Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (MB) ametembelea banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) lililopo katika maonesho yaliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa lengo la kutangaza kazi za taasisi mbalimbali zilizopo chini ya wizara hiyo kupitia mkutano wa 15 wa wadau wa kutathmini utendaji kazi wa sekta ya uchukuzi kwa mwaka mmoja.

Mbarawa akiambatana na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Africa (AFDO) Dkt. Patricia Laverley, wameelezwa umuhimu wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya ujenzi na uchukuzi ikiwa ni pamoja na huduma mahususi za usafiri wa barabara, maji na anga.

Aidha,kupitia maonesho hayo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA,Wilbert Muruke alizungumza na vyombo vya habari na kuelezea umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya uchukuzi jinsi zinavyosaidia katika kutekeleza majukumu ya sekta vilevile kukabiliana na athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa.

“Kama mnavyoelewa huduma za hali ya hewa ni mtambuka kwa sekta mbalimbali mojawapo ya sekta ambayo tunaihudumia ni sekta ya usafirishaji ambapo katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo viwanja vya ndege.

“Pia reli, barabara na madaraja moja ya taarifa muhimu katika mipango yao ni taarifa za hali ya hewa zitakazowawezesha kupanga vyema mipango yao na hivyo kusaidia kuepusha hasara zitakazojitokeza kutokana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa” amesema Muruke.

Muruke ameongezea kwa kuwataka wadau kuendelea kufuatilia taarifa mbalimbali za hali ya hewa zinazotolewa mara kwa mara na TMA hususani katika kipindi hiki ambacho dunia imeendelea kukumbwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Hii itasaidia kupunguza au kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na hali mbaya ya hewa

By Jamhuri