Na Mary Margwe, JamhuriMedia,Simanjiro
Wananchi wa jamii ya Kimasai wametakiwa kuendeleza mila zinazowaunganisha kuwa wamoja na zile ambazo zinasaidia kusukuma Maendeleo chanya na kuwaletea Uchumi imara kwa Taifa.
Hayo yamebainishwa Jana na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka wakati alipokua kwenye sherehe ya kusimikwa kwa mlezi wa Rika la Imegoliki ndani ya Kijiji Cha Londoto Kata ya Msitu wa Tembo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mbunge Sendeka amesema kufanya hivyo kutawasaidia katika kuungana pamoja na Watanzania wengine katika kuleta mabadiliko Chanya yanayoweza kusaidia kushindana na mabadiliko ya Dunia kama ambavyo imekua ikisisitizwa na viongozi wa Kitaifa.
” Nataka niwaombe sana na namna pekee ya kuwasaidia vijana hawa wadogo wa rika ambao leo tunaliandaa kuanza kuwahakikishia Usalama wa ardhi ili baadaye watoto wao waweze kupata nafasi kuendelea kupata urithi na mahali kuanzia maisha” alisema Mbunge Sendeka.
Sendeka amesema hayo Kufuatia risala ya sherehe iliyosomwa na mtoto wa Rika Joseph Baraka ya kumtaka Mbunge Sendeka kuiingilia kati na kuwaweka mbali watu wanaotaka kuchukua eneo lao muhimu la mila, kwani eneo lao la mila za Jamii ya Maa la ” Endonyoo Morwak” ambapo ndipo shughuli za Mila za Jamii hiyo imeasisiwa na zinaendekea kufanyika hapo.
Aidha sambamba na kufuata masuala ya Mila Sendeka amewaomba Wazazi ama walezi kuhakikisha watoto wa kiume na wa kike wanapata elimu sawa hadi ya chuo kikuu na si vinginevyo, maana wapo baadhi ya watu wanadhani mtoto akipata tu e elimu darasa la saba ama ya Sekondari basi itakua ndio mwisho wa kusoma.
” Hapa sio habari kwamba mtoto amemaliza darasa la Saba unasema inatosha hapana, mtoto amemaliza Sekondari unasema inatosha hapana, mtoto amemaliza kidato cha sita au cheti, piploma unasema inatosha hapana, watoto wasome mpaka Chuo kikuu ili tupate wasomi watoto wa kike na wakiume wa jamii ya kimasai, waje washiriki katika kulingoza Taifa letu” amesema Sendeka.
Aidha amesema nia ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa Taifa hili ni kusisitiza nafasi ya vijana hususani ya jamii ya wafugaji hasa watoto wa kike kupata elimu ya juu zaidi ili waweze kutoa mchango chanya kwa ustawi wa jamii anayotokana nayo na Taifa kwa ujumla na si vinginevyo.
“Kwahiyo bado rao yangu kwenu ni kuwaomba kuendelea kuwaomba sana tuwasomeshe watoto wa kike, tuwape haki na nafasi sawa na watoto wa kiume ili kuweza kukabiliana na umaskini usio wa lazima katika jamii zinazotuzunguka, maana hakuna umaskini unaniumiza kama umaskini wa watoto kukosa elimu, alafu unamuona mtoto wa jirani yako amerudi likizo kwao unamuangalia hupati jibu, wakati muda wa watoto wako kusoma ulikua ukiwazuia” ameongeza Mbunge Sendeka.