Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeongeza Tahasusi (Combination) mpya 49, kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia Tahasusi 65.

Tahasusi hizo mpya zitakazoanza kutekelezwa Julai, 2024 zipo katika makundi saba (7) ambayo ni Tahasusi za Sayansi ya Jamii, Tahasusi za Lugha, Tahasusi za Masomo ya Biashara, Tahasusi za Sayansi, Tahasusi za Michezo, Tahasusi za Sanaa, na Tahasusi za Elimu ya Dini.

Hayo yamebainishwa leo Machi 20, 2024 jijini Dar es Salaam, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohammed Mchengerwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2023 kufanya mabadiliko ya Tahasusi za kidato cha Tano na kozi za vyuo Kwa njia ya mtandao kwenye mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha Tano na vyuo mwaka 2024.

Waziri Mchengerwa amesema Tamisemi imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye Fomu za Uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni.

“Napenda mtambue kuwa Mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 na Mitaala ya Elimu kwa Kidato cha Tano yameanza kutekelezwa, ambapo utekelezaji huo umehusisha uanzishaji wa Tahasusi mpya 49, kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia tahasusi 65.

“Kukamilika kwa zoezi hili kunatoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya mabadiliko ya machaguo/ tahasusi/ kozi kwa njia ya mtandao (online). Baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao,” amesema Mchengerwa.

Amebainisha kuwa, zoezi la kubadilisha tahasusi na vyuo limeanza rasmi leo Machi 20 hadi Aprili 30, 2024 huku akitoa wito kwa Wanafunzi, wazazi na walezi kushauriana kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalam na kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au Kozi.

Amefafanua kuwa, Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi na Kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi (Selform).

“Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

“Kwahiyo Ofisi ya Rais TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Nne mwaka 2023 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa Mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalam stahiki katika maisha yake ya baadaye. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wakati wa ujazaji wa fomu za machaguo ya awali, tahasusi mpya 49 hazikuwepo kwenye orodha ya machaguo na pia matokeo ya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne hayakuwa yametoka kumuwezesha mwanafunzi kuweza kuwa na machaguo mazuri zaidi kulingana na ufaulu wake,” amesema.

Ameongeza kuwa, zoezi hilo litatoa fursa zaidi ya wanafunzi kuongeza machaguo na kufanya machaguo mapya ya Tahasusi na Kozi.

“Kwa umuhimu huo, wahitimu wote wanahimizwa kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao, kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS) unaopatikana kupitia kiungan cha selform.tamisemi.go.tz.

“Aidha, maelekezo kwa wahitimu na jinsi ya kufanya mabadiliko yanapatikana kwenye mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi. Ili kuingia kwenye mfumo itabidi mhitimu atumie Namba ya Mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2023, Jina lake la Mwisho, Mwaka wa Kuzaliwa na Alama ya Ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa,” amesisitiza.