Serikali idhibiti ukuaji deni la Taifa

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad imeangazia mapungufu kadhaa ikiwamo kupanda kwa deni la Taifa.

Profesa Assad amewasilisha ripoti hiyo bungeni na kuitolea ufafanuzi kwa umma, kupitia mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa Profesa Assad, thamani ya sasa ya deni la taifa ni Shilingi trilioni 34.4 wakati ukomo wa kimataifa ni asilimia 56.

Pia Profesa Assad amesema thamani ya deni la nje pekee kwa pato la Taifa ni asilimia ni asilimia 19.7 wakati ukomo wa kimataifa ni asilimia 40.

Takwimu hizo na nyingine zilizotolewa kwenye ripoti hiyo, zinaendelea kujadiliwa na kutolewa tafsiri na watu wa kada tofauti hususani wachumi.

Yapo maeneo mengi yaliyoanishwa na Profesa Assad kwenye ripoti hiyo iliyoanza kujibiwa na Serikali kupitia kwa mawaziri wa wizara zilizotajwa kuchangia upotevu ama matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kwa hali hiyo, itakuwa vigumu kwetu kupitia eneo moja baada ya jingine la ripoti hiyo, kisha kuitathimini kwenye maoni haya.

Lakini tunaamini kwamba ripoti ya CAG kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/2017 imeibua maeneo mengi yenye kasoro zinazopaswa kushughulikiwa kwa ukali na haraka, ili kuokoa upotevu wa fedha ikiwamo kupitia matumizi yanayoweza kuzuilika.

Upotevu ama matumizi mabaya ya fedha yaliyoibuliwa na CAG ni moja ya viashiria vya kuwapo kwa vitendo vya kifisadi na hujuma dhidi ya rasilimali za nchi.

Tunashauri kwamba moja ya nguvu kubwa inayopaswa kutumika katika utekelezaji wa ripoti ya CAG, ni kudhibiti ukuaji wa deni la taifa na upotevu ama matumizi mabaya ya fedha za umma.

Tunaamini kwa kwa sababu hivi sasa, Serikali ipo katika hatua tofauti za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohitaji  fedha za ndani zaidi ya mikopo kutoka kwa mataifa ya nje.

Hivyo kama upotevu wa fedha uliobainishwa kwenye ripoti ya CAG utadhibitiwa, ni dhahiri kwamba nchi itakuwa na uhakika wa kubuni, kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo na kustawisha maisha ya wananchi.