Lubuva, wahariri mambo safi

nmb-4Wahariri wa vyombo vya habari nchini wameagizwa kufuata maadili ya taaluma sambamba na sheria za uchaguzi, ili kuepuka kupitisha habari kutoka vyanzo visivyo rasmi.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, amewaambia wahariri kwamba wana dhamana kubwa ya amani ya Tanzania sasa, wakati wa Uchaguzi Mkuu na baada ya mchakato huo.

“Ndugu zangu, muda uliobaki kuelekea Uchaguzi Mkuu ni mfupi mno,” anasema Lubuva na kuongeza; “Dhamana ya amani ipo kwenu na kwetu.”

Katika mkutano huo ulioanza kwa kuwakutanisha wamiliki kabla ya wahariri na makundi mengine, Jaji Lubuva alionya kuandikwa kwa habari za upendeleo na kuwa “uandishi wa namna hii hauusaidii umma.”

Akihojiwa na Gazeti JAMHURI, Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri, Neville Meena, anasema, “Tumemsikia Jaji Lubuva lakini tunamuomba tufanye kazi kwa karibu ili kuepuka hayo aliyoyasema”.

Meena, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, anasema: “Hakika hiki ni kipindi cha mawimbi mazito ya kisiasa na siasa za Tanzania zimebadilika sana. Tufanye kazi kwa ushirikiano.”

Anasema kwamba uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na miaka 20 iliyopita kwa kuwa umejaa ushindani wa hali ya juu na kusema ni bora wamekutana na NEC na kuweka kupishana kwao sawasawa.

Awali NEC ilionekana kama kushutumu vyombo vya habari kwa kuripoti kauli mbalimbali za viongozi wa kisiasa ambazo wakati mwingine zinaashiria uvunjifu wa amani.

Jaji Lubuva ameongeza kuwa ni vyema wananchi wakafahamishwa kuwa baada ya kumaliza kupiga kura kituo hicho kinabadilika na kuwa kituo cha kujumlishia kura na mawakala wote wa vyama wanasaini fomu ya matokeo na baadaye yanabandikwa kituoni, hivyo hakuna haja ya wananchi kubaki vituoni baada ya kupiga kura na badala yake warudi nyumbani kusubiri matokeo kupitia vyombo vya habari.

Wahariri hao wameelezwa kuwa wana wajibu wa kuripoti matokeo kwa kadiri yalivyobandikwa vituoni na si kumtangaza mshindi, kwani mwenye dhamana hiyo kwa mujibu wa sheria ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi. 

 Jaji Lubuva amewataka wagombea wa vyama vyote vya siasa kunadi sera zao jukwaani na iwapo wameishiwa na sera wakae kimya kusubiri siku ya kupiga kura badala ya kutoa lugha za kejeli, kukashifiana na matusi pamoja kukoma kuhamasisha wananchi kulinda kura zao.