Gazeti la JAMHURI Toleo namba 581 la Novemba 15-21, 2022 lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari kilichosomeka “Mgonjwa wa homa ‘anyweshwa’ dawa ya upele”.

Habari hiyo ilimuhusu mwanamke (50) aliyekwenda kutibiwa homa katika Hospitali ya Misheni Bwagala iliyoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro kunusurika kifo baada ya kunywa dawa ya upele.

Kutokana na taarifa hiyo iliyotolewa leo Novemba 17, 2022,Serikali kupitia ofisi ya Baraza la Famasia imetoa tamko na ufafanuzi juu ya taarifa hiyo na kukiri kutokea kwa kitendo hicho na kusema kuwa aliyetoa dawa hizo ni mwanafunzi wa ngazi ya cheti ambaye alikuwa kwenye mafunzo

“Katika ufuatiliaji wa awali, imebainika kuwa mhusika aliyetoa dawa hizo ni mwanafunzi wa ngazi ya cheti (Astashahada – NTA L5) kutoka Chuo cha Hermargs Institute ambaye alikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo (field) katika Hospitali ya Turiani St. Francis, Mvomero.

“Kiutaratibu mwanafunzi anapokuwa kwenye mafunzo anapaswa kuwa chini ya usimamizi na uangalizi wa mwanataaluma ambaye amesajiliwa na kutambuliwa na Baraza la Famasi.” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Msajili Baraza la Famasia, Elizabeth Shekalaghe.

Soma:  Mgonjwa wa homa ‘anyweshwa’ dawa ya upele

Aidha Serikali imewaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu katika kipindi ambacho suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi huku ikiahidi kuwachukulia hatua kali wote waliohusika na uzembe huo.

“Kutokana na kuwepo kwa taarifa hizi, Ofsi ya Msajili inawaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati suala hili linaendelea kufanyiwa kazi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wote watakaobainika kuzembea katika kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kitaaluma.” amesema Shikalaghe

Vilevile wito umetolewa kwa wasimamizi wote wa wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo katika taaluma ya famasia ngazi zote kufuata na kuzingatia taratibu za usumamizi wa wanafunzi hao ili kuepukama na kusababisha madhara

“Natoa wito kwa wasimamizi wa mafunzo ya vitendo (field) katika taaluma ya famasi ngazi zote kuzingatia taratibu za usimamizi wa wanafunzi wanapokuwa katika mafunzo ili kuepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na utoaji wa dawa usio sahihi na kusababisha athari kwa wagonjwa.” amesisitiza Shekalaghe.

Mnamo Alhamis ya Novemba 4, 2022 Mfamasia “Aliyetajwa kama Mwanafunzi kwa Vitendo” katika hospitali ya Turiani St. Francis Mvomero alimpa mgonjwa wa homa “Mwanamke” (50) dawa ya upele ‘Lindane Scoboma Lotion’ kwa maelekezo ya kuinywa kwa kipimo cha mils 10×2 kwa siku, ambapo dawa hiyo baadaye ilimsababishia madhara mgonjwa huyo manusura apoteze uhai mpaka pale alipopata usaidizi kutoka kwa majirani.

Dawa ya Lindane Scoboma Lotion ni nini?

Lindane Scaboma Lotion dawa ya kupaka kwenye ngozi inayotibu upele

Kwa Mujibu wa tovuti ya Appollo Pharmacy Lotion ya Scaboma ni aina ya kundi la dawa za kuzuia vimelea vinavyosabaisha ugonjwa wa ngozi kama vile upele na hutumika kupaka kwenye ngozi na si kunywa kwa mgonjwa mwenye vimelea hivyo mara baada ya kupimwa na kupewa maelekezo na daktari.