nmb-4Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Julius Ningu, amesema kuna haja kwa nchi kuweka mifumo thabiti ya kudhibiti vifaa mbalimbali vyenye madini ya zebaki.

Dk. Ningu ameeleza hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa wadau, uliolenga kujadili na kuandaa mapendekezo ya Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Matumizi ya Zebaki (MINAMATA) uliofikiwa huko Uswisi Januari 2013.

Amesema kuwApo kwa mifumo hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti matumizi ya madini hayo, ambayo yamekuwa yakileta athari kubwa kwa binadamu ikiwAmo matatizo ya kiafya, kuzaliwa watoto wenye upungufu wa viungo, watoto wenye mtindio wa ubongo pamoja na matatizo mengine kwa viumbe vingine.

“Kuondokana moja kwa moja na matumizi ya zebaki ni ngumu, cha muhimu tunachofanya ni kuielimisha jamii hasa ya wachimbaji wadogo wanaoitumia ili kutafuta njia mbadala ya kuhakikisha zebaki haileti madhara kwao, wachimbaji wakubwa hawaitumii katika shughuli zao,” amesema Dk. Ningu.

Ameongeza kwamba zebaki ina athari kubwa kwa maisha ya binadamu, hivyo wao kama Serikali wanaangalia madhara ya muda mfupi na mrefu wa madini hayo pamoja na kuangalia njia mbadala zitakazosaidia kupunguza matumizi yake.

Ameeleza kwamba uwepo wa madini hayo si wa hapa nchini pekee kwa sababu Tanzania si wachimbaji bali huyaagiza kutoka nje kihalali na wakati mwingine kuingizwa kwa njia zisizokuwa halali, hivyo kupitia mkataba wa Minamata ambao Tanzania imeuridhia watashirikiana na nchi nyingine wanachama kuzuia matumizi yake. 

Naye mkuu wa Sehemu ndogo ya Chakula Salama, Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kiberiti, amesema Serikali inaandaa mkakati wa kubadili vifaa tiba vyenye viambata vyenye madini ya zebaki ili kulinda afya ya jamii.

Katika mahojiano yake na JAMHURI, Kiberiti ambaye katika mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira ufadhili wa Shirika la Kimataifa la UNEP, amesema mkakati huo umelenga kuhakikisha afya za binadamu zinakuwa salama.

Amesema Wizara ya Afya inashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais kuhakikisha wanalinda na kuhifadhi mazingira kwa ajili ya ustawi wa jamii, na kwamba mikakati iliyopo ni kuhakikisha wanabadili vifaa tiba hivyo kwa maslahi ya Taifa. Amevitaja baadhi ya vifaa tiba vyenye viambata hivyo kuwa ni vipima joto, vipimo vya kifua ambavyo kwa sasa vimeanza kubadilishwa kuwa ni pamoja na kuacha kujaza meno yaliyotoboka kwa kutumia madini hayo na vingine badala yake kutumia madini mengine yakiwamo ya shaba.       

Tanzania iliridhia mkataba huo wa Minamata Oktoba 10, 2013 na kuongeza nguvu kwa nchi nyingine zilizouridhia kama njia ya kuzuia matumizi ya zebaki.

2931 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!