Serikali kuunganisha mashirika 16, kufuta manne

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali imeekeza kuunganishwa mashirika na taasisi 16 na kufuta mengine manne yaliyokuwa chini ya Msajili wa Hazina ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alipozungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu amuzi huo.

Prof. Mkumbo ametaja mashirika yatakayovunjwa kuwa ni Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi (TPSCF), Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Bodi ya Pareto na Shirika la Elimu Kibaha.

Katika uamuzi huo Shirika la Elimu Kibaha (Kibaha Education Center – KEC) linavunjwa na kuundwa Shule ya Sekondari Kibaha ama kuwa Chuo Cha Ufundi au jina ambalo Mamlaka husika zitaamua.

Prof. Mkumbo alisema “Uamuzi huu utaihamisha Hospitali ya Tumbi Kibaha toka kuwa sehemu ya Shirika la Elimu Kibaha na kuwa Hospitali ya Mkoa wa Pwani.”

Mkumbo amesema kuwa Msajili wa Hazina ameshaelekezwa kukamilisha taratibu za makabidhiano na Wizara ya Afya, hukua akieleza kwa upande mwingine Bodi ya Pareto inafutwa na shughuli zake zitahamishiwa Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CEREAL AND OTHER PRODUCE REGULATORY AUTHORITY-COPRA)”

Kuuhusu mashirika yanayounganishwa, Prof. Mkumbo ameyataja mashirika hayo kuwa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Udhamini, Utambuzi na Ufilisi (RITA), Mengine ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo huku Bodi ya Chai itaunganishwa na Wakala wa Wakulima wa Chai, Bodi ya Nyama ikiunganishwa na Bodi ya Maziwa.

Aidha Profesa Mkumbo amesema Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kitaunganishwa na Mamlaka ya Maeneo ya Uchakataji Mauzo ya Nje (EPZA), kadhalika taasisi za utafiti za Chai, Tumbaku na Kahawa zinaunganishwa kuwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari).

Prof. Mkumbo amesema katika mchakato huo hakuna mtumishi atakayepoteza ajira yake

“Maslahi ya watumishi wa umma katika mashirika na taasisi husika yatalindwa na kuzingatiwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma. Ikumbukwe kuwa mashirika na taasisi nyingi za umma na serikali zina upungufu mkubwa wa watumishi.

Hivyo, watumishi wote ambao mashirika na taasisi zao zinaguswa na zoezi hili watapangiwa kazi nyingine na maslahi yao yatazingatiwa ipasavyo.” Alisema Mkumbo

Aidha mchakato wa kufuta na/au kuunganisha mashirika na taasisi za umma utazingatia sheria ambazo zimeanzisha taasisi hizo.

Mawaziri husika wameshaelekezwa kuhakikisha kuwa mchakato wa kufuta na/au kuunganisha mashirika na taasisi za umma zilizotangazwa uwe umekamilika ndani ya mwaka huu wa fedha.

“Ni kwa sababu hii, uamuzi ninaoutangaza hapa tayari ulishawasilishwa kwa mawaziri husika
ambao ndio wenye nyezo husika (Ministerial Instrument Holder) kwa hatua zao stahiki” Alisema Prof. Mkumbo

Aidha Mkumbo amesisitiza kuwa mageuzi katika utendaji na uendeshaji wa mashirika ya uma ni zoezi endelevu, na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kupima na kutathimini utendaji wa mashirika na taasisi za umma kwa lengo la kuongeza tija katika maendeleo ya nchi.