Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza wakati wa kikao na ujumbe kutoka mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali ya The Pew Charitable Trusts (PEW) na Wetlands International (WI) kwa lengo la kuainisha fursa zilizolopo kwenye uhifadhi wa maeneo ya fukwe,  jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Shirika la The Pew Charitable Trusts (PEW) Bw. Simon Reddy akifafanua jambo wakati wa kikao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo  jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la The Pew Charitable Trusts (PEW) Bw. Simon Reddy (kushoto) na Bi. Julie Mulonga kutoka Wetlands International (WI) kwa lengo la kuainisha fursa zilizolopo kwenye uhifadhi wa maeneo ya fukwe,  jijini Dodoma.

……..

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali itaendelea kufungua milango kwa wadau wenye nia ya kuchangia katika hifadhi endelevu ya mazingira.

Amesema hayo wakati wa kikao na ujumbe kutoka mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali ya The Pew Charitable Trusts (PEW) na Wetlands International (WI) kwa lengo la kuainisha fursa zilizopo kwenye uhifadhi wa maeneo ya fukwe, Aprili 17, 2024 jijini Dodoma.

Dkt. Jafo amewashukuru wadau hao kwa kutambulisha mradi huo hususan katika eneo la mifumo ya ikolojia ya mikoko na nyasi bahari kwa faida za kutunza bioanuai na kukabiliana na athari mabadiliko ya tabianchi.

Amesema taarifa za kitafiti zitakazotokana na mradi huo zitasaidia katika maandalizi ya taarifa ya nchi kuhusu mchango wa kitaifa wa kupunguza gesi joto duniani (NDC).

“Tutambue Tanzania imedhamiria kupunguza uzalishaji wa gesijoto kwa asilimia 30 hadi 35 ifikapo mwaka 2030, hivyo mchango wenu utasaidia katika eneo hilo,“ amesema Dkt. Jafo huku akiwahakikishia kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuwapa ushirikiano mkubwa ili kufika malengo katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa vizuri na kuwa endelevu.

Awali Mkurugenzi wa PEW Bw. Simon Reddy ameelezea mkakati wa shirika hilo katika kushirikiana na WI kutekeleza mradi huo katika maeneo ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Ameomba ushirikiano kutoka serikalini ili kufikia malengo katika kuhakikisha utekelezaji wa mradi unakuwa wa mafanikio kama unavyotekelezwa katika nchi zingine.

Pia, Bi. Julie Mulonga kutoka WI shirika hilo limejikita zaidi katika kusaidia katika kuendeleza hifadhi pamoja na kurejesha uoto wa asili hapa nchini. 

Amesema tangu walipoanza shughuli zao wametoa mchango wao katika kupitia mpangokazi wa kuendeleza maeneo ya mikoko hususan katika Delta ya Rufiji.

Kikao hicho kimewahusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).