Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefanikiwa kuwawezesha Watu wasioona hususan katika eneo la Ajira, Michezo na TEHAMA.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, amebainisha kuwa serikali kupitia Mwongozo wa Viwango vya Vifaa vya TEHAMA wa mwaka 2020 umejumuisha mahitaji ya watu wasioona ili kuweka mazingira rafiki kwenye Ofisi za Umma na maeneo ya kutolea huduma kwa wananchi.

Ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Watu wasioona Kitaifa yaliyofanyika Babati Mjini, Mkoani Manyara jana Oktoba 21, 2022.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ujumuishwaji wa Watu Wasioona katika Ajira, Michezo na Tehama kwa Maendeleo Endelevu”.

Amebainisha kuwa Serikali imeendelea kutoa Ajira kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye ulemavu wa kutoona ambapo kwa mwaka 2022 Ajira zilizotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI za Kada ya Walimu nafasi 9,800 na Kada za Afya 7,612 jumla ya Watu wenye Ulemavu 261 sawa na asilimia 2.7 walikidhi vigezo na kupata ajira ya ualimu.

“Kati ya hao 261 watu wasioona walikuwa 61 (Ke. 13 na Me.49). iIlevile, kwa upande wa Kada za Afya jumla ya Watu wenye Ulemavu 42 walikidhi vigezo na kupata ajira ambapo miongoni mwao wasioona walikuwa wanne (4) Ke. 1 na Me.3”

Katambi amefafanua kuwa Serikali inatambua na kutoa kipaumbele kwa masuala ya watu wenye ulemavu, ambapo tayari imezindua Mwongozo wa Taifa wa Utambuzi wa Mapema na Afua Stahiki kwa Watoto wenye Ulemavu.

“Lengo kuu la kuzindua mwongozo huu ni kusaidia kuwatambua watoto wenye ulemavu na kusaidia kuweka mipango mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya ili kuwapunguzia makali ya ulemavu na pengine kuuondoa kabisa” amesema.

Aidha,Katambi ameongeza kuwa Serikali imeona ipo haja ya kuhakikisha Watoto wenye ulemavu wanapata elimu kama watoto wengine wasio na ulemavu na hivyo kutunga Sera ya Elimu Jumuishi, hii ni hatua ya kuhakikisha kuwa Watoto wenye ulemavu wa kawaida wanaweza kupata elimu pamoja na watoto wengine katika maeneo yao.

Mhe Katambi amesisitiza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutoa vifaa saidizi. Kwa mwaka jana wa fedha (2021-2022), Serikali imeweza kutoa fimbo nyeupe na vifaa vingine muhimu katika kuwasaidia watoto wasioona kuweza kujifunza.

“Vifaa vilivyotolewa ni: Fimbo nyeupe 50 kupitia Ofisi hiyo, miwani kwa wanafunzi 174, Essilor glasses 174, miwani yenye lenzi inayobadilika kulingana na mionzi ya jua 172, monocular 268, makasha ya miwani 183, mabegi 341 kupitia mdau Standing Voice na wengine wengi mnaosaidia katika kutoa huduma mbali mbali”

By Jamhuri