Uzinduzi sera ya ubia utaongeza kasi ya maendeleo NHC,Taifa

Na Stella Aron, JamhuriMedia

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika uzinduzi wa Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwenye  Kituo cha Mkutano cha Kimataifa cha Julius. Nyerere jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2022. 

Serikali imeliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),kusimamia imara miradi itakayoingia ubia na wawekezaji ili kutekelezwa kwa ufanisi na tija ili miradi itakayotekelezwa, itekelezwe kwa ufanisi na tija kwa taifa na mwekezaji husika.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizindua Sera ya Ubia ya NHC iliyofanyiwa marekebisho kwa lengo la kuweka uwazi na kuongeza tija katika miradi ya ujenzi wa nyumba baina ya shirika hilo na sekta binafsi.

Waziri Majaliwa amesema kuwa Serikali ingependa kuona wawekezaji na NHC wanajenga ubia imara utakaosaidia ukuaji wa sekta ya nyumba ambayo ni moja ya sekta muhimu nchini.

“Ni vizuri NHC kwanza ikachambua kwa umakini aina ya wawekezaji watakaoleta maombi ya ujenzi wa nyumba na kuingia ubia imara ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema kuwa Serikali itakuwa karibu katika kuhakikisha wawekezaji wanaopata miradi ni wale wenye sifa na sio wale wawekezaji wababaishaji.

“Ni vizuri NHC mkasimamia miradi hii ili iendane na thamani ya fedha iliyokusudiwa kwa kuepuka majengo kujengwa kwa kiwango cha chini ikiwamo kuanguka na kuleta madhara kwa wananchi, lakini pia hasara kwa taifa,” amesema.

Ameongeza kuwa katika miji mingi ukiwamo Dar es Salaam, kwa sasa kuna majengo mengi na hakuna nafasi za kutosha za maegesho ya magari na kuiagiza NHC katika miradi yake ya ubia na wawekezaji kujenga pia majengo ya maegesho ya magari.

Waziri Majaliwa ameeleza kuwa sera hiyo imefanyiwa maboresho makubwa ili kukidhi mahitaji na kuwa na tija kwa wawekezaji jambo litakaloleta faida ikiwamo kuufanya ubia husika kuwa endelevu na wenye manufaa kwa umma.

Amesema kuwa tangu kuanza kwa Sera ya Ubia miaka 2012 iliyopita, shirika limeingia mikataba 194 na sekta binafsi ambapo mikataba 73 ilifutwa kwa sababu ya ukiukwaji wa masharti, mikataba 111 yenye thamani ya shilingi bilioni 300, utekelezaji wake umefanyika ambapo mikataba 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 240 utekelezaji wake umekamilika na mikataba 30 yenye thamani ya shilingi bilioni 60 utekelezaji unaendelea.

“Serikali inatambua makazi ni jambo muhimu kwa maendeleo ya taifa, ndiyo maana imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuwezesha sekta ya nyumba kuwa endelevu na yenye tija kwa wananchi na uchumi wa nchi,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Nehemia Mchechu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba NHC nakala ya Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumbna la Taifa (NHC) baada ya kuzindua Sera hiyo  kwenye   Kituo cha Mkutano cha Kimataifa cha Julius. Nyerere jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2022. Katiakati ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makala na Katibu Mkuu wa Wizara ya  Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi.

Waziri Majaliwa amesema takwimu zinaonesha kuwa nchini kuna uhaba wa nyumba milioni tatu na mahitaji hayo yanaongezeka kwa wastani wa nyumba 200,000 kila mwaka.

Alibainisha kuwa upungufu huo unachangia wamiliki wa nyumba binafsi kutoza kodi kubwa na wakati mwingine kudai kodi ya mwaka mzima kwa mkupuo mmoja.

“Lengo la serikali ni kuwezesha wananchi wengi zaidi kumiliki nyumba zinazojengwa na shirika hili na waendelezaji wengine wa nyumba.

Ameongeza kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la mikopo iliyotolewa ya uendelezaji miliki ikiwamo mikopo ya nyumba ambapo hadi kufikia Septemba, mwaka huu, NHC imewezesha benki na taasisi za fedha 33 kutoa mikopo ya nyumba ya Sh bilioni 147.7 kwa wananchi 6,177.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula nakala ya Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) baada ya kuzindua Sera hiyo  kwenye   Kituo cha Mkutano cha Kimataifa cha Julius. Nyerere jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2022. 

Amesema matokeo ya mafanikio hayo yamewezesha kuongezeka kwa mchango wa sekta ya miliki katika Pato la Taifa.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo,Mkurugenzi wa NHC, Nehemia Mchechu amesema shirika hilo limefungua milango kwa wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi hivyo anaamini kuwa ubia huo utasaidia kupunguza changamoto mbalimbali walizokuwa wakikabiliwa nazo za mrundikano wa maombi ya wapangaji.

“Tumeanzia hapa Dar es Saalam tuna wiki tatu za kuelimisha na kufanya mafunzo kila kwa wafanyabiashara kuwaeleza nini kinafanyika katika sera hii kisha titaenda mikoa ya Mwanza na Arusha lakini baadae tutangalia ratiba ili tuweze kuwafuata baadhi ya wawekezaji wa nje ya nchi,” amesema Mchechu.

Mchechu ameongeza kwamba sekta hiyo ina manufaa mengi sana kwani kila mmoja wetu anahitaji nyumba bora kwa ajili ya kuishi na kwa sasa Watanzania wapo wengi hivyo shirika pekee haliwezi kujenga nyumba za kutosheleza uhitaji ndio maana NHC imeamua kushirikisha sekta binafsi katika miradi yake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Uzinduzi wa   Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakionyesha nakala za sera  hiyo iliyozinduliwa na Waziri Mkuu  kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere  Jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2022.  Kutoka kushoto ni  Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makala, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Dkt. Angelina Mabula, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi, Mwenyekiti wa Bodi ya NHC, Dkt.  Sophia Kongeli na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu.

Ameongeza kwamba shirika hilo linaendelea na mradi wa ‘Samia House Scheme’ ambapo nyumba hizo zinajegwa Kawe na mwezi ujao zitaanza kujengwa Dodoma na mikoa mingine lakini pia miradi yote itaendelea bila kusita.

“NHC itafanya vikao na benki mbalimbali ili wawe tayari kuwakopesha wajenzi pamoja na wanunuzi wa nyumbani hizo wenye vigezo vinavyotakiwa,” amesema.

Hata hivyo amesema kuwa sera za uwekezaji kwa NHC imeweka sera rafiki ambazo zipo wazi na mwekezaji atakaa na kukubaliana na shirika kabla ya kuanza kuwekeza ili kufahamu nini anachotakiwa kufanya na nini mafanikio kwake na Serikali.

Amewatoa hofu wawekezaji kwa kutokuwepo kwa urasimu wowote pindi watapokwenda ofisi za NHC kwa nia ya kufanya uwekezaji kwenye miradi kwa kuelimishwa na namna bora ya kuwekeza bila ya kufanyiwa utapeli ili miradi iweze kufanyika kwa wingi na kuongeza pato la Taifa kwa maslahi ya Watanzania.

Msechu amesema kuwa Sera imeboreshwa kwa kuongeza vitu vikubwa vinne ikiwemo kutumia ardhi kama mtaji, sera nyingine ni NHC inaweka ardhi na mbia anaweka fedha halafu wanatekeleza mradi kwa pamoja na hii ni kwa miradi mikubwa ya kuanzia sh.bilioni 50.

Nehemia Mchechu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba NHC akizungumza wakati wa uzinduzi wa Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  kwenye  Kituo cha Mkutano cha Kimataifa cha Julius. Nyerere jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2022. 

Ametaja sera nyingine kuwa ni kujenga jengo kati ya shirika na wabia kisha kuuzwa na mapato kugawanywa na sera ya mwisho ni shirika kutoa ardhi kwa mkataba wa miaka 10 na mbia anajenga, baada mkataba kuisha jengo linakuwa mali ya shirika.

“Sera hii ina lenga kuwapa fursa wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini, ambapo itafungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba ili kuunga mkono maono maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binfasi ambayo ni injini ya kuleta maendeleo ili iwekeze mitaji yao katika kujenga uchumi wa Taifa letu,” amesema Msechu.