Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki amesema Serikali itatumia takribani Sh trilioni 1.2 katika kuboresha elimu ya sekondari nchini.

Kairuki ameyasema hayo wakati wa kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kasisi, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo mara baada kukagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kasisi unaogharimu Sh. milioni 470.

Amesema kiasi hicho cha fedha kitatumika ndani ya miaka mitano ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari(SEQUIP).
Aidha, Kairuki amesema pia Serikali imefanya tathmini ya shule Kongwe za msingi kwa ajili ya kuongezwa madarasa kukarabatiwa na kujengwa upya

Amesema kwa kutambua umuhimu wa elimu hasa katika maeneo ya pembezoni ambapo watoto wanatembea umbali mrefu kufuata elimu, Serikali imeweka mkakati wa kusogeza huduma hiyo karibu na wananachi.

Pia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini kwa kujenga miundombinu ya elimu.

“Tabora pia kuna Watanzania, kuna watoto wanaohitaji huduma, hivi kama atatembea umbali mrefu sana atakuwa na kiwango cha ufaulu unaotakiwa, hivyo kwa kutambua hilo tunasogeza huduma ya elimu karibu na wananchi” amesema Mhe. Kairuki

Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha hakuna kata inakosa shule ya sekondari ili kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata fursa ya upata elimu.

Ametoa rai kwa wananchi kujitoa katika kusaidia shughuli za maendeleo ili kuunga mkono juhudi za Serikali

Amewataka wananchi kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na kuzalisha ili serikali iweze kukusanya mapato kwa ajili ya kuendeelea kuboresha huduma kwa jamii.

Aidha, Kairuki amewaomba wazazi kuwahimiza watoto wao kujikita katika masomo na kuhakikisha wanatoa muda kwa ajili ya kujisomea ili wanachofundishwa waweze kukielewa na kukitumia baadaye na kuwa na kizazi cha wasomi na wanaojitambua.