Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepokea malalamiko ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na Jeshi la Magereza katika kijiji cha Rusumo Wilayani Ngara Mkoani Kagera.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Rusumo Wilayani Ngara Mkoani Kagera baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kutazama mgogoro uliopo baina ya wananchi na Jeshi la Magereza.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, nisikivu hivyo suala hilo la mgogoro huo atalifikisha katika vikao vya kamati ya maamuzi ili liweze kutatuliwa.

“Niwaombe wakazi wa kata na Kijiji hiki cha Rusumo Rais Dk. Samia anawapenda sana na sisi kama wizara tumewekwa kwa ajili ya  kumuwakilisha yeye ili kutatua changamoto zenu, suala hili la Mgogoro huu nimelichukua na tutalishughulikia” amesema Sillo

Naye Mbunge wa Jimbo la Ngara Ndaisaba Ruhoro amesema kuwa, mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya miaka 18 na kwamba umekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli za uzalishaji mali.

“Naibu Waziri Mgogoro huu umedumu kwa zaidi ya miaka 18 sasa nikuombe utusaidie kwani wananchi wanakumbana na changamoto mbalimbali nakushindwa kufanya shughuli zao za uzalishaji mali ili kujiinua kiuchumi” amesema Ruhoro.

Katika hatua nyingine Sillo amesema Serikali ya Tanzania imetenga Dola milioni 100 kwa ajili ya kununua magari ya Zimamoto na Uokoaji hapa nchini ilikukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea.

“Eneo hili la Kituo cha forodha cha mpaka wa Rusumo ni eneo muhimu kwa ajili ya Uchumi wa Taifa letu na linahudumia nchini jirani ya Rwanda hivyo ni muhimu kuwa na vifaa vya utayari kwa ajili ya uokoaji pindi majanga yanapotokea” alimalizia .