Polisi Shinyanga wakamata silaha zinazotumika kuendesha uhalifu

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limekamata Bunduki za Kivita AK47 mbili, za kiraia 27(S\gun 9, Riffle 5 pamoja na Gobole 15 zilizokuwa zinatumika kutendea uhalifu. 

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatatu Novemba 21,2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema silaha hizo zimekamatwa kufuatia

misako na operesheni zilizofanywa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha miezi mitatu (3) kuanzia mwezi Septemba 2022 hadi mwezi Novemba 2022.

“Mbali na kukamata silaha hizo pia tumefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya Heroine kidonge kimoja naa kete 10kg, bangi 55kg, mirungi 10kg, mitambo miwili ya kutengenezea pombe haramu ya gongo, Tv tatu, mitungi ya gesi 5, majiko ya gesi 4, computer 3, Subwoofer 6, monitor 3, Darubini 3, king’amuzi kimoja, magodoro 3 na bidhaa mbalimbali za madukani”,amesema Kamanda Magomi.

“Watuhumiwa mbalimbali wanashikiliwa na wengine wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali. Jeshi la Polisi linaendelea kuwaasa wananchi kufuata sheria za nchi wakati wote na kutojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa namna yoyote ile”,amesema.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawaomba wananchi kufika katika kituo kikubwa cha Polisi Shinyanga mjini kwa ajili ya kuzitambua mali zao mbalimbali kuanzia Novemba 23,2022 hadi Novemba 30,2022.

Hayo ameyasema leo kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi wakata akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema tayari watuhumiwa wameshikiliwa na wengine kufikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali.