Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira imesema itashirikiana na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha inawajengea mazingira wezeshi wafanyakazi wa Shirika hilo kwa kuwaondolea vikwazo vinavyoweza kuwasababishia matatizo ya Afya ya akili hali itakayoongeza uwajibikaji.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira Patrobas Katambi, alipokuwa akifungua mkutano wa baraza kuu la 53 la wafanyakazi wa shirika hilo linalofanyika kwa siku mbili kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.

Amesema ili wafanyakazi wafanye kazi kwa bidii lazima kuwe na mahusiano mazuri baina ya viongozi na wafanyakazi na kwamba Serikali ipo tayari kuhakikisha kila mfanyakazi wa shirika anapata haki yake ikiwemo mikataba,malipo,kuongezewa madaraja,usafiri na mawasiliano.

“Ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa watumishi maslahi ya watumishi yanapaswa kupewa kipaumbele , ufanisi wa shirika letu unategemea uzalishaji wa umeme,ili haya yafanyike lazima wafanyakazi wawe na afya ya akili iliyo imara,lazima kuzingatia maslahi yao ili kuwaondolea stres na kuongeza tija na ubunifu,”amesema Katambi

Katambi pia ametumia nafasi hiyo kuwataka watumishi wa shirika hilo kuzingati wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu kabla ya kudai haki zao.

“Kabla ya kudai haki zetu lazima tuangalie wajibu wetu katika maeneo yetu tumeutimiza kwa ukamilifu suala la umeme nchini ni jambo la muhimu sana hivyo tunapaswa kutimiza majukumu yetu ili kuondoa malalamiko ya mgao wa umeme nchini”alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Gissima Nyamo-hanga amesema mkutano wa baraza hilo utafanyika kwa siku mbili ukiwa lengo la kujadilia mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya kiutendaji.

Kadhalika, amesema maagizo yote yalitolewa na Naibu waziri Katambi watayafanyia kazi ili kuongeza ufasi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa watumishi wao.

“Baraza kuu la wafanyakazi ni chombo ambacho pia majukumu yake ni kuangalia maslahi na haki za wafanyakzi hivyo pia katika kikao chetu tutakwenda kujadili masuala ya maslahi kwa watumishi na haki zao”amesema

By Jamhuri