote anakuwa anawafahamu, hapana. Wengine analetewa majina mezani yakiwa yamepambwa kwa sifa nyingi na kutokana na mambo mengi anayokuwa nayo anajikuta ameteua watu kwa ukabila au udini bila yeye kujua. Wasaidizi ni watu hatari sana.

“Wakati wa Uchaguzi Mkuu ilikuwa kufuru. Wapo watendaji wawili ndani ya CCM waliotumia muda huo kukusanya mabilioni. Zaidi ya asilimia 40 ya wabunge na madiwani walipita kwa nguvu na walikusanya fedha kutoka kwao. Ilikuwa wanawahakikishia kuwa ukitoa ‘mzigo’ unapata ubunge au udiwani, na wengi walifanya hivyo.

“Hizi fedha ilikuwa wanazikusanya na kumkabidhi [jina linahifadhiwa] ambaye ni mfanyabiashara mkubwa Kanda ya Ziwa. Na sasa hivi wamefanya vikao wamekubaliana wawe na mradi wa mgombea wao 2025. Ndio hao unasikia kila wanapokuwa wanatoa maagizo na matamko… hawa ni shida kubwa kwa sasa. Ukitaka kufahamu vema mpango mzima mtafute yule kijana aliyetimuliwa pale CCM kwa kukataa kushiriki hujuma. Sasa hivi ameajiriwa katika ofisi nyeti, anayafahamu vema madudu yao hawa watu,” anasema mtoa habari wetu.

JAMHURI limemtafuta kijana huyo, ambaye kupitia kwa mtu wake wa karibu anasema amewasilisha kila kitu kwa wakubwa wafanyie kazi. “Huyu kijana anasema hawa watu walikusanya fedha nyingi mno. Wakipekuliwa utabaini fedha walizonazo hazilingani na mishahara yao. Kwa sasa wamelewa fedha kiasi hata wanadiriki kumdhihaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia. Wanajipanga kwa ajili ya 2025,” amesema.

Kiongozi mwandamizi ndani ya CCM ameliambia JAMHURI: “Tunaufahamu mpango wote na kila kitu tunacho na wanachofanya na wanachopanga kufanya. Kimsingi hawa ni wepesi mno, wala hawatusumbui. Chama ni zaidi ya mtu. Tena washukuru wamepoteza nafasi wakabaki na baadhi, ingeweza kutokea wakapoteza kila kitu.

“Tunafahamu fedha walizokusanya, miradi wanayoitumia kuficha fedha hizo na watu wanaoshirikiana nao. Bahati mbaya au nzuri nchi hii ina watu wenye mapenzi makubwa kwa nchi. Tanzania ni nchi ya amani. Katika hilo kundi wanalodhani wako wamoja, kuna watu wanatuletea taarifa zao na tunawafahamu kwa majina ni kina nani na wamepanga kufanya nini.

“Tunasubiri muda ufike. Tunaona wameanza kutikisa kiberiti, lakini tunawaambia Rais Samia yuko imara na sisi tuko naye asilimia 100. Watanzania wanamuunga mkono. Unafikiri Watanzania wanapenda nchi irudishwe kwenye ile kamata kamata? Unadhani watu wanataka kupiga simu kwa kutumia VPN wakiogopa kusikilizwa?

“Hivi tangu Mama Samia ameingia madarakani unafahamu wafanyabiashara walivyopata nafuu kwa kulipishwa kodi ya haki bila akaunti zao kuingiliwa na kuporwa fedha? Unajua hakuna Mtanzania aliyefikishwa mahakamani kwa kutoa maoni yake mtandaoni? Unajua sasa hivi watu wa kawaida wameanza kukarabati nyumba zao na ujenzi wa nyumba mpya umerejea? Unajua biashara nyingi zilizokuwa zimefungwa sasa zinafunguliwa kwa kasi kubwa?

“Bado tunachunguza hata haya mashitaka dhidi ya [Freeman] Mbowe kama ni ya kweli au ni mpango wa kumchonganisha Mama Samia na wanasiasa wa upinzani. Bahati mbaya Mama hataki kuingilia Mahakama. Ndiyo maana amesema hili la kesi ya Mbowe tuiache Mahakama ifanye kazi yake, lakini tunafuatilia kwa karibu kama haya mashitaka ni ya kweli au ‘yanabumbwa’ kutengeneza maadui?” Kimesema chanzo chetu kingine.

Mitandao ni suala ambalo limekuwa likiibuka ndani ya CCM kila unapokaribika Uchaguzi Mkuu. Mwaka 1985 aliyekuwa Waziri Mkuu, Dk. Salim Ahmed Salim, aliukosa urais kutokana na mtandao ulioongozwa na wakongwe, akiwamo Mama Gertrude Mongella, ambaye anatajwa kuwa nguvu yake ilimwezesha Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Rais wa Zanzibar kuupata urais wa Jamhuri ya Muungano.

Mzee Mwinyi katika hotuba yake ya kushukuru baada ya kuteuliwa kugombea urais, aliashiria ugumu wa mchakato alioupitia, lakini pia akaonyesha kuwa hakutarajia, hivyo akaomba msaada wa Mwalimu Nyerere katika kuiongoza nchi kwa kusema: “Mimi, nikilinganishwa na Mwalimu Nyerere, ni sawa na Mlima Kilimanjaro na kichuguu cha mchwa…”

Mwaka 1995 nayo haikuwa haba. Aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela, alilazimika kujiuzulu wadhifa huo; na Mzee Mwinyi akavunja Baraza la Mawaziri mwaka 1994 baada ya kuwa na harakati zilizoacha mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM, ikiwamo ajenda ya kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika. CCM ilibaki salama hata baada ya mtikisiko huo.

Mzee Mwinyi alimteua Cleopa Msuya kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye naye aligombea urais mwaka 1995, ila akakutana na msukosuko mkubwa wa mtandao wa Jakaya Kikwete, aliyekuwa mshirika wa karibu wa Edward Lowassa enzi hizo wakifahamika kama ‘Boys II Men’, ambao walikitikisa chama na jumuiya zake, ikiwamo Umoja wa Vijana (UVCCM) ukiongozwa na Mwenyekiti wake, John Guninita, aliyeamua kutangaza hadharani mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na UVCCM.

Hata hivyo, hatua ya tatu bora walifikia Mzee Msuya, Kikwete na Bejamin Mkapa. Mzee Mkapa aliibuka mshindi katika uchaguzi ambao unatajwa kama “Maajabu ya White House” Dodoma. Fukuto halikuzimika. Mwaka 2004 joto lilianza kupanda baada ya taarifa kuvuja kuwa Rais Mkapa chaguo lake lilikuwa Dk. Abdallah Kigoda, hivyo wakaanza kumzonga Kikwete.

Katika moja ya vikao vya Kamati Kuu ya CCM Zanzibar, inatajwa kuwa Kikwete aliwatolea uvivu wajumbe na kuwataka waache fitina na hujuma dhidi yake kwani “alilolipanga Mungu, huwa, hata kama wanadamu watajitahidi kulizuia.” Msimamo huo wa Kikwete ulipoza joto na wengi waliishangaa hotuba ya Rais Mkapa ndani ya NEC na Mkutano Mkuu mwaka 2005 aliposema “Hii ni zamu ya vijana.” Kikwete alikuwa anaisaka nafasi ya urais kwa mwavuli wa ujana.

Fukuto ndani ya CCM lilishuhudiwa tena mwaka 2012, ambako ilielezwa kuwa Lowassa anajiandaa kutenganisha kofia mbili; uenyekiti na urais kwa nia ya kupunguza madaraka ya Kikwete. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2012 uliompa ushindi Kikwete ndani ya chama, kampeni za ‘kummaliza’ Lowassa ambazo awali zilitanguliwa na ‘Operation Vua Gamba’ iliyoyeyukia hewani ndani ya CCM, ziliendelea hadi mwaka 2015.

Mwaka 2015 ndio ulikuwa kilele cha misuguano ndani ya CCM ambako kambi kubwa mbili ziliibuka, kwa maana ya ‘Timu Lowassa’ na ‘Timu Kikwete’ na haya yakiwa mapande mawili yaliyotokana na ‘Mtandao’ uliojengwa rasmi mwaka 1995. 

Lowassa alikuwa anagombea urais, huku kambi ya Kikwete ikimuunga mkono Bernard Membe. Baada ya ‘Timu Lowassa’ kuona jina la Lowassa limekatwa katika tano bora, Lowassa alitumia sera ya bora tukose wote.

“Lowassa aliwaambia wafuasi wake wampigie kura Magufuli, na si Membe. Kilichotokea ni historia. Magufuli alipata kura za kimbunga na Membe akapata namba za kiatu. Membe akashindwa kupenya kwenye tatu bora. Hayo ndiyo yalikuwa maajabu mengine ya ‘White House’ Dodoma ambako mgombea ambaye hakuwa na mizizi ndani ya chama alipita katikati ya ugomvi wa mafahari wawili,” kimesema chanzo chetu.

Mtoa habari wetu ameongeza: “Ninachokiona, huu mchezo wa mitandao haujaisha. Rais Magufuli alijitahidi kuleta watu wapya kabisa kutoka nje ya mfumo wa chama akidhani anavunja mtandao wa kisiasa uliokuwa umetandaa ndani ya chama kwa wale waliokuwa wanajiita wafia chama, kumbe bila kujua akawa anajenga mtandao mpya… leo hawa mamluki waliokuja kwa hoja ya kuunga mkono, sasa wameonja asali wameamua kuchonga mzinga.

“Bahati mbaya hawakuwa na uzoefu wala uelewa wa siasa au utumishi wa umma. Kila kitu walifanya kwa maelekezo ya ‘mwendazake’. Yeye alikuwa mzalendo wa kweli na alikuwa anaipigania nchi. Aliamini watu aliowateua, hasa wengi kutoka vyuoni wangekuja na mawazo mapya ya kujenga nchi, ila bahati mbaya wametoka kwenye chaki wakaonja mashangingi, sasa wanaona kuondolewa si haki yao. Wanapambana kwa dhati kurejea mwaka 2025.

“Mimi ninasema hapana, hawa walitufikisha pabaya kama nchi. Kuwaruhusu tena wakashika nchi itatubidi kwanza tuandae sera ya kupanua magereza ya kufungia watu. Hilo ndilo wanalopenda hawa. Hawa ni watu wa visasi, wasio na maarifa, wanaotaka kuchuma fedha, hivyo naomba wanachi wakatae mipango yao. Tumeshuhudia walivyojikusanyia utajiri muda mfupi waliopewa madaraka, leo tukiwapa nchi watatufilisi. Wamwache Mama Samia aende hadi mwaka 2030 na huko atakuwa ameishajenga nchi iliyostaarabika inayofanya siasa za kistaarabu na uchumi imara,” anasema mtoa habari wetu.

Wachambuzi wanasema kundi hilo la ‘mamluki’ waliopewa madaraka na Rais Magufuli, kauli na matendo yao vinapingana dhahiri na msimamo wa chama na Mwenyekiti Rais Samia; suala ambalo walikuwa hawalifanyi wakati wa Awamu ya Tano.

Please follow and like us:
Pin Share