Na Israel Mwaisaka, JamhuriMedia, Nkasi

SERIKALI wilayani Nkasi imelishukuru kanisa la Assemblies of God (TAG) la mjini Namanyere kwa msaada wa mifuko 10 ya Cementi iliyoitoa kwa ajili ya kuikarabati shule ya msingi Nkomolo ambayo inaitaji ukarabati mkubwa baada ya shule hiyo kuchakaa sana.

Shukrani hizo zimetolewa na mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali kwenye maadhimisho ya miaka 85 ya TAG toka kuanzishwa kwake Nchini na miaka 36 toka lianzishwe Namanyere baada ya kanisa hilo kuyatumia maadhimisho hayo kuchangia ukarabati wa shule hiyo kwa kutoa mifuko hiyo ya Sementi.

Amesema kuwa serikali ipo bega kwa bega na taasisi za dini katika kuhakikisha Maisha ya jamii yanaboreshwa na kuwa kitendo cha kanisa kuunga mkono jitihada za wananchi katika kujiletea maendeleo ni jambo la busara na la kuigwa na taasisi nyingine ikiwa ni pamoja na watu binafsi.

Hivyo ameutaka uongozi wa shule na Kijiji cha Nkomolo kuhakikisha kuwa sementi hiyo inatumika sawa katika kukarabati shule na kazi yake ionekane na kuwa kufanya hivyo kutwawpa nguvu kanisa hilo na kuona kuwa walichokitoa kimefanya kazi kusudiwa kama yalivyokuwa malengo ya kanisa.

Lijualikali amedai kuwa TAG Nkomolo wamefungua ukurasa kwa dini nyingine katika kuona kwamba suala la kuchangia maendeleo kwa ajili ya ustawi wa jamii ni jukumu lao na kila mmoja badala ya kuachia serikali ifanye kila kitu.

Awali mchungaji wa kanisa hilo Efraimu Lyandulu alisema kuwa kanisa hilo limetimiza miaka 85 toka kuanzishwa kwake na wao walionelea katika maadhimisho hayo kuchangia ukarabati wa shule ya msingi Nkomolo mifuko 10 kama sehemu ya kuchangia nguvu za Wananchi ambazo wamezianza katika uboreshaji wa shule hiyo.

Alidai kuwa kanisa hilo kwa muda mrefu limekua mstari wa mbele katika kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kufanya matendo ya huruma kama kuwatembelea Wafungwa magerezani ,Wagonjwa hospitalini,kujitolea damu,kuwaona Watoto yatima na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Mwenyekiti kiongozi wa Kijiji cha Nkomolo Sitivini Tontololo amelishukuru kanisa hilo kwa msaada huo na kuwa yeye hiyo ni mara ya kwanza kuona kanisa linajitoa kuisaidia serikali kama TAG walivyofanya na kuwa hicho ni kitendo cha kuigwa na kuwa huo ni mwanzo mzuri kwa taasisi za dini.

Na amedai kuwa kama kiongozi atahakikisha sementi hiyo inafanya kazi ya kuonekana katika jamii ili kuweza kuwatia moyo waumini na viongozi wa dini hiyo ili kuona kwamba kile walichokitoa kinathaminiwa na kimetoa mchango katika jamii.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Richard Kasomo amesema kuwa kitendo kilichofanywa na kanisa hilo na kuamua kuisaidia shule hiyo ni jambo kubwa na kuwa na wao kama Walimu kimewatia moyo cha wao kuendelea kufanya kazi kwa bidi kwani kumbe kazi yao inathaminiwa na jamii

By Jamhuri