Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inaiangalia sekta binafsi kwa mtazamo chanya wa kuwa mdau muhimu wa uchumi na maendeleo.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipofungua Mkutano mkuu wa kumi na tano(15) wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, uwanja wa ndege Zanzibar tarehe: 19 Februari 2024.

Aidha Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa tayari kazi ya kuandaa sheria inayohusisha maendeleo ya sekta binafsi inaendelea chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikisimamiwa na Sekretarieti ya Baraza la Taifa la Biashara.

Vilevile Rais Dk.Mwinyi amemtaka Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe.Omar Said Shaaban kusimamia kukamilika kwa sheria hiyo mwishoni mwaka huu.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi ametoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kuitangaza Zanzibar katika majukwaa mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa kuvutia wawekezaji wengi zaidi ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali imeanzisha mifumo mbalimbali ya kurahisisha mazingira bora ya kufanya biashara nchini katika kuendana sambamba na maendeleo ya dunia ya sayansi na teknolojia ili kurahisisha huduma za maisha ya wananchi.

Rais Dk.Mwinyi pia ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kufanya biashara kwa misingi ya haki na uadilifu kwa mujibu wa sheria ikiwemo kulipa kodi

By Jamhuri